Daladala zinazogusa 'Mwendokasi' Mbagala zaendelea kupiga kazi
Moja ya daladala ikiwa inashusha abiria kutoka hatua chache kilipo kituo kikuu cha 'mwendokasi' Mbagala
Muktasari:
- Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) imesema inafuatilia suala hilo huku Kampuni ya Mofat ikieleza inaendelea kuchapa kazi kama kawaida.
Dar es Salaam. Licha ya leo Jumatano, Julai 1, 2026 daladala zinazotumia barabara ya Kilwa kutakiwa kuanza kutekeleza agizo la kutoshusha na kupakia abiria vituo vya katikati hadi zifike mwisho wa safari yake, hali hiyo imeonekana kutotekelezwa.
Pia, kwa zile daladala zinazotoka Mkuranga, Toangoma na vitongoji vingine, kutakiwa kuishia Kituo cha Mwendokasi cha Mbagala Rangitatu, agizo hilo pia halijatekelezwa.
Ikumbukwe Juni 15, 2026 Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) ilisema kuanzia Julai mosi, mwaka huu, daladala zote zinazotumia Barabara ya Kilwa hazitaruhusiwa kutoa huduma katika maeneo yanayohudumiwa na mradi wa mabasi yaendayo haraka, maarufu mwendokasi.
Uamuzi huo wa Latra unakuja ikiwa imepita miezi mitatu tangu mtoa huduma wa mabasi hayo, Kampuni ya Mofat, ilalamikie kukosa faida ya uwekezaji wake, ikisisitiza uwepo wa daladala unafanya mabasi yake kutoa huduma chini ya uwezo wake.
Mofat ina mabasi 200 lakini kwa sasa 50 pekee ndiyo yanayoelezwa na uongozi kuwa yanayofanya kazi huku mengine 150 yakiwa yameegeshwa.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habibu Suluo, alisema wananchi wanaotoka maeneo ya Mkuranga, Toangoma na vitongoji vingine watashuka katika Kituo cha Mbagala Rangitatu na kuunganisha safari zao kwa kutumia mabasi ya mwendokasi kwenda katikati ya jiji na maeneo mengine.
Eneo maalum ndani ya kituo Kikuu cha mwendokasi Mbagala lililotengwa kwa ajili ya maegesho ya daladala likiwa halina gari hata moja kama linavyoonekana kwenye picha.
Mkurugenzi huyo alieleza tathmini iliyofanywa, imeonesha mabasi ya mwendokasi yanatumika kwa wastani wa asilimia 50 ya uwezo wake, hali inayotishia uwezo wa wawekezaji kurejesha mikopo waliyochukua kwa ajili ya mradi huo.
Hali ilivyo
Mwananchi asubuhi ya leo Jumatano Julai Mosi imepita katika barabara hiyo na kushuhudia daladala zikiwa zinaendelea kutoa huduma zake kama kawaida kwa kupakia na kushusha kwenye vituo hivyo vya katikati kama vile hakuna katazo lolote.
Zinafanya hivyo huku Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani wakionekana kutapakaa kwa wingi katika barabara hiyo bila kuwachukulia hatua yoyote.
Saluo wakati anatangaza katazo hilo, alisema tayari maelekezo yametolewa kwa askari wa usalama barabarani kusimamia sheria kikamilifu na daladala zitapaswa kushusha na kupakia abiria katika maeneo yaliyotengwa na si kusimama ovyo ndani ya eneo linalopitiwa na mradi wa mwendokasi.
Ukiacha ushushaji na upakiaji abiria hata katika eneo lililotengwa kwa ajili ya kuegeshwa daladala katika kituo hicho cha mwendokasi, hakuna gari hata moja iliyoonekana kuwepo hapo.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Uendeshaji na Usimamizi wa Miundombinu wa Dart, Philimon Mzee, amesema Kituo cha Mbagala kimejengwa kwa uwezo wa kuhudumia idadi kubwa ya daladala, bajaji na bodaboda kwa wakati mmoja.
Amesema eneo hilo lina uwezo wa kupokea zaidi ya daladala 50 kwa wakati mmoja, pamoja na maeneo maalumu ya bajaji na bodaboda.
Akizungumzia hilo, Msemaji wa Mofat, Philip Chalanga amesema licha ya kutotekelezwa kwa agizo hilo wao wanaendelea kutoa huduma kama kawaida.
"Hili suala unajua ni la mamlaka zinazosimamia usafirishaji, hivyo sisi hatuwezi kuzungumza chochote kwa kutotekelezwa kwa agizo hilo isipokuwa tutaendelea kutoa huduma zetu kama kawaida kwa kuwa tuna magari ya kutosha," amesema Chalanga.
‘Tunafuatilia’
Akilizungumzia hilo, Kaimu Meneja wa Leseni wa Latra, Ngereza Patel, amekiri kuwepo kwa jambo hilo na kueleza bado wanafutilia na kuahidi kuja na majibu.
"Ni kweli hata sisi tumeliona hilo ila bado tupo tunafuatilia, tutawapa majibu muda sio mrefu," amesema Patel.
Kwa mujibu wa Patel barabara hiyo ina jumla ya daladala 1,637 zinazotoa huduma ambazo kutokana na kuanza kusitisha vibali vya usafirishaji inatarajiwa hadi kufika katikati ya mwaka ujao zitakuwa zimeondolewa zote.
Baadhi ya wananchi walisema nao kutokana na tangazo lile, walijipanga kuunganisha gari, lakini baada ya kufika hapo waliona yakiendelea na safari.
"Binafsi nilijipanga kuja kuunganisha gari nitakapofika hapa mwendokasi ya Mbagala nikiwa natokea Kisemvule, lakini tulipofika gari ikanyoosha, hiyo pia ni afadhali kwangu nimepunguza gharama," amesema Dyna Jimmy.