CWT yalaani walimu kunyang’anywa madawati

Mwenyekiti wa Chama cha Waalimu (CWT) Wilaya ya Geita Doto Joseph akizungumzia sakata la walimu kukaa chini.

Muktasari:

  • Shule ya Msingi Nyansalala iliyoanzishwa mwaka 2019, ina walimu 12 ambao tangu kuanzishwa kwake wanatumia madawati kutokana na kutokuwa na meza wala viti.

Geita. Chama cha Walimu (CWT) Wilaya ya Geita kimelaani kitendo kilichofanywa na uongozi wa Kijiji cha Nyansalala kuwanyanganya walimu wa shule ya msingi ya kijiji hicho madawati waliyokuwa wakiyatumia kikisema kitendo hicho hakipaswi kufumbiwa macho.

Walimu wa shule hiyo walinyang’anywa madawati na uongozi wa kijiji hicho ukiongozwa na Ofisa Mtendaji, Makarios Rweyemamu Januari 23, 2024 wakati walimu wakiendelea na shughuli zao shuleni hapo.

Mwalimu mkuu msaidizi wa shule hiyo, Mathias Mashala amesema Serikali ya kijiji ikiwa na mwenyekiti wa kamati ya shule na mtendaji wa kijiji walifika shuleni hapo saa tatu asubuhi na kuamuru walimu watoke kwenye madawati kwa kuwa yaliandaliwa kwa ajili ya wanafunzi.

Akizungumzia kitendo hicho leo Januari 26, Mwenyekiti wa CWT Wilaya ya Geita, Doto Joseph amesema kitendo kilichofanywa si utawala bora na ameiomba mamlaka kumchukulia hatua za kinidhamu.

“Kama wapo walimu wapo tayari kukaa chini waje, lakini huu udhalilishaji na kuvunjiwa heshima maofisa wa Serikali wanakaa chini sio sawa.

“Hakuna aliye juu ya sheria na kama kuna jambo (mtendaji) afuate taratibu na atumie busara, lakini si kuja na mgambo kuwanyang’anya walimu madawati. Mkuu wa wilaya yupo mkurugenzi yupo, washughulikie hili jambo,” amesema Joseph.

Amesema ofisa mtendaji kama msimamizi wa rasilimali watu kwenye eneo lake alipaswa asaidie kutatua changamoto zilizopo katika shule hiyo na si kuongeza tatizo.

“Kitendo cha kumwambia mwalimu akae chini, hili jambo halikubaliki tunalaani kitendo hiki walimu wanakaa chini mwanafunzi anaefundishwa anakaa kwenye dawati, watoto wanalionaje jambo hili na watamchukuliaje mwalimu,” amsema.

“Ilileta taharuki na kuwavunja moyo walimu maana kilikuwa kitendo cha ghafla. Kama ni viti tulishawaeleza, viti vipo kwa fundi havijakamilika na kweli wapo wanafunzi wanakaa chini kwa kukosa madawati na shule hii pia ina wanafunzi wengi kitendo kilichofanyika si cha kiungwana kwa sisi watumsihi,” amesema Mwalimu Mashala

Akizungumzia kadhia hiyo, Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Joseph Mfungi amesema mtendaji wa kijiji amekuwa akiwabugudhi walimu mara kwa mara, ikiwemo kuwataka walimu kumwagia maji kwenye ujenzi unaoendelea shuleni hapo.

Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Makarios Rweyemamu amekiri kushirikiana na viongozi wenzake wa Serikali ya Kijiji kuondoa madawati na kuyapeleka kwenye madarasa ambayo watoto wanakaa chini.

“Kila mwaka mwalimu mkuu hupewa fedha za ukarabati na kwenye vikao vyetu vya halmashauri ya kijiji kwa kuwa yeye ni mjumbe na tumekuwa tukifanya vikao mara kwa mara tukimtaka atumie fedha hizo kutengeneza viti.

“Novemba mwaka jana tulimbana akadai ana Sh1.8 milion na tukamtaka azitumie kutengeneza viti na akaahidi atatekeleza lakini hakutekeleza,” amesema.

Amesema kwa pamoja waliazimia ifikapo Januari 8, 2024 wataondoa madawati na kuyapeleka madarasani na kwamba yeye kama mtendaji alitekeleza maazimio ya kikao cha halmashauri ya kijiji.