Dawa mseto yaanza kujenga usugu

Muktasari:

  • Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa magonjwa ya binadamu (Nimr) umebaini malaria bado ipo kwenye kiwango kikubwa nchini, huku dawa mseto ya ugonjwa huo, Artemether-Lumefantrine (ALU) ikianza kujenga usugu katika mkoa wa Kagera.

Dar es Salaam. Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa magonjwa ya binadamu (Nimr) umebaini malaria bado ipo kwenye kiwango kikubwa nchini, huku dawa mseto ya ugonjwa huo, Artemether-Lumefantrine (ALU) ikianza kujenga usugu katika mkoa wa Kagera.

Hayo yamebainika kupitia mradi wa miaka mitatu wa utafiti wa kufuatilia malaria kwa kutumia mbinu za vinasaba, ulioanza kufanyika nchini Mei 18, 2020.

Utafiti huo ulilenga kuangalia jinsi vinasaba vya malaria vinavyotofautiana katika vimelea vinavyotoka maeneo mbalimbali ya nchi na hali halisi ya utendaji wa dawa na vipimo vya ugonjwa wa malaria.

Mtafiti Mkuu wa mradi huo, Dk Deusdedit Ishengoma alisema kwenye kongamano la 31 la kisayansi la Nimr kuwa watafiti hawajaona tofauti katika vinasaba vya vimelea vinavyopatikana Tanzania na kuwa bado Tanzania ipo kwenye kiwango kikubwa cha malaria.

“Kwenye upande wa dawa zinavyofanya kazi imeonekana dawa ya Alu bado ipo vizuri, ila kuna dalili ya hatari katika mkoa wa Kagera. Tulipima wagonjwa 383 na wagonjwa 30 walionekana wana vimelea vya malaria ambavyo vimeanza kujenga usugu.

“Wagonjwa hao wote 20 wapo wilaya ya Karagwe, tisa wapo Kyerwa na mmoja Ngara ikionyesha kabisa kwamba eneo hilo linaanza kuwa hatarishi kwa usugu dhidi ya malaria,” alisema Dk Ishengoma.

Hata hivyo, utafiti huo haujabaini usugu wa dawa hiyo katika mikoa mingine iliyoshirikishwa.

Kutokana na matokeo hayo, Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi alipozungumza na Mwananchi alisema “tutakaa na programu ya malaria tuone nini cha kufanya.”

Alipoulizwa ni kiwango kipi cha usugu kinachofikiwa hadi dawa kuondolewa, Msasi alisema “ili dawa iweze kuondolewa katika mzunguko ni lazima iwe na mbadala. Hatuwezi kusema dawa ifikie asilimia ngapi ya usugu ndipo iondolewe sokoni, zipo nyingine zina asilimia 30 na nyingine 50 na bado tunazitumia kutibu,” alisema.


Usugu wa dawa

Usugu wa malaria ulianza kushuhudiwa miaka ya sitini wakati ugonjwa huo ulipotangazwa kuwa sugu dhidi ya chloroquine katika eneo la Mekong, Vietnam na kusambaa hadi Afrika ambapo vifo vinavyotokana na ugonjwa huo viliongezeka, hasa miongoni mwa watoto.

Wakati chloroquine ilipotengenezwa wanasayansi walifikiri ugonjwa huo ungetokomezwa ndani ya miaka michache, lakini tangu miaka hiyo ya 1950 vijidudu hivyo vimekuwa vikijitengenezea usugu dhidi ya dawa mbalimbali zilizoonesha mafanikio katika kupambana na vijidudu vya malaria mwanzoni.

Tanzania iliachana na chloroquine miaka kadhaa nyuma baada ya usugu kufikia zaidi ya asilimia 50 na kupatikana dawa aina ya Fansider (SP) kabla ya kuachana nayo pia na kutumia Alu.

Rais wa Chama cha Wafamasia Tanzania (PST), Fadhili Hezekiah alisema sababu za usugu wa dawa hutokana na matumizi yasiyofaa au yasiyo sahihi ya dawa.

Alisema inaweza kuwa matumizi kupita kiasi, au matumizi chini ya kiwango.

“Usugu wa dawa pia unaweza kusababishwa na matumizi ya dawa kiholela, yaani kutumia dawa bila kuthibitisha kama tatizo linaendana na dawa,” alisema Hezekiah.

Mkaguzi wa dawa kutoka Mamlaka ya Dawa, Vifaatiba na Vitendanishi (TMDA), Venance Burushi alionya utupaji holela wa dawa baada ya matumizi kwa kuwa hata yakibaki majivu zinaendelea kuwa dawa au kemikali ambazo zinaweza kuleta madhara, hivyo yafaa zirudishwe famasi au vituo vya afya kwa uteketezaji.

“Kuchoma, kutupa dawa ina athari nyingi kwa binadamu, ikiwemo kutengeneza usugu wa vimelea kwa aina ile ya dawa, lakini pia huathiri wanyama na wao hujenga usugu dhidi ya aina hiyohiyo ya dawa,” alisema Bushiri.


Sababu za utafiti

Dk Ishengoma alisema utafiti huo pia umelenga kufundisha watafiti nchini waweze kujenga uwezo wa kitafiti na kuchakata tafiti kisha kuziwasilisha na kujenga mfumo wa kushirikisha wadau serikalini na kwingineko.

“Utafiti huu unafanyika katika mikoa 13 ya Tanzania yenye viwango tofauti vya malaria, lakini pia inahusisha utaratibu wa maabara wa kuchakata sampuli na kuziwasilisha,” alisema.