CWT inajivunia kujitoa kwa walimu kunusuru elimu katika janga la Uviko-19

Muktasari:
- Oktoba 5 kila mwaka ni siku ya mwalimu ambayo huadhimishwa kote duniani kwa ajili ya kuwapongeza walimu kwa kazi kubwa wanayoifanya.
Oktoba 5 kila mwaka ni siku ya mwalimu ambayo huadhimishwa kote duniani kwa ajili ya kuwapongeza walimu kwa kazi kubwa wanayoifanya.
Hii ni kumbukumbu ya kupitishwa kwa pendekezo la ILO / UNESCO la 1966 kuhusu hadhi ya walimu, ambayo inaweka vigezo kuhusu haki na majukumu ya walimu, na viwango vya maandalizi yao ya awali, ajira, na mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
Siku ya Walimu Duniani imekuwa ikiadhimishwa tangu 1994 kwa ushirikiano kati ya Shirika la Kazi Duniani (ILO), UNICEF na Shirikisho la Vyama vya Walimu Duniani (Education International - EI).
Kaulimbiu ya siku ya walimu duniani mwaka huu 2021 ni “Walimu kiini cha kuhuisha elimu”. Kauli mbiu hii imekuja kufuatia kuwepo kwa janga la UVIKO 19 na jinsi walimu walivyopambana kuinusuru elimu katika nchi mbalimbali.
Kipindi cha mwaka mmoja na nusu kilichopita tumeshuhudia dunia ikipita katika janga la Uviko-19 na kuathiri taaluma ya ualimu na utoaji elimu kwa ujumla, hivyo basi siku ya walimu duniani ya 2021 imezingatia zaidi msaada mkubwa ambao walimu wameuotoa kikamilifu katika kuhuisha elimu katikati ya janga hili kubwa.
Chama cha walimu Tanzania kama walivyo wanachama wengine wa shirikisho a vyama vya walimu duniani kinaungana na walimu wote duniani katika kuadhimisha siku hii muhimu kwa walimu.
Tangu kuanzishwa kwake tarehe Novemba 1, 1993, Chama cha Walimu Tanzania kimekuwa kikitekeleza madhumuni yake ambayo ni; Kujenga nguvu ya pamoja katika kudai haki, maslahi na mazingira bora ya kazi, Kuwalinda wafanyakazi katika sehemu zao za kazi dhidi ya uonevu na ukandamizaji wa mwajiri, kusuluhisha migogoro ihusuyo ajira zao, kuwawezesha wafanyakazi kutoa maoni yao kuhusu changamoto zinazowakabili katika mazingira yao ya kazi, Kutoa maoni ya jinsi ya kuongeza tija na namna ya kukabiliana na vikwazo katika uzalishaji, Kujadili na kupendekeza miundo mizuri ya utumishi.
Chama cha Walimu Tanzania kimekuwa kikitekeleza majukumu yake ya kumuhudumia mwanachama kwa kuzingatia katiba, kanuni, sera na miongozo mbalimbali iliyojiwekea. Shughuli mbalimbali zinazofanywa na CWT zinajikita katika kuitangaza kauli mbiu yake ambayo ni wajibu na haki.
Mahusiano ya CWT na wanachama wake
Kwa kipindi cha uwepo wa chama takriban miaka 28 tangu kuanzishwa kwake CWT imefanikiwa kufanya baadhi ya mambo yafuatayo:-
Uanzishwaji wa benki ya Mwalimu (MCBL) Julai 2016 inayoendelea kukua na kufikia hatua ya kuanza kupata faida kwa kipindi cha mwaka 2021.
Ili kutekeleza lengo la kuwainua walimu kitaalamu na kitaaluma CWT Kwa kushirikiana na shirika la Helvetas tunaendesha mradi wa kuboresha mbinu za kufundishia katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Dodoma, Shinyanga, Singida na Tabora.
Kuimarisha mazingira bora ya utendaji kazi kwa kujenga ofisi za Wilaya 38 na ukarabati wa ofisi 9 kwa “forced account”.
Chama kuwepo, kuendelea kukua na kuimarika kwa kipindi cha miaka 28 na kuendelea kuongeza idadi ya wanachama takribani wanachama laki tatu tangu kuanzishwa kwake.
CWT kwa namna nyingine imeendelea kusaidia wanachama kutoa elimu kwa njia ya vyombo vya habari kipindi cha janga la Uviko 19 kati ya mwezi Aprili hadi Juni 2020.
Chama kimekuwa kikiendelea kutoa huduma ya utetezi ikiwa ni pamoja na kutetea walimu kwenye kesi mbalimbali zinazowakabili walimu mahakamani, ambapo kwa kiwango kikubwa kesi zinapungua baada ya kuelimishwa na kukumbushwa wajibu wao kama wanachama kwa mwajiri/Serikali na jamii.
Wanachama kuendelea kukijua chama chao na kupelekea kukua kwa demokrasia ambapo kwa mwaka 2020, takwimu zinaonesha walimu waliojitokeza kugombea nafasi mbalimbali walikuwa Zaidi ya 91,000 sawa na asilimia 45.
Mahusiano ya CWT na Serikali
CWT imefanikiwa kuondoa ukomo wa madaraja kwa walimu ambapo awali madaraja yetu na vyeo vya walimu yalikuwa na ukomo, kwa mfano mwalimu mwenye cheti ukomo wake kwa kipindi hicho ulikuwa “E”, mwenye stashahada ulikuwa “F”, ukomo huu uliondolewa na CWT sasa hivi hakuna ukomo.
Majadiliano yaliyofanyika kati ya CWT na Serikali ulileta vianzia vya mishahara ya wakufunzi wa vyuo vya Ualimu (Vyuo vya Kati).
Posho za madaraka kwa wakuu wa Vyuo vya kati, maafisa elimu kata, wakuu wa shule na walimu wakuu.
Kufikia Juni 2021 walimu wapatao 121,074 walipanda vyeo kwa bajeti yam waka 2020/2021 na waliobadilishiwa mshahara hadi tarehe 30 Juni 2021 ni walimu 93,355.
Hitimisho
Kupitia siku ya walimu duniani tunapenda kutoa wito kwa wadau wengine wa eimu nchini kutumia siku hii kwa kufanya tathimini juu ya huduma mbalimbali wanazozitoa kwa walimu na kuangalia njia bora zaidi za kutatua changamoto zinazowakabili walimu ili kurahisisha kazi yao ya utoaji elimu nchini.
Aidha watumie siku hii pia kutambua kazi za walimu na kuwapa heshima kwa kutambua mchango wa mwalimu katika Jamii.
Tunapenda kuwapongeza walimu wote kwa kazi nzuri walizoendelea kuzifanya hasa katika kipindi kigumu cha janga la UVIKO 19.
Tunatoa wito kwao kuendelea kufanya kazi zao kwa umahiri na kuendelea kulinda afya zao kwa kushiriki kupata chanjo ya Uviko 19 kwa hiari ili kuendelea kulinda nguvu kazi ka