DC Njombe: Tuwakinge wanafunzi dhidi ya baridi
Muktasari:
- Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Kissa Kasongwa ameshauri mamlaka za elimu kuangalia uwezekano wa kusogeza mbele muda wa kuanza masomo ili kuwakinga wanafunzi na baridi kali jambo ambalo limeungwa mkono na Kamishna wa Elimu, Dk Lyabwene Mtahaba
Njombe. Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Kissa Kasongwa ametoa wito kwa mamlaka za elimu kubadilisha muda wa kufika shule bila kuathiri masomo, kama njia mbadala ya kuwakinga wanafunzi dhidi ya baridi kali wilayani humo.
Wito huo umetoka na ukweli kuwa katika kipindi hiki cha baridi, wanafunzi wengi kwenye shule mbalimbali za msingi, sekondari na hata vyuo mkoani Njombe, wamekuwa wakitetemeka mikono na kukosa nguvu ya kuandika (kukakamaa).
Awali, ilikuwa kawaida kwa wanafunzi hao kutengeneza makopo na kuweka moto ndani yake kwa ajili ya kuota darasani jambo ambalo kwa sasa halifanyiki.
Licha ya baridi kali inayofikia nyuzi joto 5 kwa leo, wanafunzi hawanabudi kufika shule na kuhudhuria vipindi vyote huku sare za shule ikiwa ni zilezile, sweta na suruali za vitambaa zinazopitisha baridi.
Hata hivyo Kamishna wa Elimu Tanzania, Dk Lyabwene Mtahaba amesema ikiwa lengo la Mkuu wa Wilaya ya Njombe la kuomba muda wa masomo usogezwe mbele ili kulinda watoto wasidhurike na baridi linapaswa kufanyiwa kazi.
“Kama anataka kulinda watoto wasidhurike kiafya na masomo yaendelee kuna baya ndugu yangu? DC anataka kulinda watoto hili halina tatizo,” alisema Dk Mtahaba.
Akizungumza na Mwananchi DC Kasongwa amesema baridi ni kali zaidi nyakati za asubuhi.
“Wakuu wa shule na bodi za shule zinapaswa kuangalia upya muda ambao wanafunzi wanachukuliwa na mabasi nyumbani ili kupelekwa shuleni,” amesema DC huyo.
Amesema changamoto hiyo ameiona hasa Njombe mjini ambapo wanafunzi wanafuatwa nyumbani saa kumi na moja asubuhi lakini ni bora wafuatwe saa kumi na mbili kwasababu muda angalau baridi limepungua.
"Masomo yakianza saa mbili kamili nafikiri siyo mbaya kama kwenye shule tutaridhia bila ya kuathiri muongozo wowote wa elimu lakini pia kuangalia mustakabali wa hawa watoto ambao wanakwenda shule," amesema Kasongwa.
Amesema mikoa ambayo kipindi hiki huwa kuna baridi shule na mamlaka za elimu zinaweza kuziangalia kwa jicho tofauti ili kuwasaidia wanafunzi hasa wale wenye umri mdogo.
"Unakuta mtoto amebebwa kwenye ‘school bus’ anazungushwa weee mpaka anafika shule unakuta tayari hali siyo nzuri kwa sababu wameamshwa mapema saa kumi na moja, ni ushauri tu kwa mamlaka za elimu kuangalia hili," amesema Kasongwa.
Amewataka wananchi kufuatilia ushauli unaotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), ili kuchukua tahadhari hasa kwa watoto kwa kuwavalisha nguo nyingi wanapoenda shuleni.
Mmoja wa wananchi wa Mkoa wa Njombe, Juliana Thomas, amesema ni kweli wazazi wanatakiwa kuwa makini katika kipindi hiki cha baridi kwa kuwasitiri watoto kwa nguo nzito.
"Kwasababu mwanafunzi anapokuwa darasani na baridi inapokuwa kali inaweza kumuathiri katika kumsikiliza mwalimu na hata katika kuandika mikono inakuwa na baridi hasa anapokuwa hajavaa gloves," amesema Thomas.