DC Muheza awaita wakulima kusajiliwa

Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Halima Bulembo

Muktasari:

  • Mkuu wa Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga, Halima Bulembo amewataka wakulima kujitokeza kujiandikisha na kujisajili kwenye Ofisi za serikali za vijiji vyao ili waweze kunufaika na mpango wa Serikali wa kuwapunguzia makali ya bei ya mbolea kupitia ruzuku.

Muheza. Mkuu wa Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga, Halima Bulembo amewataka wakulima kujitokeza kujiandikisha na kujisajili kwenye Ofisi za serikali za vijiji vyao ili waweze kunufaika na mpango wa Serikali wa kuwapunguzia makali ya bei ya mbolea kupitia ruzuku.

Wito huo ameutoa wakati akizindua usajili kwa wakulima katika wilayani hiyo.

Amesema kuwa Serikali imeamua kutumia mfumo wa kidigitali kutekeleza mpango wa ruzuku ya mbolea ili kuongeza ufanisi, kupunguza mianya ya udanganyifu Pamoja na gharama.

Mkuu huyo wa Wilaya ameeleza kuwa mfumo huo utafanya kazi kwa mkulima aliyesajiliwa ataenda kwa mfanyabiashara wa mbolea aliyesajiliwa kwa ajili ya kununua mbolea na kuonyesha namba ya utambulisho aliyopewa wakati wa usajili.

"Serikali za vijiji, viongozi, watendaji na mabalozi sambamba na maofisa ugani naomba mshiriki kikamilifu katika zoezi la usajili wa wakulima na utoaji wa ruzuku ili kuhakikisha mkulima anafaidika na jambo hili" amesisitiza Mkuu huyo wa Wilaya.

Baadhi ya wakulima walioshiriki wenye uzinduzi huo wamesema kuwa mfumo wa huo wa usajili umekuja wakati muafaka na kwamba itawasaidia kuongeza uzalishaji.

Amani Hatibu Hella amesema mfumo huo ni mzuri hauna dhuluma na kwamba anaimani utawasaidia kuongeza tija katika kilimo chao.

Hata hivyo ofisa Kilimo wa Wilaya ya Muheza, Hoyange Mbwambo amesema tayari wakulima 998 wameshaingizwa kwenye mfumo huo wa kusajiliwa na kwamba wakulima hao ni wakutoka kata nane za wilaya hiyo.