DC Hai aagiza ujenzi shule iliyopigwa tetemeko la ardhi

Muktasari:

Mkuu wa Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro, Juma Irandu amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmasshauri hiyo, Dionis Myunga kuhakikisha ujenzi wa madarasa matatu katika shule ya Msingi Nsongoro iliyopo Kijiji cha Mashua unaanza baada ya madarasa ya shule hiyo kuharibiwa na tetemeko la ardhi.

Siha. Mkuu wa Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro, Juma Irando amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmasshauri hiyo, Dionis Myunga kuhakikisha ujenzi wa madarasa matatu katika shule ya Msingi Nsongoro iliyopo Kijiji cha Mashua unaanza baada ya madarasa ya shule hiyo kuharibiwa na tetemeko la ardhi.

Madarasa ya shule hiyo yaliharibika baada ya tetemeko la ardhi kupiga katika shule hiyo mwaka 2020.

Irandu ametoa agizo hilo leo Jumatano Desemba Mosi, 2021 akiwa shuleni hapo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru ili kuwatia wananchi hamasa ya kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Amesema "Nimepita nimekagua huko na nimeona madarasa ni machakavu na yanahitaji ukarabati, tumeona kuna umuhimu wa kufanya ukarabati mkubwa kwenye madarasa haya"' amesema Irando

“Kutokana na hali halisi naomba mwenyekiti wa Halmashauri na Mkurugenzi kwa pamoja katika fedha zetu za maendeleo tuanze ujenzi wa madarasa matatu hapa katika shule hii,tunafanya hivyo tukijua muda ni mfupi, madarasa hayo yajengwe hapa kabla ya Januari 2022” amesema 

Amesema kuwa wanafanya hivyo kwasababu darasa la kwanza wataanza muda sio mrefu na katika mazingira hayo lazima wapite sehemu salama ya kusomea.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Rajabu Eliasi alisema hali ya miundombinu katika shule hiyo ni mbaya kwani wanafunzi hawana madarasa ya kusomea madarasa matatu yanayobakia ni chakavu yanahitaji ukarabati mkubwa kwani hujaaa maji wakati wa masika.

Imeandikwa na Bahati Chume