CUF yakwaa kisiki kortini, yafunguka

Muonekano wa jengo lililokuwa makao makuu ya CUF Zanzibar.Picha Masktaba
Muktasari:
Chama cha ACT-Wazalendo kimeshinda kesi ya madai dhidi ya Chama cha Wananchi (CUF) katika Mahakama Kuu ya Zanzibar, Tunguu.
Unguja/Dar. Chama cha ACT-Wazalendo kimeshinda kesi ya madai dhidi ya Chama cha Wananchi (CUF) katika Mahakama Kuu ya Zanzibar, Tunguu.
Katika kesi hiyo, CUF wanadai majengo yanayotumiwa na ACT-Wazalendo Zanzibar ni mali yao kabla ya wanachama wake, akiwemo aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kukihama chama hicho.
Kesi hiyo ilifunguliwa na CUF dhidi ya viongozi 20 wa ACT Wazalendo wakiongozwa na mdaiwa namba moja ambaye ni kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe.
Hukumu hiyo iliyotolewa juzi na Jaji wa mahakama hiyo, G.J Kazi alisema baada ya kupitia maelezo ya pande zote mbili mahakama imejiridhisha CUF kimeshindwa kuthibitisha uhalali wa majengo hayo na uharibifu wa mali wanazodai ziliharibiwa huku wakitaka kulipwa fidia ya mali hizo.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji Kazi alisema wadai walishindwa kuthibitisha uhalali wa umiliki wa maeneo na mali walizodai zimeharibiwa na kuchukuliwa na mdai, hivyo ameamua kuiondoa kesi hiyo mahakamani kwa gharama.
Jaji alisema kupitia ushahidi uliowasilishwa na chama hicho ulishindwa kuonyesha bila kuacha shaka uhalali wa umiliki wa mali hizo.
“Hoja ya kwanza imejibiwa bila kuweka usawa, kwa misingi hiyo moja kwa moja hoja ya pili inakufa, kwa hiyo naondoa shauri hili kwa gharama,” alisema.
Jana, gazeti hili lilizungumza na Katibu Mkuu wa CUF, Hamad Masoud aliyesema hawajaipata hukumu ya mahakama, hata hivyo alisema ACT- Wazalendo ilianzishwa kati ya mwaka 2013 hadi 2014 na majengo hayo yapo tangu mwaka 1992.
Chanzo cha kesi
Walikuwa wakidai ofisi zinazotumiwa na ACT Wazalendo, zikiwemo za Mtendeni, Vuga, Kilimahewa, Mfenesini ni mali ya CUF, huku wakitaka walipwe samani za ofisi ambazo nazo walidai ziliibiwa.
Mbali na mali hizo, pia walidai bendera za chama hicho nazo ziliibiwa, hivyo kutaka walipwe.
Kwa mujibu wa mdai alieleza tangu mwaka 1992 walikuwa wakijenga chama (CUF) na kutumia gharama kubwa katika majengo, ikiwemo Zanzibar
Alisema Machi 18, 2019 ACT walitangaza kwenye vyombo vya habari kujiunga na chama kingine kwa kaulimbiu ya ‘shusha tanga pandisha tanga’, kwa hiyo mdaiwa namba 2 hadi 20 walitumia ofisi zilizotangazwa hapo juu kupandisha bendera za chama cha ACT na walishusha bendera za CUF na kuziiba, huku kadi za wanachama na samani za ofisi navyo vikipotea na kuharibiwa.
Katika kesi hiyo, mdai aliwakilishwa na Wakili Mashaka Ngole, huku upande wa mdaiwa ukiwakilishwa na wakili Is-haq Shariff.