DC mteule ahojiwa na polisi dakika 50, Rais CWT…

Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Japheth Maganga akizungumza kwenye mkutano wa chama hicho, kushoto kwake ni Rais wa Chama hicho Leah Ulaya. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Mara baada ya kumaliza kuhojiwa na polisi kuanzia saa 4:36 hadi saa 5:24 asubuhi  nje ya ukumbi wa mkutano huo unaofanyikia Hoteli ya Regal Naivera, Mtaa wa Bombo jijini Tanga, Ulaya alirejea ukumbini na baadaye kidogo alitoka nje.

Tanga. Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Japheth Maganga ambaye ameteuliwa kuwa mkuu wa wilaya ameshiriki kuongoza mkutano wa viongozi wa chama hicho jijini Tanga huku akisema kwa sasa hawezi kueleza kwanini hajaripoti katika wilaya aliyopangiwa ya Kyerwa, mkoani Kagera

Vilevile, Maganga alihojiwa na Mkuu wa Upelelezi wa Polisi Mkoa wa Tanga na Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Tanga zaidi ya dakika 50 lakini si yeye wala wanausalama hao walioweka wazi sababu za mahojiano hayo.

Maganga na Rais wa CWT, Leah Ulaya waliteuliwa wiki iliyopita na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa wakuu wa wilaya lakini wakati wenzao wakiapishwa kwenye maeneo yao leo Jumatatu, Januari 30, 2023 wao wapo Tanga wakiongoza mkutano wa viongozi wakuu wa CWT.

Ulaya aliteuliwa kuwa DC wa Mbogwe, Mkoa wa Geita ambapo wenzake wanaapishwa leo Jumatatu na Mkuu wa Mkoa huo, Martin Shigela.

Mara baada ya kumaliza kuhojiwa na polisi kuanzia saa 4:36 hadi saa 5:24 asubuhi nje ya ukumbi wa mkutano huo unaofanyikia katika Hoteli ya Regal Naivera, Mtaa wa Bombo jijini Tanga Maganga alirejea ukumbini na baadaye kidogo alitoka nje.

Nje ya ukumbi ambapo Mwananchi Digital limeweka kambi, Magamba amesema, “kwa sasa nimeziba mdomo labda usubiri tutakapomaliza kikao ndipo nitazungumza kuhusu nafasi ya U-DC na CWT."

Wakati Maganga akisema hayo, Rais wa CWT hakutoka ndani ya ukumbi wa mkutano huo huku maofisa wa CWT wakisema hajaruhusiwa kuzungumza na vyombo vya habari.

Kitendo cha viongozi wakuu hao wa CWT kuonekana Tanga wakati wenzao wakiapishwa kimezua mjadala mitandaoni na kuna taarifa ambazo hazijathibitishwa kwamba wameomba wateuliwe wengine kwenye nafasi hizo za U-DC ili kuwawezesha kuendelea na majukumu yao katika chama cha walimu.


Endelea kufuatilia mitandao yetu kwa habari zaidi