DCEA yaja na operesheni maeneo yanayouzwa shisha

Muktasari:

  • Wanaotumia shisha kuvuta dawa za kulevya wapo hatarini kukamatwa baada ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kutangaza kuanza operesheni dhidi yao.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), imetangaza operesheni katika maeneo yanayouza shisha, ili kuwabaini wanaotumia dawa za kulevya ‘unga’.

 Operesheni hiyo inakuja katika kipindi ambacho kumekuwepo na madai ya uwepo wa watu wanaotumia shisha kuvuta dawa za kulevya.

Hayo yameelezwa jijini Dar es Salaam leo, Alhamisi Januari 25, 2024 na Kamishna Mkuu wa DCEA, Aretas Lyimo alipozungumza na waandishi wa habari na kusema watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kisheria.

“Tutatembelea kumbi na hoteli zinakouzwa shisha, tutapima mitungi ya shisha ili kubaini kama kuna uchanganyaji na dawa za kulevya na tukigundua tunawakamata wahusika," amesema.

Operesheni hiyo pia itahusisha maeneo ya nchi kavu ikiwemo kwenye mashamba ya dawa za kulevya, mipakani na kwenye vijiwe vya usambazaji na utumiaji wa dawa za kulevya.

Aidha, ameeleza operesheni ya mwaka huu itahusisha maeneo ya baharini ikiwemo katika fukwe na katikati ya bahari.

Wauza shisha

Erasto Mrusha, mmoja meneja wa moja ya kumbi kubwa za starehe jijini Dar es Salaam, amesema hata yeye anasikia uwepo wa watu wanaochanganya dawa za kulevya kwenye shisha.

"Sisi kwetu hatufanyi hivyo, kikubwa tunachofanya ni kuweka ladha mbalimbali katika shisha, mteja anachagua harufu anayopenda lakini si dawa za kulevya," amesema.

Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kuchanganya dawa za kulevya katika shisha, mfanyabiashara wa mitungi ya shisha Dar es Salaam, Dami Lohora amesema inawezekana.

Amesema namna inavyowezekana kuchanganya ladha mbalimbali za moshi, ndivyo inavyofanyika katika dawa za kulevya.

Lakini, amesema wengi wanaochanganya na dawa za kulevya ni wale wanaomiliki mitungi ya shisha ndani kwao kwa matumizi binafsi.

"Sina uhakika na maeneo ya starehe kama wanaochanganya, lakini wale wanaonunua mtungi kwa ajili ya matumizi yake binafsi wengi waachanganya na dawa za kulevya.

"Wanakuwa huru kwa sababu anatumia ndani kwake. Ukichanganya kwenye kumbi za starehe kila atakayevuta Moshi huo lazima alewe," amesema.

Amependekeza uchunguzi huo ufanywe kwa wanaomiliki shisha kwa matumizi binafsi nyumbani, akisisitiza ndiyo hasa wanaochanganya na dawa za kulevya.

Wanne wakamatwa

Katika hatua nyingine, Kamishna Lyimo amesema mamlaka hiyo imemkamata kinara wa mtandao wa wafanyabiashara wa dawa za kulevya aina ya cocaine nchini.

Pamoja na mtuhumiwa huyo, amesema dawa hizo gramu 692.336 zimekamatwa zinazowahusisha watuhumiwa wanne.

Kuhusu mfanyabiashara huyo, amesema alikuwa akitafutwa tangu mwaka 2000 na hatimaye amekamatwa Boko, jijini Dar es Salaam.

"Amekamatwa na washirika wake watatu na kati yao wawili wamekamatwa jijini Dar es Salaam na mmoja amekamatwa mkoani Mbeya," amesema.

Kwa mujibu wa kamishna huyo, mfanyabiashara huyo wa mtandao wa cocaine ana wabebaji 10 kwa wiki wanaotumia tumbo kusafirisha dawa hizo kutoka eneo moja kwenda lingine.

Akifafanua hilo, ameeleza wabebaji hao humeza dawa hizo tumboni au kuweka kwenye maungo ya mwili.

"Wabebaji huzimeza zikiwa katika mfumo wa pipi ambapo kwa mara moja mtu mmoja hubeba kuanzia gramu 300 hadi gramu 1,200 na baadhi wanaweza kubeba hadi gramu 3,000 kwa wakati mmoja," amesema.

Watu maarufu

Kamishna huyo ameeleza kufanyika kwa uchunguzi wa kubaini watu maarufu wakiwemo wasanii wanaotumika kusafirisha dawa hizo.

Amesema ni vigumu kuthibitisha uwepo wa watu hao, lakini mamlaka hiyo inafanya uchunguzi kubaini hilo.

Uchunguzi huo, amesema utafanyika kwa kuwapima wale wanaohisiwa kufanya hivyo na wakibainika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.