Dar si salama
Muktasari:
Lakini wanaume nao huonekana kila dakika wakipapasa mfuko wa suruli hali kuhakikisha kama waleti ipo salama.
Ukiingia ndani ya daladala na kuona wanawake walivyokumbatia mikoba yao, unapata picha ya fikra zao kwa watu walio karibu yao.
Lakini wanaume nao huonekana kila dakika wakipapasa mfuko wa suruli hali kuhakikisha kama waleti ipo salama.
Hali ndivyo ilivyo kwa dada aliyekaa dirishani, ambaye hatakikufungua kioo cha daladala, akihofia simu yake kuporwa.
Hata ambaye yupo ndani ya gari binafsi jijini Dar es Salaam wakati wote anafunga vioo na kama mafuta ya kuungaunga basi atahakikisha anakuwa macho kulinda vitu vyake kwa kuviweka chini ya viti ili visiibwe. Hofu zaidi huja pale unapoona vijana wawili wakiwa juu ya bodaboda pembeni ya gari lako, kwani wengi wameporwa na watu wa aina hiyo.
Vijana hawa wa bodaboda ni maarufu kupora chochote, iwe pochi au simu za akina mama wanaotembea pembezoni mwa barabara au abiria wanaoongea na simu kwenye vyombo vya usafiri.
Aina za uhalifu hutofautiana kutokana na maeneo na kwa mujibu wa Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro hakuna eneo ambalo ni salama. Kamanda Sirro anasema wahalifu hutumia mbinu mbalimbali kulingana na maeneo, hivyo watu wanapaswa kufahamu kuwa wanatakiwa kujilinda na kutoa taarifa za uhalifu.
Ukikosa fedha tatizo
Kwa baadhi ya maeneo ni mashaka makubwa kutembea bila kitu mfukoni. Mkazi wa Tabata Kisukuru, Andrew Msakati anasimulia alivyonusurika kutoka mikononi mwa vibaka waliotaka ‘kumteka’ na kumpeleka kusikojulikana baada ya kugundua kuwa hakuwa na kitu chochote mfukoni.
Msakati aliyekuwa akitoka katika matembezi alijiamini kutembea kwa miguu kuelekea nyumbani kwake kwa kuwa hakuwa na kitu chochote mfukoni.
“Wakati natoka nyumbani niliacha kila kitu kumbe ilikuwa kosa kubwa, wale vibaka waliponikaba na kunisachi waliniuliza kwa nini mwanaume mzima natembea bila kitu mfukoni, wakaanza kunivutia kichochoroni, bahati nzuri ilitokea gari wakakimbia na kuniacha,” anasimulia.
Wakazi wengi wa Jiji la Dar es Salaam waliozungumza na gazeti hili wanasema ni hatari zaidi kutembea bila fedha au simu kwani vibaka wakikukaba wanaweza kukufanyia unyama.
Simu
Matumizi ya simu yamerahisisha maisha kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam lakini pia imekuwa chanzo kikuu cha kuwaingiza katika matatizo. Kwa mfano, kibaka anapomnyemelea mtu, kitu cha uhakika ambacho anajua atakipata ni simu ya mkononi. Uhalifu mwingine maarufu ni wa kupigiwa simu na namba ngeni, lakini mpigaji hujitambulisha kama mtu anayekufahamu na mwisho wa siku lengo huwa ni kukuibia fedha au vitu vingine.
Hivi sasa mtu anapopigiwa simu ya mkononi au kuombwa fedha hulazimika kuchukua hatua kadhaa kujiridhisha iwapo ni kweli anatuma fedha hizo kwa mtu sahihi.
Kuulizwa pia kesi
Wangapi wameingia katika mtego wa matapeli kwa kuulizwa njia au jengo fulani? Ni wengi mno. Simama katikati ya Jiji la Dar es Salaam na jaribu kumuuliza mtu kuhusu chochote uone namna atakavyokujibu. Anaweza kuamua kunyamaza au kukujibu huku akiendelea na shughuli zake kwa kuwa haamini kutokana na matukio ya kutapeliwa yaliyowakuta wasamaria wema.
Dar hakuna lifti
Tazama asubuhi na jioni watu walivyojaa kwenye vituo vya mabasi huku magari binafsi yakiwa tupu.
Ingewezekana watu hao wangewasaidia abiria vituoni kwa kuwapa lifti katika magari yao, lakini baadhi ya wenye magari wamewahi kuamka wakiwa hospitalini baada ya kuamini kuwa walikuwa wakitoa msaada kumbe walibeba wahalifu.
Sadick Juma (siyo jina lake) anasema aliwapa lifti wanawake wawili katika kituo cha Mwananyamala Komakoma na katika maongezi walimweleza kuwa walikuwa wakienda kumtazama mgonjwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Walipofika barabara ya Kinondoni karibu na Makaburini alianza kuhisi kizunguzungu na wanawake hao walimshauri aegeshe gari pembeni. Baada ya hapo alishtuka siku ya pili akiwa Hospitali ya Mwananyamala na kugundua kuwa alikuwa ameibiwa kila kitu likiwamo gari.
Tahadhari usiku
Kama hulipendi gari lako katiza barabara ya Tandale usiku halafu kwa bahati mbaya lipate hitilafu, hapo ndipo utakapojua kuwa kuna Watanzania wanalifahamu gari kuliko kitu kingine, kwani kifaa kimoja kimoja kitang’olewa na baada ya dakika 15, gari litakuwa tupu.
Maeneo kama Magomeni, Temeke, Tandale ni hatari kwa madereva nyakati za usiku hasa pale gari linapopata hitilafu kwani vibaka hutumia mwanya huo kuiba vifaa na kuliacha kama chuma chakavu.
Ukilala simu ficha uvunguni
Madirisha kutobolewa na simu ‘kuchotwa’ ni kitu cha kawaida katika maeneo ambayo nyumba hazijajengwa kwa mpangilio maalumu kama Buguruni, Tandale, Mbagala, Gongo la Mboto au Kipawa.
Vibaka hutumia sayansi ya kipekee kuiba simu baada ya kutoboa madirisha na kuingiza kifaa maalumu ambacho huichota au kuichomoa katika chaja.
VOX POP
Joram Munuo (32)
Kazi- Dereva bodaboa
Mkazi wa Tabata Kimanga
Wiki iliyopita nilikuwa nimeegesha kituoni mwananchi majira ya saa sita na robo usiku nikiajiandaa kurudi nyumbani alikuja abiria na kuniomba nimpeleke kimanga Mnarani nikakubali kwa sababu ni jirani na maeneo ninayoishi.
Nilipofika aliponielekea alishuka na kuniwekea bastola kichwani na kuniamuru nitoke kwenye pikipiki na nilale chini. Aliambia kama nataka kuishi nimpe ufunguo wa pikipiki.
Tumaini Msuya
Kazi- Dereva bajaji
Mkazi- Mabibo
Niliibiwa vitu vya ndani vyote halafu wezi walivyokuwa wajanja walinisogezea feni liendelee kunipuliza wakati wanachukua vitu. Niliposhtuka nilihisi ni ndoto tu nikaendelea zangu kulala.
Nilienda polisi kutoa taarifa lakini baada ya kuona sifanikiwi nikaenda kwa waganga wajadi ili wanisaidie kuwaadhibu wezi hao.
Jackson Kapange
Kazi- Dereva taksi
Mkazi wa Tabata Kisiwani
Mimi pamoja na mama mwenye nyumba tuliibiwa saa 8.20 mchana mimi nikiwa huku kutafuta ridhiki yeye akiwa amejipumzisha ndani.
Haukupita muda mrefu nikaibiwa tena siku chache baada ya kununua vitu vipya. Mwishowe nikaona isiwe tabu nikahama kabisa mtaa huo.
Salma Ismail (18)
Mkazi wa Chanika
Kazi- Mfanyabiashara
Wiki iliyopita nikiwa Buguruni kuna mwanamume alikuwa akinifuata kaw nyuma, nilikuwa na mashaka naye hivyo nikawa makini kila hatua ninayopiga.
Hata hivyo aliponikaribia sijui nilishikwa na ganzi gani kwani alinikaba na kupora mkoba uliokuawa na kila kitu ndani yake ikiwemo fedha na simu.