DC Shaka ataka uchunguzi kisa mtoto kufanyiwa ukatili
Muktasari:
- Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, amelaani vikali kitendo cha mtoto wa mitatu (jina limehifadhiwa), kupigwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili pamoja na kuchomwa na maji ya moto kwenye makalio.
Morogoro. Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, amelaani vikali kitendo cha mtoto wa mitatu (jina limehifadhiwa), kupigwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili pamoja na kuchomwa na maji ya moto kwenye makalio.
Matukio hayo yanadaiwa kuanywa na mtu anayetajwa kuwa ni shangazi wa mtoto huyo, aliyekuwa akimlea katika Kijiji cha Majambaza, Kata ya Msowelo, wilayani Kilosa.
Akizungumza mara baada ya kufika katika Kituo cha Afya cha Mtakatifu Joseph, kilichopo Dumila ambako mtoto huyo anapata matibabu, Shaka ameagiza Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa (DED), kulifuatilia suala hilo.
DC Shaka amesema baada ya kufika katika kituo hicho, na kuona hali ya mtoto huyo, ni dhahili kuwa mtoto huyo amepitia maisha magumu na ya mateso, ambayo inadaiwa kumsababishia madhara ya kisaikolojia.
"Mimi na kamati yangu ya ulinzi na usalama, tumemkagua mtoto na tumeona namna alivyounguzwa na kusababishiwa majeraha makubwa sehemu za makalio, lakini pia ana alama za fimbo na kufinywa kwenye mgongo, mapaja na miguuni," amesema Shaka.
Shaka amesema kuwa taarifa alizopata zinaeleza kuwa mama mzazi wa mtoto huyo yuko mkoani Singida ambako alichukuliwa na ndugu zake baada ya kupata matatizo ya afya ya akili, huku mtoto akichukuliwa na mjomba wake.
Hata hivyo inadaiwa kuwa, aliyefanya ukatili huo, mke wa mjomba wa wa mtoto huyo (jina bado hajafahamika).
Kufuatia tukio hilo DC Shaka amemuagiza DED kumuhoji Mtendaji wa Kata, Mtendaji wa Kijiji na Ofisa Ustawi wa kata hiyo, ili waeleze kwa nini walishindwa kuchukua hatua wakati tayari taarifa za ukatili huo walishazipata.
"Hawa Watendaji na Ufisa Ustawi, walikuwa na taarifa za ukatili huu, na kwa kutotambua wajibu wao, walizikalia taarifa hizi, mpaka mtoto huyu anapata madhara,” amesema Mkuu wa Wilaya huyo na kuongeza;
“Sasa katika uchunguzi tunaofanya na vyombo vyangu vya ulinzi na usalama, tukigundua kuna uzembe wowote umefanywa na hawa watendaji, hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao."
Pia Shaka ameamuagiza OCD kuhakikisha mama aliyefanya ukatili huo pamoja na mume wake wanakamatwa haraka na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa kituo hicho cha afya, Dk Seleman Sakoro, ameeleza kuwa baada ya uchunguzi wa kitabibu, walibaini kuwa majeraha aliyokuwa nayo mtoto huyo, hayakuwa mapya na hayajawahi kupata matibabu yoyote.
Dk Sakoro amesema kwa sasa mtoto huyo anaendelea vizuri tofauti na alivyofukishwa hospitalini hapo na kwamba madaktari wanaendelea kumpatia matibabu ambapo ikitokea kama watakaona kuna huduma za ziada wanaweza kumuhamishia katika Hospitali ya Wilaya ama ile ya Rufaa Mkoa wa Morogoro.
Kwa sasa mtoto huyo anahudumiwa na Serikali chini ya uangalizi wa mlezi na msimamizi wa kituo cha watoto yatima cha Dumila, Coroline Matemu, ambaye ndiye aliibua ukatili huo uliokuwa ulifanywa dhidi ya mtoto huyo.
Caroline amesema kuwa alipata taarifa za ukatili huo kutoka kwa Mtendaji wa Kijiji ambapo baada ya kufika nyumbani alikokuwa akiishi mtoto huyo, alimkuta akiwa na majeraha huku akikosa huduma, hivyo aliamua kumchukua na kumpelekea hospitali.
Greyson Ng'umbi ni mmoja wa wakazi wa Kata ya Msowelo, yeye ameliomba jeshi la polisi kuhakikisha mama aliyefanya tukio hilo pamoja na mume wake ambaye ni mjomba wa mtoto huyo wanakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adamu Malima, akiwa katika ziara wilayani humo, amekutana na taarifa hizo na hivyo kutoa maelekezo ya kuhakikisha matukio ya ukatili wilayani humo na mkoa kwa ujumla yanashughulikiwa ipasavyo na kukomeshwa kabisa.