DC Moshi atoa onyo kwa vijana kuhusu vurugu za uchaguzi
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava akizungumza na vijana Kilema Kati.
Moshi. Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava amewataka vijana kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba, akisisitiza kuwa ni jukumu lao kulinda utulivu katika maeneo yao.
Akizungumza Mei 19, 2025, wakati wa kufunga mashindano ya Yuvecup League yaliyofanyika kata ya Kilema Kati, Mnzava alisema Serikali haitavumilia makundi yanayopandikiza chuki au kuhamasisha vurugu kwa vijana.
“Vijana wenzangu, tusikubali kurubuniwa na mtu yeyote au taasisi yoyote inayotaka kutuvuruga. Serikali yetu ipo imara na uchaguzi utafanyika kama kawaida. Sisi vijana hatupaswi kuwa mawakala wa uhalifu, bali tuwe walinzi wa amani,” amesema Mnzava.
Aidha, aliwataka vijana kuachana na tabia za kihalifu kama wizi, matumizi ya dawa za kulevya na unywaji pombe uliokithiri. Aliongeza kuwa si busara kutaka mafanikio ya haraka kwa njia zisizo halali kwani huo ni mtego wa kupoteza nguvu kazi ya taifa.
“Tusikubali kuingizwa kwenye makundi ya kuhamasisha mgomo wa uchaguzi. Wapo wanaotaka vijana wasishiriki kwenye uchaguzi, lengo lao ni kusababisha vurugu. Serikali ipo macho na watu hao hawatafanikiwa,” amesisitiza.
Mnzava amewahimiza vijana kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi huo na kuwachuja kwa makini wagombea wote watakaojitokeza, akieleza kuwa Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa ya maendeleo.
Katika hatua nyingine, alihamasisha vijana kutumia fursa ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri kwa ajili ya kuanzisha miradi ya kiuchumi.
“Ni muhimu vijana kujiunga kwenye vikundi ili wawezeshwe kupata mikopo. Tumeelekeza wataalamu kwenye sekta mbalimbali wasimamie vizuri matumizi ya mikopo hiyo ili iwasaidie kuinua hali zao za maisha,” amesema.
Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Moshi, Yuvenal Shirima.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Wilaya ya Moshi Vijijini, Yuvenal Shirima amesema wamejipanga kuhamasisha vijana kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi huo.
“Tumekubaliana kuwahamasisha vijana kugombea nafasi za udiwani na ubunge. Hatutamuacha nyuma kijana yeyote mwenye nia ya kweli. Tunakuomba mkuu wetu utuunge mkono,” alisema Shirima.
Aidha, ameeleza changamoto ya upatikanaji wa mikopo ya asilimia 10 akidai kuwa baadhi ya vijana hukosa kutokana na kutotimiza vigezo.
“Hili limekuwa changamoto kwa vijana wetu, wengi hukataliwa kwa kukosa sifa. Tunaiomba Halmashauri iweke utaratibu wa kutoa semina ili vijana waelewe vigezo na kunufaika na mikopo hiyo,” alisema.
Shirima alimalizia kwa kusema kuwa mwaka huu vijana watahakikisha Rais Samia anapata kura za kishindo, “iwe jua au mvua, iwe mchana au usiku.”