Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chongolo awapa somo Kilimanjaro

Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo akiwa katika ofisi za chama hicho za wilaya ya Siha wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Kilimanjaro leo. Picha ya Ericky Boniphace

Muktasari:

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amewataka wananchi mkoani Kilimanjaro kutumia fursa za utalii zilizopo kubuni miradi ya kiuchumi ili kujiongezea kipato na kuondokana na umasikini.

Hai. Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amewataka wananchi mkoani Kilimanjaro kutumia fursa za utalii zilizopo kubuni miradi ya kiuchumi ili kujiongezea kipato na kuondokana na umasikini.

Chongolo ametoa rai hiyo leo Jumanne Agusti 2, 2022 wakati akizungumza na wananchi wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi, ambapo amesema kwa sasa utalii umefumuka.

"Natambua watu wengi kwa sasa wanafanya kazi ya utalii na wamenufaika, utalii kwa sasa umefumuka wageni ni wengi sana, jana pekee zaidi ya wageni 800 wameingia ni idadi kubwa, ni wakati wa wananchi sasa kutumia fursa hiyo ya utalii kuchapa kazi ili kujikwamua kiuchumi," amesema

"Haya ni mabadiliko makubwa ndani ya nchi yetu, ambayo yanetokana na filamu ya Royal Tour iliyotengenezwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ambapo aliitangaza nchi kimataifa, sasa kila mmoja aangalie fursa kutokana na utalii."

Amesema ifike wakati sasa wachaga kuiga mfano wa wale wa kimasai, ambao wamekuwa wakijiunga vikundi na kutengeneza shanga na bidhaa nyingine za utalii, ambazo huwaongezea kipato na kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.

"Angalieni fursa hizi za utalii na tufike mahali sasa wachaga nao watengeneze vikundi vya utalii kama vile vya utamaduni na asili, waige wale wamasai ambao hutengeneza bidhaa mbalimbali ikiwemo shanga, msihangaike tu na mikungu ya ndizi, sasa changamkieni fursa".

Akizungumza katika mkutano huo, mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya Uviko-19 na wale ambao hawajachanja, wahakikishe wanapata chanjo.

"Niwasihi wananchi, tuendelee kuchukua tahadhari juu ya Uviko-19, wale ambao hamjachanja, hakikisheni mnachanja kwani Serikali imeendelea kuhakikisha chanjo zinapatikana ili kuendelea kuwa salama dhidi ya ugonjwa huu"