Chui aliyevamia makazi Musoma auawa

New Content Item (1)
Chui aliyeonekana kwenye makazi ya watu katika Manispaa ya Musoma akiwa ameuwawa na kikosi cha kuzuia wanyama waharibifu kabla hajaleta madhara kwa watu na mali zao. 

Muktasari:

Chui ambaye hajafahamika mahali alipotekea amevamia makazi ya mtu katika Manispaa ya Musoma na kuleta taharuki kabla ya kuuwawa na kikosi cha kuzuia wanyama waharibifu.

Musoma. Kikosi cha kuzuia wanyama waharibifu kutoka wilaya ya Bunda mkoani Mara  kimefanikiwa kumuua chui aliyevamia makazi ya watu katika manispaa ya Musoma kabla hajaleta madhara.

Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk Halfan Haule amesema chui huyo ameonekana leo Machi 24, 2023 Saa tatu asubuhi akiwa ndani ya uzio wa moja ya nyumba iliyopo Mtaa wa Rwamlimi Manispaa ya Musoma ndipo wananchi kutoa taarifa kabla hajaleta madhara.

“Alionekana kwenye mji wa mtu mmoja pale Rwamlimi akiwa tayari ameingia ndani ya uzio na kujificha kwenye kona mle ndani na baada ya kuonekana wananchi walitoa taarifa,”amesema

Amesema baada ya kupata taarifa hizo waliwasiliana na kikosi cha kuzuia wanyama waharibifu kilichopo wilayani Bunda kwaajili ya msaada wa haraka ambacho kilifika mapema na kufanikiwa kumuua chui huyo.

Amesema  ingawa hadi sasa bado haijajulikana chui huyo ametokea wapi lakini upo uwezekano wa kuwa alipotea kutoka katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Baadhi ya wakazi wa manispaa hiyo, wameipongeza Serikali kwa muitikio wa haraka wakidai uharaka huo umesaidia kuokoa maisha ya watu waliokuwa katika eneo hilo.

“Kwakweli baada ya taarifa kutolewa hawakuchukua muda mrefu wahusika wamefika kwa wakati na kumuua mnyama huyo bila kuleta madhara kwa watu ingawa tayari kulikua na taharuki kwa watu wa eneo hilo,” amesema John Wegoro