Dawa ya magugu kufanyiwa utafiti ikidaiwa chanzo cha saratani

Dawa ya kuua magugu kwenye shamba.Kwa sasa dawa aina ya Roundup inafanyiwa utafiti na Taasisi ya Viuatilifu Tanzania (TPRI).Picha ya Mtandao.

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa TPRI, mahitaji ya Roundup ni makubwa yakichukua asilimia 50 ya viuatilifu vyote vinavyotumika nchini. Kiuatilifu hicho kilisajiliwa nchini miaka 20 iliyopita ikiwa ni mbadala wa DDT.

Dar/Arusha. Mamlaka nchini zinajipanga kuondoa hofu inayotokana na viuatilifu vya kuua majani kuhusishwa na ugonjwa hatari wa saratani nchini Marekani.

Hofu hiyo inatokana na raia mmoja wa Marekani, Edwin Hardeman (70) kushinda kesi katika mahakama ya Shirikisho ya San Francisco na hivyo kutakiwa alipwe Sh262 bilioni baada ya kudai kuwa kiuatilifu chapa ya Roundup chenye kiambata aina ya glyphosate, ambacho amedai kimemsababishia saratani aina ya non-Hodgkin lymphoma (NHL).

Hardeman alidai kuwa alianza kutumia kiuatilifu hicho mwaka 1986 na kumsababishia saratani iliyodhoofisha mfumo wake wa kinga.

Kiuatilifu hicho cha Roundup hutumiwa na wakulima wengi, hasa katika nchi za Afrika, kuua magugu kabla ya kupanda mbegu, lakini kwa muda mrefu kumekuwa na mjadala kuhusu athari zake, si barani Ulaya pekee bali hata na Afrika.

Hivi sasa wataalamu wa Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu ya Tanzania (TPRI) watafanya utafiti ili kuthibitisha madai dhidi ya Roundup kuwa inaweza kuwa sababu ya saratani.

“Tutafanya uchunguzi kutokana na taarifa zinazohusisha matumizi ya kiuatilifu hicho na ugonjwa wa saratani. Mpaka sasa hatuna ushahidi wowote mezani,” alisema Mkurugenzi mkuu wa TPRI, Dk Margaret Mollel ambaye alizungumza na The Citizen ambalo ni gazeti dada la Mwananchi.

Alisema kiuatilifu hicho kitaendelea kutumika nchini, licha ya hofu hiyo ya saratani, hadi ushahidi wa kisayansi utakapothibitisha na hivyo kupiga marufuku.

Kwa mujibu wa TPRI, mahitaji ya Roundup ni makubwa yakichukua asilimia 50 ya viuatilifu vyote vinavyotumika nchini. Kiuatilifu hicho kilisajiliwa nchini miaka 20 iliyopita ikiwa ni mbadala wa DDT.

Hata hivyo, Dk Mollel ameshauri wakulima nchini kutumia dawa hiyo kwa umakini.

“Kama vilivyo viuatilifu vingine, Roundup ina sumu. Wakulima wanapaswa kuchukua tahadhari kama wanavyofanya kwenye viuatilifu vingine,” alisema.

Tayari kuna mashitaka zaidi ya 9,000 yamefunguliwa yakiwa na madai hayo dhidi ya kampuni ya Monsanto ambayo ni ya kimataifa inayouza dawa hiyo duniani kote, kwa mujibu wa gazeti la UK Guardian linalotolewa nchini Marekani.

Lakini mjadala wa athari za kemikali za dawa hiyo ni mkubwa.

“Glyphosate hutumiwa na wakulima wa mpunga katika Bonde la Mto Senegal, lakini hakuna utafiti wowote uliofanywa dhidi ya kiambata hicho,” alisema Amadou Diop, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Cheikh Anta Diop cha Dakar akikaririwa na tovutio ya scidev.net.

“Wakati kunapokuwa hakuna msingi wa tuhuma dhidi ya kiambata kwamba kinaweza kuwa na sumu na ushahidi wa kisayansi hauonyesha athari zake kwa binadamu, akili ya kawaida inasema unatakiwa kuacha kuitumia hadi unapopata ushahidi. Huo ndio msimamo ambao Afrika ilitakiwa ichukue.”

Taasisi ya kilimohai nayo iliwahi kufanya utafiti wake na kufikia pendekezo kuwa “athari za muda mrefu za kutumia Roundup zinazidi faida ya kuitumia na hivyo inashauriwa kutumia dawa rafiki kwa mazingira na maisha”.

Kesi iliyotolewa uamuzi nchini Marekani inamfanya Hardeman kuwa mtu wa pili kushinda dhidi ya watengenezaji wa kiuatilifu hicho.

Shauri la Hardeman limetuma ujumbe kwa nchi nyingi ambako Roundup inatumiwa na tayari wakulima nchini Kenya wameanza kuigomea.

Gazeti la Daily Nation limewanukuu waendesha kampeni wakitaka Serikali ipige marufuku.

Moja ya maandiko yanaonyesha kuwa glyphosate inaweza kuwa hatari kwa ngozi lakini inapinga uwezekano wa kuathiri mfumo wa upumuaji na mfumo wa mawasiliano ya homoni. Hata hivyo, kwa hatari inasomeka “inawezekana, hali yake haitabiriki”.

Kuhusu, “hali ya kutotabirika”, Dk Mollel alisema inamaanisha kuwa bado TPRI haijafanya utafiti utakaothibitisha kuwa glyphosate ina visababishi vya saratani.

“Maana yake ni kwamba, hakuna ushahidi wa kutosha kuhusisha Glyphosate na carcinogens,” alisema.

Mtaalamu wa magugu, Ramadhan Kilema alisema kiuatilifu hicho hutumika wakati wa kutayarisha shamba kupambana na magugu badala ya kukwatua.

“Kwa kuwa inatumika tu kutayarisha shamba, hakuna uwezekano wa mazao ya mwisho kupata kemikali za dawa hiyo,” alisema.