DC Mjema apiga marufuku kuwatoza fedha machinga ili kupewa maeneo

Muktasari:

  • Mkuu wa wilaya ya Arusha, Sophia Mjema amepiga marufuku wafanyabiashara ndogo kutozwa fedha kwa ajili ya kupangiwa maeneo mengine ya kufanyia biashara na kuondolewa maeneo ya sasa.

Arusha.  Mkuu wa wilaya ya Arusha, Sophia Mjema amepiga marufuku wafanyabiashara ndogo kutozwa fedha kwa ajili ya kupangiwa maeneo mengine ya kufanyia biashara na kuondolewa maeneo ya sasa.


Akizungumza na wafanyabiashara hao leo Jumatatu Septemba 27, 2021 katika maeneo ya masoko ya Samunge, Kilombero, Soko Kuu na Kituo kidogo cha mabasi, DC Mjema amesema uhamishaji huo unalenga kutekeleza maagizo ya Serikali.


DC hiyo amesema maagizo yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa wakuu wa mikoa na wilaya kuhakikisha mpangilio mzuri wa wamachinga hao hayana budi kutekelezwa kikamilifu bila upendeleo wa kumwonea yeyote.


"Kumekuwa na malalamiko kwa baadhi ya wafanyabiashara kulipishwa fedha kiasi cha Sh500 na Sh1,000 kwa ajili ya kudurufu majina. Nimepiga marufuku mfanyabiashara yeyote kutoa fedha kwa huduma hii, kwani inatolewa na serikali kupitia halmashauri ya jiji la Arusha," amesema Mjema.


Hata hivyo, amesisitiza kuwa uandikishwaji wa majina utafanywa na viongozi wa wamachinga wenyewe kutokana na kutambuana ili kuepuka migogoro inayoweza kutokea kutokana na baadhi ya wafanyabiashara kuongeza majina ya wasiohusika.


Ameyataja maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wafanyabiashara hao kuwa pamoja na Morombo, Kilombero, Machame na kuwa uongozi wa halmashauri ya jiji wataweka huduma za vyoo pamoja na vibanda na kuwaondoa hofu ya kupangwa maeneo yasiyo na wateja.


Mwenyekiti wa Machinga mkoa wa Arusha, Amina Njoka amekiri kupokea fedha za wafanyabiashara hao akisema walizitumia kama posho kutokana na kazi hizo wanafanya pasipo malipo yoyote kutoka serikalini.


"Lakini kupitia agizo hilo la Mkuu wa wilaya Mjema sitapokea pesa yoyote kuanzia sasa kazi hii itafanyika kwa umakini na hatutaruhusu wafanyabiashara wadogo kutoka nje ya mkoa wa Arusha," amesema Njoka.

Mmoja wa wafanyabiashara hao katika soko la Kilombero amesema wanashukuru serikali kwa kusimamia vyema na kusikiliza changamoto zao lakini uandikishwaji ukamilike mapema ili waendelee kujitafutia kipato.