Daktari aliyesema Trump ana afya njema kuliko marais wengine afariki dunia

Daktari aliyesema Trump ana afya njema kuliko marais wengine afariki dunia

Muktasari:

  • Harold Bornstein ambaye ni daktari binafsi wa zamani wa Rais wa Marekani, Donald Trump anayemaliza muda wake Januari 20, 2021  amefariki dunia.
  • Tabibu huyo mwenye nywele ndefu alikuwa daktari wa Trump kuanzia mwaka 1980 hadi 2017.

Marekani. Harold Bornstein ambaye ni daktari binafsi wa zamani wa Rais wa Marekani, Donald Trump anayemaliza muda wake Januari 20, 2021  amefariki dunia.

Bornstein atakumbukwa kwa kauli yake kwamba Trump ndio rais mwenye afya njema kuliko marais wengine duniani.

Taarifa zinaeleza kuwa daktari huyo alifariki dunia Ijumaa iliyopita Januari 8, 2021 akiwa na umri wa miaka 73 huku  gazeti lililoripoti taarifa hizo la New York Times likificha chanzo cha kifo chake. Alikuwa daktari wa Trump kuanzia mwaka 1980 hadi 2017.

Bornstein alizua gumzo Desemba,  2015 wakati timu ya kampeni za urais ya Trump ilipoweka wazi barua yake ikieleza afya ya kiongozi huyo.

“Kama akichaguliwa Trump naweza kusema bila ya shaka atakuwa mtu mwenye afya bora kuwahi kuchaguliwa kuwa rais,” ilieleza sehemu ya barua hiyo.

Daktari huyo ambaye makazi yake yalikuwa katika Jiji la New York aliiambia shirika la habari la CNN mwaka 2018 kwamba rais huyo wa Marekani ndiye aliyesema mwenyewe maneno yote ya barua hiyo.

"Sikuandika barua ile," alisema Bornstein ambaye ndoto zake za kwenda ikulu na Trump zilififia baada ya  kuliambia gazeti la New York Times kuwa rais huyo alikuwa akinywa dawa za kukuza nywele zake.

Pia alinukuliwa na televisheni ya NBC News akieleza kuwa baada ya habari hiyo kuchapishwa na gazeti la Times, mlinzi alikwenda katika ofisi yake iliyopo Park Avenue na kuchukua nyaraka zote zinazohusu afya ya rais huyo.