Dawa za kulevya yadaiwa kuuzwa hadharani Kiteto

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara, RPC. George Katabazi akitoa elimu kwa wananchi washirikiane na Jeshi hilo kukabiliana na vitendo vya uhalifu vikiwemo ubakaji, na matumizi ya madawa ya kulevya. Picha na Mohamed Hamad Kiteto

Kiteto. Wananchi wa Kata ya Matui wilayani Kiteto mkoani Manyara wamesema, hawana matumaini tena kama vijana wao watawasaidia baaaye kutokana na wengi wao kujihususha na dawa ya kulevya.

Wamesema dawa za kulevya aina ya mirungi na bangi zinauzwa hadharani, huku wauzaji wakijìtapa kuwa hawawezi kufanywa lolote kwa kazi hizo.

Wakizungumza hayo Machi 3, 2023 baadhi ya wananchi wa Kata ya Matui mbele ya Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara, RPC George Katabazi wamesema, hawana matumaini tena kama watakuwa na vijana wa kuwasaidia baadaye kutokana na wengi wao kujihusisha na madawa ya kulevya.

"RPC hapa Matui hatuna matumaini tena kama tutakuwa na vijana wa kutusaidia baadaye...vijana wanavuta bangi wanakula mirungi makundi kwa makundi mchana kweupee...nani wakutusaidia baaaye,” alisema mkazi wa eneo hilo Kidawa Athumani.

Saa hivi mbali na matatizo tuliyonayo ya muda mrefu wakulima na wafugaji kugombea ardhi hili nalo la dawa za kulevya ni janga jingine. Tunaomba Kamanda wa Polisi tuokolee vijana wetu sisi wazazi wametushinda, wanazunguka usiku kucha hawalali nadhani ni hivi vitu vyao wanavyokula,” amesema Richadi Chimosa.

Mkazi mwingine Msafiri Omari alisema wanawake wanaishi kwa hofu kubwa hapo kijijini kwani vijana wao wamebadilika wanabaka na hata kulawiti watoto wadogo.

"Mimi sasa hivi hata shambani sifanyi kazi kwa uhuru hata kidogo… Nimejawa na hofu kubwa tunaombeni jamani mtusaidie kuondokana na hali hii," amesema.

 "Bangi inauzwa hadharani ni makundi kwa makundi ya vijana wanavuta tunawaona na wanatudhuru. Hatuna matumaini ya kesho kama kuna vijana wa kutusaidia, tuna mateja wa baadaye kinachoonekana,” ameongeza.

Akizungumzia madawa hayo Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara, George Katabazi anasema, wazazi, jamii na viongozi wa dini wana nafasi kubwa ya kubadili tabia za watoto wao kutenda matendo mema huku akisema Jeshi la Polisi nalo litaendelea kuwa mstari wa mbele kukabiliana na mapambano hayo.

“Polisi tutawakamata kama kawaida na tunaendelea kuwakamata kazi yetu ni kuwafikisha mahakamani. Viongozi wa dini mnayo nafasi kubwa kuwausia watoto,” amesema RPC George Katabazi

"Mambo yote hayawezi kufanywa na Jeshi la Polisi peke yao, jamii, wazazi na viongozi wa dini mna jambo la kufanya katika kubadilisha vijana hawa. Sisi tutawakamata na kuwapeleka mahakamani ila haitoshi tushirikiane kwa hili ndugu zangu," amesema RPC Katabazi.