DC Kilombero awatoa hofu wananchi baada ya mauaji ya ofisa ardhi
Mkuu wa wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyobya
Muktasari:
- Ofisa ardhi huyo, Zakaria Malika (57), ameuawa na watu wasiojulikana baada ya kumvamia nyumbani kwake na kumshambulia kwa kitu chenye ncha kali kichwani. Amezikwa leo, Julai 21, nyumbani kwao mkoani Iringa.
Morogoro. Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyobya, amewataka wananchi na watumishi wa Halmashauri ya Mji Ifakara kutokuwa na hofu kutokana na mauaji ya ofisa ardhi wa halmashauri hiyo, Zakaria Malika (57), yaliyotokea usiku wa kuamkia Julai 20.
Malika aliuawa na watu wasiojulikana waliomvamia nyumbani kwake na kumshambulia kichwani kwa kitu chenye ncha kali.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, uchunguzi wa awali unaonesha tukio hilo linahusishwa na mgogoro wa ardhi uliodumu kwa muda mrefu kati ya marehemu na watu wengine.
Kutokana na tukio hilo, baadhi ya wananchi na watumishi wa Halmashauri ya Mji Ifakara wameeleza hofu kuhusu usalama wao.
Akizungumzia hali hiyo, Kyobya amewahakikishia wananchi kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea na kazi ya kuwatafuta wahusika wa tukio hilo, huku vikichukua hatua za kuimarisha ulinzi ili kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao unaendelea kuimarishwa.
Amewataka wananchi kuendelea na shughuli zao za kila siku bila hofu na kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola kwa kutoa taarifa zitakazosaidia uchunguzi na kukamatwa kwa wahusika wa mauaji hayo.
"Ni kweli tukio hili limetushtua, si tu watumishi, bali hata wananchi, na hii inatokana na mazingira ya tukio lenyewe, ambalo limetokea mapema majira ya saa mbili usiku.
“Mimi, nikiwa mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hii, nawahakikishia wananchi usalama na nawaomba waendelee na shughuli zao kama kawaida. Vyombo vyetu vya usalama vipo macho," amesema Kyobya.
Amesema baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi na mamlaka nyingine za kiuchunguzi zimeanza kazi, hivyo amewaomba wale wote wenye taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa watuhumiwa watoe ushirikiano.
Katika hatua nyingine, Kyobya amekemea tabia ya kuchukua sheria mikononi na kuwaahidi wananchi kuwa wote waliohusika na mauaji hayo watakamatwa.
Kwa upande wake, Diwani wa Kibaoni, Rashid Namtuka, amesema kutokana na hofu waliyonayo wananchi baada ya mauaji hayo, amepanga kufanya kikao na wananchi kwa lengo la kuwaondoa hofu, lakini pia kuwataka wawe na tabia ya kutambuana.
"Eneo alilokuwa akiishi marehemu limejitenga, na ni eneo ambalo wanaishi watumishi wengi. Hivyo, muda mwingi limekuwa kimya, hali inayoweza kufanya uhalifu kutendeka bila kujulikana haraka.
“Kupitia kikao hicho nitawasisitiza wawe na mazoea ya kutambuana kama majirani ili anapotokea mgeni ajulikane," amesema Namtuka.
Amesema tukio hilo la mauaji limeacha taswira mbaya kwa wananchi kwa kuwa halijawahi kutokea tukio la namna hiyo, licha ya kuwahi kutokea matukio ya wizi mdogo mdogo.