DC Lulandala: Momba tunaunga mkono uwekezaji bandari wa Dar

Momba. Mkuu wa Wilaya ya Momba Mkoani Songwe, Faki Lulandala amesema kuwa Wilaya hiyo inaunga mkono uwekezaji wa uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam kwa kuwa ufanisi wa bandari hiyo utaleta faida kubwa katika wilaya ya Momba.

Pia, Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa anapinga na kukemea baadhi ya watu wakiwemo viongozi wa siasa wanaoeneza upotoshaji na ubaguzi kuhusu uwekezaji huo.

Amesema kuwa viongozi na wananchi wa wilaya hiyo wanaunga mkono mashirikiano kati ya Kampuni ya DP World na TPA na wanaopinga uwekezaji huo wana ajenda zao.

DC Lulandala maesema hayo leo Ijumaa Julai 14, 2023 wakati akizungumza na waandiahi wa habari kuhusu namna ambavyo Wilaya hiyo itanufaika na uwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaam kutokana na wilaya hiyo kuwa na mpaka wa Tunduma.

Amesema kuwa viongozi wa Wilaya hiyo wameamua kuzungumzia uwekezaji huo kutokana na upotoshaji unaoenezwa na baadhi ya watu.

"Kuna watu wameibuka wanapotosha kuhusu mkataba wa Bandari ndio maana nimewaita hapa ili na sisi tuzungumze. Na kwa nini sisi tuzungumze?, ni kwa sababu ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam utatunufaisha Momba hasa mji wa Tunduma" amesema

"Wapo watu wameibuka wanapotosha kuwa nchi imeuzwa, watuambie kama imeuzwa imeuzwa shilingi ngapi" ameeleza

Amesema kuwa baadhi ya watu wanaopinga mkataba huo ni wanufaika wa mifumo ya sasa huku akibainisha kuwa

Kampuni ya DP World ina uwezo mkubwa na mitambo ya kisasa na imewekeza nchi nuingi duniani.

"Wanaopinga ni wanufaika hali ya sasa wanaona kuwa kukiwa na ufanisi katika bandari hiyo watashindwa kunufaika"


Bunge limeridhia makubaliano

TPA na DP World. Sisi tumeamua kuzungumza maana uongo ukisemwa sana watu wanaweza kudhani kuwa ni ukweli, lazima tutoke tuseme na tukemee. Uongo ni uongo tu hata kama ukisemwa na nani" amesisitiza

"DP World imewekeza Uingereza, Marekani. Tunachotaka ni mwekezaji mwenye uwezo. Haijalishi anatoka wapi" amesema

Amesema kuwa Wilaya hiyo inapinga ubaguzi unaofanywa na baadhi ya watu kuhusu uwekezaji huyo.

"Kuna ukaburu umeibuka kuhusu uwekezaji huo, Wanaosema kuwa Rais ameridhia uwekezaji huo kwa vile anatoka Zanzibar huo ni ubaguzi" amesema na kuongeza

"Anasema yeye ni wa Tanganyika, huo ni ubaguzi. Sisi kama wana Momba tunaupinga kwa nguvu zote" amesema

Mkuu wa Wilaya ya Momba, Faki Lulandala.

 Akaribisha wawekezaji Momba

Akizunguza katika mkutano huo, DC Lulandala amesema kuwa Wilaya hiyo inakaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kuwekeza katika Wilaya hiyo.

"Sisi tuna eneo lenye ukubwa wa eka 2000 tunawakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza katika Wilaya yetu bila kujali ni wa ndani au toka nje ya nchi" ameeleza

"Tunachotaka ni mwekezaji mwenye uwezo. Hata DP World anaweza kuja kuwekeza Momba" ameeleza

Amesema kuwa ili kujiandaa na uwekezaji huo kama wilaya imeandaa eneo la bandari kavu ili kutumia fursa hiyo pale uwekezaji wa bandari utakapo kamilika.


 Mapato kupaa Momba

Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa amejitokeza kuzungumzia uwekezaji huo kwa kuwa kama utafanikiwa wilaya hiyo itanufaika na ukusanyaji wa mapato tofauti na sasa.

Amesema kuwa nchi nyingi za SADC zinategemea mpaka wa Tunduma kupitisha mizigo hivyo ufanisi wa bandari ya Dar es Salaam utaleta mabadiliko chanya kwenye ukusanyaji wa mapato Tunduma.

"Kwa sasa kila siku Halmashauri ya Mji Tunduma tunakusanya Sh8 milioni mpaka Sh10 milioni kwa siku kutokana na kupitisha magari. Sasa kama DP World watawekeza tunategemea mapato yatazidi kuongezeka hivyo hatuna sababu ya kupinga uwekezaji huo" ameeleza


 Amshukuru na kupongeza Rais Samia

DC Lulandala amesema kuwa Wilaya hiyo inamshukuru na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka wazi mikataba hiyo hali ambayo ni tofauti na vipindi vya nyuma.

"Tunamshukuru na kumpongeza Rais Mama Samia kwa kuweka wazi mkataba huu na kuupeleka bungeni. Hii inaonyesha kuwa Rais ana nia njema na nchi" amesema

"Wanaopiga kelele ni wale ambao waliomba nafasi ya kuongoza nchi wakashindwa hivyo wanataka kumrudisha nyuma Mama Samai"

"Kwanza wanatafuta waingilie eneo gani maana mwanzoni walijua kuwa mama Samia atashinwa kuongoza sasa wakiona mambo yanaenda vizuri wanakosa cha kuzungumza" amesema

Amesema kuwa wanamshukuru Rais Samia kwa nia yake ya kuruhusu uwekezaji ambao utainufaisha moja kwa moja wilaya ya Momba.