Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dar yaanza operesheni kuondoa spika zenye kelele Kariakoo

Muktasari:

  • Hatua hiyo inakuja ikiwa zimepita takribani wiki tatu baada ya gazeti la Mwananchi kuandika mfululizo wa makala maalumu kuhusu spika za matangazo ya biashara, ikiwemo vipaza sauti, kugeuka kuwa sauti rasmi katika masoko mengi ya jijini Dar es Salaam, likiwemo la Kariakoo.

Dar es Salaam. Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeanza mchakato wa kuondoa spika za matangazo zinazolalamikiwa kusababisha kelele kwa wanunuzi na wapita njia katika maeneo mbalimbali ya jiji, hususan Kariakoo na masoko mengine.

Spika hizo, zikiwemo za kutumia ‘flashi’ na vipaza sauti vinavyotumiwa na wafanyabiashara wakubwa na wadogo kutangaza bidhaa zao kupitia matangazo yaliyorekodiwa, zimekuwa zikisababisha kelele kubwa katika maeneo ya biashara.

Kwa muda mrefu, imekuwa kawaida katika masoko kama Kariakoo kuona kila mfanyabiashara akitumia kipaza sauti au spika kubwa kutangaza bidhaa zake, hali inayosababisha usumbufu kwa wanunuzi na wapita njia, hivyo kuibua uhitaji wa kudhibiti matumizi ya vifaa hivyo.

Hatua ya Jiji la Dar es Salaam imekuja ikiwa zimepita takribani wiki tatu baada ya gazeti la Mwananchi kuandika mfululizo wa makala maalumu kuhusu spika za matangazo ya biashara, ikiwemo vipaza sauti, kugeuka kuwa sauti rasmi katika masoko mengi ya jijini Dar es Salaam, likiwemo la Kariakoo.

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imekuja na hatua hiyo wakati tayari Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limezindua mikakati mipya ya kukabiliana na ongezeko la uchafuzi wa kelele katika miji mikubwa nchini.

Operesheni ya kuondoa spika hizo imeanza Juni 2, 2026 katika mitaa mbalimbali ya Kariakoo, ikiwemo ya Msimbazi, Narung’ombe na Aggrey, ambako kunatajwa kukithiri kwa changamoto za kelele zinazosababishwa na spika hizo.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ameliambia Mwananchi leo Juni 6, 2026 kuwa wameanza kuziondoa spika hizo ambazo amesema zimekuwa kero kwa wananchi na kushusha hadhi ya soko la Kariakoo.

“Tulishaamua kuwa ni marufuku kuendelea na matumizi ya spika katika maeneo yote ya maduka Kariakoo, badala yake waandike mabango ya kawaida. Kama tutaruhusu kila mmoja afunge spika zake, wale wenye uwezo watachukua bendi kabisa Kariakoo ili kutumbuiza.

“Haya, wewe unayeuza sumu ya mende unaweka spika, sumu ya panya unaweka, unayeuza jeans au fulana unaweka; halitakuwa soko tena bali kelele. Kwa hili Serikali tumesema hapana, lazima tuziondoe spika kwenye eneo la Kariakoo,” anasema Mpogolo.

Kabla ya kuanza kwa operesheni hiyo walifanya kikao na Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo (JWK), walioeleza kuwa moja ya changamoto ni kelele hizo, barabara za mitaa ya soko hilo kutopitika kwa urahisi na wafanyabiashara wa mboga kufanya shughuli zao pembezoni mwa soko.

“Katika hili lazima tusimamie sheria, marufuku watu kuweka spika zao nje au kuweka spika za matangazo kwa sababu ni kero. Soko la Kariakoo si kwa ajili ya matakwa ya mtu binafsi bali watu wote. Tumeshawatangazia na hatua itakayofuata ni kuwapeleka mahakama ya jiji ili hatua za kisheria zichukuliwe.

“JWK ilishawahi kuniandikia barua wakilalamikia suala la kelele, hivyo tunaendelea kushirikiana na jumuiya hiyo kwa ukaribu,” anasema Mpogolo.

Mpogolo ametumia nafasi hiyo kuwaeleza wafanyabiashara wengine wasiokuwa na taarifa kuacha mara moja matumizi ya spika, huku akisisitiza kuwa operesheni hiyo ni endelevu.


JWK yatoa neno

Katika hatua nyingine, Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo (JWK) imeishukuru Serikali kwa utekelezaji wa kuondoa spika hizo zilizokuwa kero hata kwa wafanyabiashara wengine wa Kariakoo.

Mwenyekiti wa JWK, Severin Mushi, amesema baadhi ya mitaa ya Kariakoo ikiwemo ya Swahili, Nyamwezi na Mchikichi iko katika hali nzuri hivi sasa tofauti na wiki iliyopita kabla ya Serikali kuziondoa spika hizo.

“Kumekuwa na mwitikio mkubwa wakati maofisa wa Serikali wakitekeleza jukumu hili, hali ya Kariakoo inaanza kubadilika na utulivu umekuwepo kwa kiasi fulani.

“Suala hili lilikuwa kero kwa sababu wateja na wafanyabiashara hawakuwa wakisikilizana hata pale simu inapopigwa. Ingawa wenye spika wanalalamika watafanyaje biashara, lakini kwa watu wanaokuja Kariakoo wamelipokea vizuri,” amesema Mushi.

Mushi amesema watu wanaokwenda Kariakoo wakipita baadhi ya mitaa watakuwa na uwezo wa kuongea kwa simu kwa utulivu na kusikilizana baada ya kelele hizo kupungua.

“Kilichobaki hivi sasa ni kuondoa baiskeli za miguu mitatu katikati ya barabara na meza ili njia zipitike vizuri kwa wananchi wanaofanya manunuzi,” amesema Mushi.


Walichokisema wananchi

Julius Mapo amesema spika hizo zimekuwa kero, hivyo hatua ya Serikali kuanza kuziondoa katika mitaa mbalimbali ya Kariakoo yenye maduka mengi ni jambo la kupongezwa.

“Ni mwanzo mzuri, sasa tukitoka hapo Serikali ihamie kwenye masoko ya mitumba ya Tandika na Kariakoo, nako kuna balaa la kelele. Wakifanya hivi watatusaidia sana sisi wananchi,” amesema Mapo.

Naye, Margreth Martine ameungana na Mapo akitaka hatua zaidi zichukuliwe dhidi ya spika hizo ambazo zimekuwa kero pindi wanapokwenda katika masoko ya Kariakoo, Karume na Tandika.

“Wameanza Kariakoo basi wasipoe. Nimekuja leo nimeshangaa kuona utulivu katika baadhi ya mitaa, kumbe inawezekana. Hatua hii isiwe nguvu ya soda bali iwe endelevu, maana wanaweza wakarudia tena,” amesema Martine.