DC Tabora aahidi manispaa kutopata hati chafu

Muktasari:

Mkuu wa Wilaya ya Tabora ameahidi kuwa Manispaa ya Tabora kwa mwaka huu wa fedha haitapata hati chafu kutokana na kazi nzuri inayofanywa na watendaji na madiwani wa Manispaa ya Tabora.

Tabora. Mkuu wa Wilaya ya Tabora ameahidi kuwa Manispaa ya Tabora kwa mwaka huu wa fedha haitapata hati chafu kutokana na kazi nzuri inayofanywa na watendaji na madiwani wa Manispaa ya Tabora.


Akizungumza katika Baraza maalum la Madiwani leo Jumamosi Septemba 25, Mkuu wa Wilaya ya Tabora Dk Yahaya Nawanda amesema ni lazima Manispaa ifanye vizuri katika makusanyo ya mapato kutokana na mwenendo unaoendelea Sasa hivi.


Amesema kuanzia Julai Agosti, makusanyo yanaendelea vizuri na lengo ni kufikisha asilimia 70 ifikapo Desemba mwaka huu.
"Mwaka huu Manispaa hatutaki hati chafu, iwe mvua au jua ili tuezeke maboma yetu ya majengo yakiwemo ya shule na zahanati," amesema.

Amesema tangu ateuliwe kuwa mkuu wa Wilaya ya Tabora ametembelea kata 28 kati ya 29 na kuulizwa na wananchi maswali 488 ambayo amesema atayatolea ufafanuzi.
Naye Meya wa Manispaa ya Tabora, Ramadhan Kapela amempongeza mkuu wa Wilaya kwa kazi nzuri anayofanya.


Amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuwateua viongozi wanaotoa Ushirikiano kwa wananchi na viongozi waliopo Tabora.


Amewataka madiwani na watendaji kumpa Ushirikiano mkuu huyo wa wilaya ili atekeleze majukumu yake kikamilifu.

Imeandikwa na Robert Kakwesi, mwananchi
[email protected]