Dawa ya ‘vumbi la kongo’ yaendelea kutikisa sokoni
Muktasari:
Licha ya kufutiwa usajili mojawapo ya dawa za kuongeza nguvu za kiume aina ya hensha inayofahamika kama vumbi la kongo, bado imeendelea kuwepo katika mauzo ya mitandaoni.
Dodoma. Licha ya kufutiwa usajili mojawapo ya dawa za kuongeza nguvu za kiume aina ya hensha inayofahamika kama vumbi la kongo, bado imeendelea kuwepo katika mauzo ya mitandaoni.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi umebaini kuwa dawa mbalimbali za kuongeza nguvu za kiume maarufu kama vumbi la kongo, kasongo, mundende au puturuu zimekuwa zikitangazwa kwenye mitandao ya kijamii ikiwamo Instagram, Facebook na Telegram, licha ya kutokusajiliwa rasmi na Baraza la Tiba Asili nchini.
Akizungumza na Mwananchi, Mfamasia wa Baraza la Tiba Asili nchini, Ndahani Msigwa amekiri kuwepo kwa uuzaji wa dawa za tiba asili ambazo hazijasajiliwa rasmi, ikiwemo vumbi la kongo.
Alisema jitihada zinachukuliwa na baraza hilo kukabiliana na biashara hiyo haramu ambayo imeonekana ikishamiri mitandaoni.
“Vumbi la kongo sio aina moja ya dawa, ni jina maarufu linalotumika kwa dawa za kuongeza nguvu za kiume.
“Hatua zinazochukuliwa kwa wale wanaobainika kutangaza dawa za tiba asili ambazo hazijasajiliwa ni pamoja na faini ya zaidi ya Sh1 milioni kwa mtu binafsi na chombo alichotumia kutangazia biashara hiyo,’’ alisema.
Msigwa alitoa rai kwa wanunuzi wa bidhaa za mtandaoni kuwa makini na vitu wanavyonunua, hasa dawa kwani nyingi huwa zina madhara.
“Sisi tumejikita zaidi kusimamia usalama wa dawa hizi na si ufanisi. Ubora wa dawa upo juu ya mtengenezaji wa tiba asili husika ambapo ni lazima kuhakikiwa na kuthibitishwa na baraza kabla ya kuingia sokoni na kutangazwa mitandaoni,’’ alisema.
Kwa upande wa Katibu wa Umoja wa Waganga na Wakunga wa Tiba Asili Tanzania (Uwawata), Lukas Mlipu alisema: “Dawa hii ilikuwa inachanganywa na dawa ya famasia aina ya viagra, kitu ambacho ni kinyume na vigezo vya tiba asilia.
“Bado kuna kazi kubwa huko mbele katika hili, kwani dawa nyingine hazijasajiliwa lakini zipo sokoni kwa jina la tiba asili na zimeendelea kutangazwa mitandaoni”.
Denis Kanuti, mkazi wa Moshi alisema: “Kikubwa ni kuangalia njia ya kuhalalisha dawa hizi za kuongeza nguvu za kiume ambazo mahitaji yake yanazidi kuongezeka siku hadi siku na mwarobaini wake si kuifutia usajili kwa sababu zipo njia nyingi za kuipata na kuitumia na mahitaji ni makubwa”.