Daladala za Moshi zagoma kutoka huduma

Muktasari:

  • Madereva wa magari yanayotoa huduma katika maeneo kadhaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro wamegoma hali iliyosababisha usumbufu kwa wakazi wa mji huo.

Moshi. Magari madogo ya abiria maarufu kama Hiace, yanayotoa huduma katika maeneo ya KCMC, Soweto, Majengo na Bonite Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, yamegoma kutoa huduma kuanzia saa 5:00 asubuhi kwa madai ya kupinga kukamatwa na polisi kutokana na kukwepa kulipa ushuru.

Madereva wa magari hayo, wamegoma kulipa ushuru wa Sh1,000 wa maegesho ya magari kwa siku katika manispaa hiyo, kuanzia Novemba 19, 2018, wakipinga bajaji kutoa huduma katika maeneo ya mji huo kama hiace.

Akizungumza leo Jumatano Machi 13, 2019, katibu wa Hiace zinazotoa huduma maeneo ya KCMC, Alfan Shaban amesema wamegoma kutoa huduma baada ya polisi kuanza kuwakamata na kuwadai ushuru.

"Leo Asubuhi magari matano ya KCMC, mawili ya Soweto na Bonite yalikamatwa na polisi na kupelekwa eneo la kuhifadhi magari la Manispaa kule majengo, kutokana na kutolipa ushuru, sasa na sisi tukaona kuliko tukamatwe, bora tugome maana huu ni uonevu," amesema Shaban.

"Mbali na hiyo Sh1,000 kwa siku, bado tunapaswa kulipa Sh15,000 kwa mwaka kwa ajili ya stika na ni kwa ajili pia ya maegesho, tumeshakaa vikao mara kadhaa na manispaa kuomba kuondolewa ushuru mmoja lakini bado kilio chetu hakijasikilizwa," ameongeza.

Alipotafutwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Michael Mwandezi, kuzungumzia suala hilo amesema anatambua wanapaswa kulipa ushuru kwa mujibu wa sheria ila hana taarifa kama kuna mgomo wa magari katika manispaa hiyo.

Naye Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchikavu (Sumatra) mkoa wa Kilimanjaro, Johns Makwale amesema hajapata taarifa zozote kama kuna mgomo.

Kutokana na mgomo huo, hali ya usafiri kwenye maeneo hayo imekuwa ngumu kwa abiria kulazimika kutembea na wengine kutafuta njia mbadala kuhakikisha wanafika wanakokwenda

Endelea kufuatilia Mwananchi kujua kinachoendelea