Corona yabadili utaratibu wa abiria kupanda mabasi mwendokasi

Muktasari:

Mamlaka ya Usafiri wa Ardhini (Latra) imeagiza mabasi yanayobeba abiria kuhakikisha wanazingatia utaratibu wa kubeba abiria wachache na kuwanawisha abiria mikono kwa maji yanayotiririka au vitakasa mikono ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona vilivyoingia nchini Tanzania.

Dar es Salaam. Baada ya kuripotiwa watu sita kuugua ugonjwa wa corona nchini Tanzania, abiria wanaotumia usafiri wa mwendokasi kutoka Kimara Mwisho kwenda  Gerezani, Morocco na katikati ya Jiji la Dar es Salaam wanalazimika kupanga foleni ili waweze kupanda magari hayo.

Mwananchi imeshuhudia foleni hiyo leo Ijumaa Machi 20,2020 inaanza pale tu abiria wanaposhuka katika mabasi ya mwendokasi yanayofanya safari zake kati Mbezi mwisho na  Kimara mwisho.

Abiria hao baada ya kushuka katika magari hayo hulazimika kupanga mistari kwa ajili ya kunawa mikono au kupaka vitakasa mikono (Sanitizer).

Katika eneo hilo, kuna njia mbili , abiria anaamua anawe mikono au apake kitakasa mikono.

Baada ya hapo anaingia upande wa pili kwa ajili ya kupanda gari kwenda sehemu anayoenda.

Licha ya matangazo kuendelea kutolewa katika kituo hicho kwa kipaza sauti, upande huo wa pili, kuna utaratibu mwingine umewekwa, ambapo askari waliovalia kiraia na wengine wenye sare pamoja na wafanyakazi wa Udart, wanatoa maelekezo kwa abiria sehemu wanapoenda , ambapo abiria wa kivukoni wanapanga mstari wao, hivyohivyo wa gerezani na Morocco nao wanapanga mstari lakini katika maeneo tofauti.

Baada ya hapo kila gari na safari yake na lina simama sehemu yake kwa ajili ya kubeba abiria.

Magari hayo baada ya kufika sehemu yanapotakiwa kubeba abiria, hufungua milango miwili tu kwa ajili ya kubeba abiria na kila abiria anaingia kwa kufuata utaratibu wa foleni.

Hata hivyo, magari ya ‘Express’ hayajai kama zamani, kwa sasa watu wakishakaa kwenye viti, wanaoruhusiwa kusimama ni wachache na baada ya hapo , askari huamuru dereva aondoke.

Kwa mabasi ambayo sio ‘express’ naona wanajaa kwa sababu gari inasimama kushusha abiria na kupakiza kila kituo .

Kitu kingine kwa sasa abiria hawaruhusiwi kuzunguka na gari ili apate siti, mfano abiria akipandia kituo cha Korogwe akifika Kimara mwisho anatakiwa ashuke apite upande wa pili na sio kushuka na kubaki  kituoni hapo, ili apande gari nyingine.

Utaratibu huo upo pia Kivukoni, ambapo abiria wanaopandia vituo vya karibu kama Kituo cha Jiji na Posta ya Zamani kwa ajili ya kuzunguka na gari hadi Kivukoni kwa ajili kupata siti, wakifika Kivukoni wanashushwa wote, hakuna abiria anayebaki kwenye gari.

Mmoja wa abiria aliyekuwa anakwenda Gerezani, Amina Juma anasema hali hiyo kwa kiasi chake inaweza kupunguza maambukizi lakini bado abiria ni wengine kuliko mabasi hivyo kunahitajika kuongezwa mabasi mengine.