Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere chasaini mkataba ujenzi wa miundombinu

Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT) Profesa Lesakit Mellau (wa kwanza kulia) pamoja na Mkurugenzi wa Kampuni ya Epitome Architects, David Kibebe wakisaini mkataba kwaajili ya Ushauri Uelekezi kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa majengo 16 ya chuo hicho kampasi kuu ya Butiama. Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

Chuo kikuu cha Mwalimu Julius Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT) kimetia saini  makubaliano ya ujenzi pamoja na usimamizi wa mradi wa ujenzi wa  chuo hicho ujenzi unaotarajiwa kukamilika ndani ya miezi 18 ukihusisha majengo 16 katika kampasi kuu ya Butiama.

Butiama. Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT) kilichopo wilayani Butiama Mkoa wa Mara kimesaini mkataba kwaajili ya ujenzi wa kampasi kuu ya chuo hicho.

Mikataba iliyosainiwa na chuo hicho ni wa mshauri mwelekezi pamoja na mkandarasi mmoja huku mikataba miwili baina ya chuo na makandarasi wengine wawili ikitarajiwa kusainiwa wiki ijayo.

Hatua hiyo imekuja baada ya Serikali kutoa zaidi ya Sh103 bilioni kwaajili ya ujenzi wa chuo hicho kilichokaa zaidi ya miaka saba bila kudahili wanafunzi kwa kile kilichoelezwa kuwa ni  kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukosefu wa miundombinu.

Akizungumza wakati wa  utiaji saini leo Jumanne Oktoba 31, 2023 Mratibu wa mradi wa ujenzi wa chuo, Profesa Msafiri Jackson amesema mradi unatarajiwa kuanza kutekelezwa siku 28 baada ya kutia saini.

"Mradi utatekelezwa ndani ya miezi 18 na kwa kuanzia tutaanza na ujenzi wa kampasi kuu hapa Butiama na tutajenga majengo 16 ikiwemo majengo ya utawala, madarasa, mabweni pamoja na miundombinu mingine ya chuo,"amesema

Amesema majengo hayo yatakuwa ni ya Ndaki ya Kilimo, Shule kuu ya kilimo na Mchakato wa Mazao pamoja na  Shule Kuu ya Uhandisi Nishati na Madini.

Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo hicho,  Profesa Lesakit Mellau amesema ana uhakika ujenzi huo utakamilika ndani ya muda uliopangwa kwavile hakuna kikwazo chochote.

"Kila kitu kipo, pesa ipo, mifumo yote inafanya kazi sasa kwanini mradi usikamilike kwa wakati ulioapangwa, tunaamini makandarasi pamoja na mshauri mwelekezi mtahakikisha lengo hili linatimia,"amesema

Amesema Serikali imedhamiria kukifanya chuo hicho kuwa na viwango vya kimataifa kwa ubora pamoja na elimu itakayotolewa na kwamba mbali na kuwa ujenzi huo kuwepo kwenye ilani ya uchaguzi ya CCM lakini pia chuo hicho kinalenga kumuenzi baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere.

"Watoto wa sasa ni vigumu kumfahamu Mwalimu Nyerere isipokuwa kupitia miradi kama hii ambayo inadhamiria kuendeleza historia yake nchini, pia mkumbuke hiki ni chuo kikuu cha umma kwa Kanda ya Ziwa kwahiyo lazima kiwe cha kisasa kuanzia kwenye majengo na mambo mengine,"amesema

Amesema kutokana na umuhimu wa chuo hicho, uwekaji wa jiwe la msingi utafanyika baada ya ujenzi kuanza ambapo mmoja wa viongozi wa ngazi za juu nchini anatarajiwa kuweka jiwe hilo ingawa hadi sasa bado haijajulikana kiongozi huyo ni nani.

Naye Mshauri Mwelekezi wa mradi huo, David Kibebe amesema kampuni yake ya Epitome Architects itahakikisha inasimamia mradi huo ili uweze kutekelezwa kwa mujibu wa mkataba na kwa kuzingatia thamani ya fedha.

"Tunajua Serikali imewekeza pesa nyingi sana kwenye mradi huu hivyo inatarajia kuwa kila kitu kitafanyika kama kilivyopangwa hivyo kwavile ni jukumu letu kusimamia nasi tunaahidi kusimamia suala hili ipasavyo,"amesema