Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dawa za kuongeza makalio hatari aisee

Muktasari:

  • Zinaua figo, maini na kusababisha saratani


Dodoma. Wakati baadhi ya wanawake wakizichangamkia dawa za asili za kuongeza ukubwa wa makalio, watalaamu wamesema mpaka sasa hakuna dawa iliyothibitishwa na Mamalaka ya Dawa na Vifaatiba (TMDA) hivyo wajiepushe nazo.

Tahadhari hiyo inatolewa huku matangazo ya dawa hizo pamoja na za kuongeza matiti na ‘hips’ katika mitandao ya kijamii yakiongezeka. Kuibuka kwa mitishamba hiyo ambayo ni mbadala wa dawa za Kichina zilizokuwa zikitumiwa na kuacha madhara.

Hata hivyo, madaktari bingwa wanatahadharisha matumizi ya dawa hizo kwamba zina madhara hasa za kumeza zinazoathiri figo na maini kutokana na kutothibitishwa kisheria.

Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Hospitali ya Bochi jijini Dar es Salaam, Alex Msoka anawataka wanawake wanaotaka kuongeza maumbile kuacha kutumia dawa za kienyeji kwa sababu hazijathibitishwa kisayansi.

“Watu wametumia dawa za kienyeji kuongeza nguvu za kiume, kuondoa fibroid (uvimbe) au kuuweka uso vizuri ila wengi wameathirika kwani maini na figo zimekufa kwa sababu dozi hazifahamiki wanakadiria tu,” anasema.

Dk Msoka amewashauri wanaotaka kuongeza ukubwa wa makalio kutumia njia za kisayansi ingawa ni ghali.

“Kila aina ya upasuaji utakaoamua kufanya ina faida na hasara zake. Ni kawaida kurekebisha makalio kwani hiyo hufanyika hata kwa waliopata ajali yakaharibika,” anasema Dk Msoka.

Mwaka 2018 suala la kuongeza ukubwa wa makalio liliibuka bungeni, Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Suzan Lyimo alipouliza madhara ya kutumia dawa, vipodozi na sindano kuongeza ukubwa.

Akijibu swali hilo aliyekuwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndungulile alisema matumizi ya sindano yana madhara makubwa ikiwamo uwezekano wa kupata saratani.


Hali ilivyo

Kwa taratibu, kabla dawa ya asili haijapewa kibali na Mkemia Mkuu wa Serikali, Mamlaka ya Chakula (TMDA) vikithibitisha mkusanyiko huo wa dawa za asili hauna madhara kwa binadamu.

Kuongezeka kwa dawa za mitishamba kunatokana na gharama kubwa za kuongeza maumbile kwa upasuaji ambao mara nyingi hufanyika nje ya nchi huku dawa za Kichina zilizokuwa zikitoa matokeo ya haraka kubainika kuwa na madhara kama vile kalio moja kuwa kubwa kuliko jingine au mwili kufa ganzi.

Wauzaji wengi wa dawa za kuongeza maumbile ya wanawake wanafanya hivyo kupitia mitandao ya kijamii na gharama zake ni kati ya Sh30,000 hadi Sh120,000 wakati hospitalini, gharama za kubadili makalio ni kati ya Sh12 milioni hadi Sh16 milioni kwa nchi za Uarabuni lakini kwa nchi za Magharibi gharama ni mara mbili au mara nne ya kiasi hicho.

Muuzaji mmoja kwenye mtandao wa kijamii anajinadi kuuza mafuta ya kupaka kwa kati ya Sh50,000 hadi Sh80,000 huku akitahadharisha kwamba:

“Tafadhali baki njia kuu epukana na njia zitakazokuletea madhara kwani naamini afya yako ni bora kuliko kitu chochote kwahiyo ni bora ukakubali kubaki na umbo lako la kawaida kuliko kutumia dawa zingine zenye madhara.”

Wauzaji wa dawa hizi ambazoni ama za kunywa au kupaka, hupanga bei kulingana na ukubwa wa makalio anaoutaka mteja ambao huanzisha inchi moja hadi sita. Anayetaka kuongeza kwa inchi moja hulipa Sh30,000 na inchi mbili ni Sh50,000 wakati inchi tatu ni Sh75,000 na dozi kamili ni Sh120,000.


Wataalamu wanasemaje

Katibu wa Umoja wa Waganga na Wakunga wa Tiba Asili Tanzania (Uwawata), Lukas Mlipu anasema hawazifahamu na hawana dawa za kuongeza ukubwa wa makalio bali wanasikia na kuziona katika mitandao ya kijamii.

“Sisi waganga wa tiba asilia hatuna dawa yoyote inayoongeza makalio. Sisi tunaisikia kama wanavyosia wananchi katika mitandao,” anasema Mlipu.

Hata hivyo, anasema jamii ielewe kuwa tiba asili na tiba mbadala nchini inasimamiwa na Sheria na 23 ya mwaka 2002 ya Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala lililopo chini ya Wizara ya Afya.

Anaishauri Serikali kuwashirikisha waganga wa tiba asili kwenye vikao vya uamuzi wa tiba asili ili kuweka mikakati ya pamoja.

“Ushauri huu ukifanyiwa kazi itarahisisha kuepusha na kudhibiti utitiri wa dawa hizi na kuleta mafanikio na jamii yetu kuwa na ustawi bora kupitia huduma za tiba asili,” anasema.

Mfamasia wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala Tanzania, Ndahani Msigwa anasema hakuna dawa yoyote ya kuongeza makalio iliyothibitishwa nchini.

“Hakuna dawa ya asili ambayo sisi tumeithibitisha ama tumeisajili ya kuongeza ukubwa wa makalio. Hiyo sio tiba, baraza hatuitambui,” anasema Msigwa.

Alisema kitu chochote ambacho kinaweza kubadilisha maumbile ya mtu mara nyingi kinakuwa na madhara ya muda mrefu ambayo mtumiaji hatoyaona kwa wakati huo na kuonya wanaotumia dawa hizo wanahatarisha afya zao.

“Tuwashauri watu wasitumie vitu ambavyo havijathibitishwa na mamlaka husika kwa usalama wa afya zao,” anatahadharisha.

Msigwa anasema hatua zinazochukuliwa kwa wale wanaobainika kutangaza dawa za tiba asili ambazo hazijasajiliwa ni pamoja na kulipa faini ya zaidi ya Sh1 milioni kwa mtu binafsi na chombo alichotumia kutangazia biashara hiyo.

Mmoja wa wataalamu wa tiba ya asili ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, anasema dawa za kuongeza ukubwa wa makalio yenye mchanganyiko wa mitishamba ni ya kupaka kwenye maeneo ambayo mtu anataka yaongezeke.

“Ukichukua full package utatumia kwa siku 15 lakini matokeo kamili ni ndani ya siku 26, hii inaongeza sehemu zote hips na makalio,” anasema.

Anayetaka kuyaongeza kwa inchi moja, anasema atatumia dawa kwa siku nne hadi tano, lakini matokeo yake atayapata ndani ya siku 14 na kwa anayetaka inchi mbili anatumia kwa siku nane hadi 10 na atapata matokeo ndani ya siku 18.

“Kwa ile ya kuongeza ukubwa wa nchi tatu matumizi ya dawa ni kati ya siku 12 hadi 14 na matokeo utayaona ndani ya siku 21,” anasema.

Anasema dawa hizo hazina kemikali, harufu wala maumivu japokuwa zinaweza kusababisha muwasho kidogo katika siku za kwanza.

Alipoulizwa kuhusu ufanisi wa dawa hizo, anasema ni mkubwa na zisipofanya kazi basi mteja hupewa vidonge ambavyo hutengenezwa kiwandani.

“Lakini issue (kesi) hizo hutokea mara chache sana mtu kupaka hii dawa halafu asipate matokeo,” anasema.


Wapenda makalio

Ingawa wengi wa watu wanaofanyiwa upasuaji huo hawapendi kujitangaza, hali ilikuwa tofauti kwa muigizaji na mwanamtindo Muna Love ambaye alifanyiwa upasuaji wa kuongeza ukubwa wa makalio nchini Uturuki mwaka jana.

Muna alijitokeza hadharani na kutamka kuwa anajutia kufanya upasuaji huo kutokana na kuathirika mwilini mwake baada ya kidonda kutopona mapema kama alivyotarajia. Muigizaji huyo aliwashauri wasichana wengine kutothubutu kufanya upasuaji kutokana na hali aliyoipitia.

Mkazi wa Nkuhungu mkoani Dodoma, Sophia Mwenda anasema anatamani kubadilisha maumbile hasa kukuza makalio ila anashindwa kwa sababu ya gharama kubwa wakati yeye hana fedha.

“Asikudanganye mtu, ukiwa na shepu inakufanya kila nguo kukukubali na unavutia, na ukishavutia unajiamini zaidi mbele za watu,” anasema mwanamke huyo.

Sophia anasema waganga wengi wanatangaza kuwa na dawa za kuongeza makalio lakini hofu yake ni kuwa zinaweza kumsababishia matatizo ya kiafya akizitumia.

Mkazi mwingine wa Dodoma, Michael Wambura anasema wanawake wenye makalio makubwa ni kivutio kwa wanaume ndio maana wakipita hutazamwa zaidi.

“Mimi napenda nyama. Zinanivutia na kunipa hisia za mapenzi na hii sio wanaume tu hata wanawake wanalifahamu hilo,” anasema.