CRDB yaipa Serikali ya Tanzania gawio la Sh6.8 bilioni

Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa CRDB, Ally Laay a

Muktasari:

Benki ya CRDB imetoa gawio kwa Serikali ya Tanzania la Sh6.8 bilioni baada ya kupata faida mwaka 2018

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania  imepokea gawio la Sh6.8 bilioni kutokana na uwekezaji wa asilimia 21 katika hisa ilizonazo katika benki hiyo.

Kiwango hicho ni sehemu ya Sh10 bilioni ambazo benki hiyo imetoa kwa Serikali na taasisi mbalimbali za umma zenye hisa CRDB kutokana na faida ya Sh64.2 bilioni iliyopatikana mwaka 2018.

Makabidhiano ya mfano wa hundi ya gawio yamefanyika leo Juni 23, 2019 jijini Dodoma ambapo Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amepokea gawio hilo kwa niaba ya Serikali na kukabidhi baadhi ya mashirika na taasisi za umma zilizopata gawio kutoka benki hiyo.

Baada ya kukabidhiwa, Dk Mpango ameupongeza uongozi wa Benki ya CRDB kwa kurudisha fadhila kwa mwananchi na kuzitaka benki na taasisi zote za fedha nchini kuiga mfano huo kwa maendeleo ya nchi.

“Benki ya CRDB na nyingine muongeze jitihada ili kuongeza gawio kwa Serikali ili iweze kuwahudumia wananchi katika huduma za kijamii ikiwamo afya, elimu na maji,” amesema Dk Mpango.

Amezitaka benki na taasisi za fedha kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa huduma za benki ili waweze kujikomboa kiuchumi na kuiwezesha nchi kupata gawio kwa ajili ya kugharamia shughuli za maendeleo.

Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa CRDB, Ally Laay amesema mwaka 2018, benki yake ilitengeneza faida ya Sh64 bilioni baada ya kodi ikilinganishwa na Sh 36.2 bilioni iliyopatikana mwaka 2017 mafanikio yaliyochangiwa na matumizi ya mfumo wa malipo kwa njia ya kielektroniki serikalini (GePG).

Kwa upande wake, mkurugenzi mtendaji wa benki hiyo, Abdulmajid Nsekela amesema CRDB imewekeza fedha kwenye mradi wa umeme katika Mto Rufiji mkoani Pwani na ipo tayari kuwekeza kwenye ujenzi wa miradi mingine ukiwamo  ujenzi wa reli ya kisasa (SGR).