CRDB yajivunia mafanikio kupata leseni ya kufungua benki DR Congo

Mwenyekiti wa bodi ya CRDB, Dk Ally Laay akizungumza katika mkutano mkuu jijini Arusha

Arusha. Benki ya CRDB imejivunia mafanikio mbalimbali ikiwemo kupata leseni ya kufungua benki katika nchi ya DR Congo jambo ambalo ni hatua kubwa sana ambayo imepigwa na benki hiyo.

Aidha benki hiyo pia imepata mafanikio makubwa kupitia   kampuni yake tanzu ya nchini Burundi ambapo kwa mwaka 2022 imepata faida kubwa zaidi ya Sh23 bilioni  sawa na ongezeko la asilimia 79 kutoka Sh12.8  bilioni ya mwaka 2021.


Akizungumza  katika mkutano mkuu wa benki hiyo uliofanyika jijini Arusha, Mwenyekiti wa bodi ya CRDB, Dk Ally Laay amesema tangia kuanzishwa kwa benki hiyo mwaka 2012 mwaka 2022 ndio imepata faida kubwa zaidi.

"Ninayofuraha kuwajulisha kwamba kampuni yetu tanzu ya nchini Burundi  inafanya vizuri sana na sasa tumepata leseni ya kufungua benki yetu katika  nchi ya DR Congo".amesema .

Akizungumzia mafanikio amesema mwaka huu benki hiyo pia imeanzika kampuni tanzu ambazo ni CRDB Bank Foundation na CRDB Insurance Company ikiwa ni benki ya kwanza kuanzisha kampuni tanzu kamili ya bima,” amesema Dk Laay.

Katika hatua nyingine Dk Laay benki hiyo imeidhinisha mapendekezo ya kulipa gawio la Sh45 kwa kila hisa kwa wanahisa  hivyo kufanya jumla ya gawio kwa mwaka wa fedha 2022 kuwa Sh117.5 bilioni.

Dk Laay alisema gawio lililopitishwa ni sawa na ongezeko la asilimia 25 likilinganishwa na gawio la Sh36 kwa hisa lililolipwa mwaka jana hali inayodhihirisha kuendelea kuimarika kwa pato kwa hisa ambalo mwaka 2022 limefika Sh34.5.

“Kwa mara nyingine tena, tunafurahi kupata matokeo mazuri kwa mwaka 2022 yaliyochangia kuongeza thamani kwa wanahisa wetu. Faida tuliyoipata mwaka 2022 ni uthibitisho wa utekelezaji makini wa mpango mkakati wetu wa miaka mitano wa 2018 – 2022.

Benki ilipata faida ya baada ya kodi ya Sh351.4 bilioni sawa na ongezeko la asilimia 31 ikilinganishwa na Sh268.2 bilioni za mwaka 2021,” amesema Dk Laay.  

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema  mwaka wa fedha 2022, waliendeleza juhudi za kukuza mapato na wakafanikiwa kwa kiasi kizuri kwani mapato ya uendeshaji yaliongezeka kwa asilimia 28 na kufika Sh745.8 bilioni yakichangiwa na kuongezeka kwa mikopo iliyotolewa. Kwa mwaka 2022, uwiano wa mikopo chechefu ulishuka mpaka asilimia 2.8 hivyo kuwa ndani ya ukomo uliowekwa kikanuni wa kutozidi asilimia 5.

Mizania ya Benki pia, amesema ilikua kwa asilimia 32 kutoka Sh8.8 trilioni mwaka 2021 mpaka Sh11.6 trilioni hivyo kuwa taasisiya kwanza ya fedha nchini kuvuka Sh10 trilioni. Ongezeko hilo, amesema limechangiwa na kuimarika kwa amana za wateja zilizoongezeka kwa asilimia 26.4 na kufika Sh8.2 trilioni kutoka Sh6.5 trilioni za mwaka 2021.   

“Juhudi zetu za kuimarisha huduma zetu zilituletea mafanikio hasa katika kubana matumizi kwani uwiano wa gharama na mapato uliimarika kutoka asilimia 66.7 mwaka 2018 mpaka asilimia 49.4 mwaka 2022,” amesema Nsekela.  

Nsekela amesema ufanisi uliopatikana umewezesha kuwekeza zaidi kuimarisha huduma kwa kuwekeza kwenye majukwaa ya kidijitali ambayo yanasaidia kukidhi mahitaji ya wateja kwa kuwapa huduma wazitakazo mahali walipo na kuzitumia kwa namna waitakayo.

“Leo hii zaidi ya asilimia 95 ya miamala yote ya benki inafanyika kidijiti hasa kupitia SimBanking, huduma za benki kwa intaneti, na kwa zaidi ya mawakala 28,000 wa Benki ya CRDB,” ameongeza.

Katika miaka mitano iliyopita, amesema Benki ilianzisha ubia wa kimkakati ambao umechangia kwenye mafanikio yake kwa mwaka 2022. Katika kipindi hicho, ubia huo umeiwezesha benki ya CRDB pamoja na kampuni tanzu zake kukuza mtaji, kuwa na teknolojia ya kisasa na kuboresha huduma hivyo kukidhi matarajio ya wateja.

Kuhusu mikakati ya baadae, Nsekela amesema Bodi ya Wakurugenzi imeidhinisha mpango mkakati wa miaka mitano kuanzia mwaka 2023–2027 unaosisitiza kujenga uchumi shirikishi, kuongeza thamani endelevu kwa wanahisa, na kuingia katika ubia wa kimkakati ili kuikuza benki na kuongeza ushawishi wake sokoni.

Mpango mkakati huo, amesema umetanguliza mbele maslahi ya wateja jambo linalomaanisha benki sasa inawekeza katika kuyatambua mahitaji ya wateja na kuyafanyia kazi ili kukidhi matarajio yao.

Nsekela amewashukuru wanahisa wa benki hiyo kwa ushirikiano ambao wameendelea kuipatia menejimenti na wafanyakazi wa benki hiyo, na kuwawathibitishia kwamba itaendelea kufanya vizuri ili kuwapa thamani ya uwekezaji walioufanya na wanaoendelea kuufanya.

Akizungumzia gawio lililoidhinishwa, Mkurugenzi Mtendaji mstaafu wa Benki ya CRDB ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Vunjo, Dk Charles Kimei alisema wanahisa wamefurahia ongezeko la gawio lililopendekezwa.

Dk Kimei ameongezea kuwa kitendo cha CRDB kutoa gawio kiila mwaka kimekuwa kikiwavutia wawekezaji wengi ndani na nje ya nchi kuwekeza ndani katika hisa za benki hiyo.