Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chunya watimiza ahadi ya Rais Samia, Sh3 bilioni kujenga stendi ya kisasa

Mwenyekiti  wa Halmashauri ya  Wilaya ya Chunya, Bosco  Mwanginde (kulia) akifurahi jambo baada ya kusaini mkataba wa ujenzi wa kituo cha mabasi cha kisasa chenye thamani ya zaidi ya Sh3 bilioni ya mapato ya ndani.Picha na Hawa Mathias

Muktasari:

  • Mradi huo unatekelezwa chini ya Mkandarasi mshauri wa Kampuni ya  Malk Consultant Ltd kwa  miezi tisa, kuanzia Septemba 16, 2024 mpaka Juni 15, 2025.

Chunya. Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya, imesaini mkataba wa zaidi ya Sh3 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kisasa cha mabasi, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan.

Rais Samia alitoa agizo hilo Agosti, 2022 alipotembelea wilaya hiyo na kuielekeza halmashauri hiyo kutumia mapato ya ndani kujenga kituo cha mabasi baada ya wananchi kuwasilisha kero zao, ikiwemo ombi la mradi huo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chunya, Tamimu Kambona amesema hayo  leo Jumatatu, Septemba 9, 2024, wakati wa hafla ya utiaji saini utekelezaji wa mradi huo ambao utaanza Septemba 16, 2024 na kukamilika Juni 15, 2025.

Mradi huo utatekelezwa na mkandarasi mshauri, Kampuni ya Malk Consultants Ltd na utakuwa na miundombinu mbalimbali, ikiwamo vibanda 400 vya biashara na eneo la maegesho ya mabasi 100 kwa siku.

Kambona amesema lengo la ujenzi wa kituo cha mabasi ni kuboresha huduma za usafiri na kuondoa adha kwa wananchi waliomwomba Rais Samia kuidhinisha mradi huo.

"Tunatekeleza mradi kwa njia ya kandarasi kwa kuzingatia Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 10 ya Mwaka 2023, ambapo mradi ulitangazwa kupitia mfumo wa NeST, ili kumpata mkandarasi mwenye sifa kulingana na taratibu za manunuzi," amesema Kambona.

Akizungumza baada ya kutiwa saini mkataba huo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kushirikiana na halmashauri kumsimamia mkandarasi vema, ili akamilishe mradi huo kwa muda uliopangwa.

"Takukuru nina imani nanyi, muda uliopo kwenye mkataba mradi huu ukamilike. Pia niombe wazee wa mila (machifu) kushirikiana na Serikali kuhakikisha mradi unakuwa na tija na kunufaisha wananchi," amesema Homera.

Amesema lengo la Serikali ni kuboresha huduma za usafiri, ili kuchochea shughuli za kiuchumi na kuonya dhidi ya ubadhirifu wa fedha za mradi huo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chunya, Bosco Mwanginde amesema mradi huo utakuwa suluhisho kwa wananchi, hasa wafanyabiashara, kwani kutajengwa vibanda 400 kwa ajili ya shughuli za kiuchumi.

"Wananchi wanatarajiwa kupanua wigo wa shughuli za kiuchumi na ndiyo maana mradi huu unatekelezwa kwa mapato ya ndani ya halmashauri, ukiwa ni miongoni mwa miradi ya kimkakati," amesema Mwanginde.

Mkazi wa Kata ya Itewe, Anna Samuel ameeleza furaha yake kwa Serikali kusikiliza kilio chao na kuelekeza ujenzi wa kituo cha kisasa cha mabasi ambacho kitachochea shughuli za kiuchumi na kuongeza mapato ya Serikali.