DC Lushoto amaliza mgogoro wa ardhi wanakijiji na mwekezaji

Wananchi wa Katurupesa wakionyesha mabango kumuomba mkuu wa wilaya ya Lushoto kutatua mgogoro wa ardhi kati yao na Mwekezaji.

Muktasari:

  • Mkuu wa Wilaya la Lushoto mkoani Tanga Kalisti Lazaro amefanikiwa kuzima jaribio la kuuzwa kwa ardhi ya kitongoji kimoja kwa mwekezaji wilayani humo na kuirejesha kwa wananchi.

Tanga. Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Kalisti Lazaro, amemaliza mgogoro wa ardhi katika Kitongoji cha Katurupesa jana Machi 28, 2023, Kata ya Mnazi wilayani humo baada ya mwenyekiti wa kitongoji hicho kudaiwa kumuuzia mwekezaji eneo lenye ukubwa wa ekari 120.

Akizungumza katika mkutano na wanakijiji wa eneo hilo, Kalisti alisema ardhi hio haitauzwa kwa ajili ya kujenga ofisi ya serikali ya kijiji kama yalivyokuwa madai ya mwenyekiti wa kitongoji hicho.

“Hatujauza ardhi kwa ajili ya kujenga zahanati, wala ofisi ya tarafa, wala kujenga shule, leo tuuze ardhi kwa ajili ya kujenga ya ofisi ya kijiji?” alisema Kalisti.

“huyo anayetaka kununua hiyo ardhi mwambieni aache kusumbua wananchi, kama anahitaji ardhi aje halmashauri, yapo maeneo ambayo hayajaendelezwa atapatiwa,” aliongeza Kalisti.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji wilayani humo, Zakayo Ngioko alisema anamshukuru mkuu wa wilaya kwa kutatua mgogoro huo kati ya wananchi wa kitongoji hicho ambao ni wafugaji na mwekezaji anayedaiwa kuuziwa eneo hilo.

“Niwaombe wananchi waendelee kupigania haki yao ili kuepeuka kupoteza haki yao kwa sababu ya ubadhilifu wa watu wengine,” aliongeza Ngioko.

Pia Namayenu Moreto,ambaye ni mkazi wa Kitongoji cha Katurupesa alipongeza uamuzi wa mkuu wa wilaya hiyo akisema kitendo cha kuuza eneo hilo hakikuwa sahihi na ni kinyume na sheria.

“Uamuzi ambao ameutoa mkuu wetu wa wilaya wa eneo letu kutouzwa, Mungu ambariki sana,” alisema Namayenu.