DC Bagamoyo amaliza mgogoro ardhi wa miaka 10

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani,  Halima Okash akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Mnindi Kata ya Vigwaza  (hawapo pichani) kwenye mkutano uliofanyika leo Ijumaa Februari 2, 2024. Picha na Sanjito Msafiri

Muktasari:

Mgogoro wa mipaka uliokuwa ukihusisha vijiji vya Mnindi, Vigwaza Mkoa wa Pwani, ulisababishwa na kung’olewa alama za utambuzi wa mipaka.

Bagamoyo. Mgogoro wa mipaka uliokuwa ukihusisha vijiji vya Mnindi, Vigwaza Mkoa wa Pwani kwa zaidi ya miaka 10, umefika tamati baada ya Mkuu wa wilaya hiyo, Halima Okash kuzungumza na wananchi na viongozi wa maeneo hayo kwenye mkutano wa hadhara.

Akizungumza katika mkutano huo leo Ijumaa Februari 2, 2024 katika Kijiji cha Mnindi, DC Okash amesema kuwa alichobaini ni kutowekwa alama za mipaka katika  vijiji hivyo.

 "Nawaagiza wataalamu wa ardhi Ofisi ya Mkurugenzi halmashauri ya Chalinze hakikisheni mnakwenda kupanda mawe yanayoainisha mipaka kati ya vijiji hivi, kazi ambayo nataka ikamilike ndani ya siku tano," amesema.

Amesema ingawa Serikali ina wajibu wa kutoa huduma kwa wananchi wote, lakini kuna umuhimu wa kutambua utambulisho wao kupitia viongozi wa vijiji wanakotoka.

Yusuph Makamba, mkazi wa Kijiji cha Mnindi amesema kuwa agizo alilotoa mkuu huyo wa wilaya linapaswa kutekelezwa kwa wakati, kwani litakuwa mwarobaini wa mgogoro huo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Mnindi, Juma Chambwele amesema kuwa mgogoro huo umekuwa ukimpa wakati ngumu kuhudumia wananchi kwa kushindwa kutambua maeneo yao ya kiutawala.

Naye Diwani wa Kata ya Vigwaza, Mussa Gama amesema kuwa kutobainishwa kwa mipaka hiyo kumekuwa kukichangia mvutano wa viongozi wa vijiji, na hata pindi wanapofika kwake kutaka usuluhishi amekuwa akipata wakati mgumu kuamua.