CMA yataja sababu zinazoongoza migogoro ya kikazi

Muktasari:

  •  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako amefungua kikao kazi cha Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) chenye lengo la kufanya tathimini ya utendaji kazi na mafunzo, mkoani Morogoro.


Morogoro. Wakati Serikali ikiwaagiza watumishi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kuhakikisha wanatatua migogoro mahali pa kazi kwa wakati, tume hiyo imetaja sababu zinazoongoza migogoro ya kikazi.

Sababu hizo ni masuala ya ubaguzi, kusimamishwa kazi, kujengewa mazingira ya kuacha kazi, madhira, mikataba kuvunjwa isivyo halali, kutolipwa mishahara au kulipwa chini ya kima cha chini na haki za kichama.

Mkurugenzi wa CMA, Usekelage Mpulla amezitaja sababu hizo leo Alhamisi, Januari 4, 2024, mkoani Morogoro katika kikao kazi cha tume chenye lengo la kufanya tathimini ya utendaji kazi na mafunzo.

Mpulla amesema katika utatuzi wa migogoro ya kikazi, tume hiyo katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2023/24 ilikuwa na migogoro 4,579 ikiwa ya kikazi 1,859 iliyovuka mwaka na migogoro 2,720 iliyosajiliwa ngazi ya usuluhishi na uamuzi.

Amesema hadi kufikia robo ya pili ya 2023, jumla ya migogoro 2,712 sawa na asilimia 59 ya migogoro ya kikazi ilivuka mwaka na iliyosajili mwaka 2023/24 ilitatuliwa.

Akifungua kikao hicho, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako amewaagiza watumishi wa tume hiyo kuhakikisha wanatatua migogoro mahali pa kazi kwa wakati, haki na kuwa chachu ya kuwekeza ufanisi katika utendaji kazi wao.

Pia, amesema CMA ni lazima ijitengenezee mazingira ya kuaminiwa na wananchi, wafanyakazi, waajiri na wawekezaji kwa kutenda haki ambayo itaonekana kwa pande zote mbili.

Waziri Ndalichako amesema CMA inapaswa kutenda haki ili kuweza kupunguza kesi zinazopelekwa kwa jaji kutokana na baadhi ya wateja wao kukosa.

Amesema tume hiyo imeaminiwa na Serikali ili kuweza kuleta mchango na kasi ya kuongeza kasi ya wawekezaji katika sekta binafsi, hivyo iwapo itatenda haki baina ya pande mbili kati ya mwajiri na mwajiriwa uwekezaji utaongezeka hapa nchini.

 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Dk Yose Mlyambina amesema Mahakama hiyo inayohudumia mikoa ya Dar es Salaam na Pwani iliitisha majalada 350 kati ya hayo 313 yaliwasilishwa mahakamani kwa wakati  na 37 hayakuwasilishwa.