Hatari ya shisha kwa vijana katika kifua kikuu

Dar/Mikoani. Ni kawaida siku hizi katika kumbi za starehe mijini kukuta mitungi ya shisha juu ya meza, huku watumiaji wakichangia kilevi hicho. Je, unajua kuna uwezekano mkubwa mtumiaji kupata maambukizi ya Kifua Kikuu (TB)?

Ijapokuwa hakuna utafiti wa moja kwa moja Tanzania unaoonyesha shisha ni chanzo cha TB, nchini Uswizi kupitia utafiti uliofanywa na Dk Anna Marchetti na kuchapishwa katika jarida la afya la ‘European Journal of Case Reports in Internal Medicine’ mwaka 2020 umebainisha kuwa kilevi hicho ni chanzo cha ugonjwa huo unaoshambulia mapafu.

Katika utafiti huo, baada ya mgonjwa mwenye umri wa miaka 20 aliyekuwa na kikohozi kikali kwa miezi mitatu, kupimwa na kubainika kuwa na TB, uchunguzi uliofanywa uligundua kuwa chanzo chake ni shisha.

Katika utafiti huo unaoitwa ‘Uvutaji wa shisha kama sababu ya hatari ya kusambaza kifua kikuu,’ uchunguzi wa X-ray na CT Scan wa kifua, sampuli za makohozi, uwapo wa mycobacteria kwa mgonjwa huyo vilibainisha maambukizi katika mapafu na kifua kikuu na kwamba mgonjwa huyo alikuwa mtumiaji wa shisha mara kwa mara.

Dk Marchetti anamalizia katika utafiti wake kwa kutoa ushauri kuwa uvutaji wa shisha ni sababu inayoweza kueneza ugonjwa wa kifua kikuu kutokana na tumbaku iliyomo au kuchangia bomba moja la kuvutia.

“Madaktari lazima waulize wagonjwa kuhusu uvutaji wa shisha ikiwa anashukiwa kuwa na TB. Iwapo mgonjwa mtumiaji wa kilevi hicho atathibitishwa kuwa na TB, watu wote walioshiriki naye kutumia shisha watafutwe na mtungi husika usitumike tena,” alipendekeza Dk Marchetti.

Makala hii imechunguza ulevi wa shisha katika muktadha wa hatari ya kusababisha maambukizi ya Kifua Kikuu, hasa kwa kundi la vijana ambao ndio watumiaji wakuu katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Dodoma na Tabora.

Katika kumbi za starehe jijini Dar es Salaam, shisha inavutwa kwa kutumia mrija maalumu (filta) ambao kila mtumiaji huwa na wake, hivyo hupokezana kuivuta.

Gazeti hili limegundua hali tofauti ya uvutaji wa shisha mikoani.

Tabora katika moja ya klabu za usiku iliyopo mjini maeneo ya Isevya, shisha huvutwa bila kuwapo ‘filta’ hivyo kusababisha watumiaji kuchangia bomba moja.

Janeth Marwa, mtumiaji wa kilevi hicho mkoani Tabora anasema hapendi kutumia filta kwa sababu inamchelewesha kupata ‘stimu’.

“Nilikuwa natumia filta nilivyokuwa Dar, ila nimekuja huku nimezoea bila filta naona kama nikiitumia sitapata stimu ninazozitaka,” anasema.

Hata hivyo, mwandishi alipomtafuta meneja wa klabu hiyo kwa masharti ya kutotajwa jina lake na la ukumbi huo wa starehe alisema filta zipo ila hutolewa kwa anayezihitaji.


Kauli ya Serikali

Meneja Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma (NTLP), Dk Peter Neema alipoulizwa kuhusu hatari ya watumiaji wa shisha kupata TB alisema uwezekano wa kupata maambukizi upo endapo kuna mtu aliyeathiriwa na ugonjwa huo kati ya wanaochangia au uvutaji kupindukia utakaoharibu mapafu.

“Ugonjwa wa Kifua Kikuu unaambukizwa kwa njia ya hewa pale mtu mwenye vimelea vya TB anapokohoa au kupiga chafya.

“Matumizi ya shisha yanahusisha uvutaji na upulizaji wa moshi ambao kwa namna moja au nyingine huwa na uwezekano wa kuchochea mtu kupata vimelea iwapo mmoja kati ya wavutao atakuwa na vimelea hivi na hajaanza matibabu,” alisema Dk Peter.

Alisema bado hakuna utafiti wa moja kwa moja kubaini ongezeko la wagonjwa wa TB unaosababishwa na uvutaji wa shisha.

“Hata hivyo, kwa namna nyingine uvutaji wa shisha kwa kipindi cha muda mrefu unaweza kuathiri mapafu na hivyo mtu kuwa na uwezekano sawa na mvutaji wa sigara katika kupata TB,” alifafanua.

Serikali katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 imepitisha ushuru wa asilimia 30 wa bidhaa hiyo, huku ikitaja lengo la kufanya hivyo ni kujumuisha bidhaa mpya zinazotumika kama mbadala wa tumbaku ambazo pia zina athari sawa na tumbaku kwa ajili ya udhibiti.

“Kutoza ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha asilimia 30 kwenye sigara na bidhaa za aina hiyo zinazotumia mbadala wa tumbaku zinazotambulika kwa Hs code 2402.90.00; tumbaku inayovutwa kwa kutumia bomba la maji inayotambulika kwa Hs code 2403.11.00; na sigara za kielektroniki, shisha na bidhaa za aina hiyo zinazotambulika kwa Hs codes 8543.40.10, 8543.40.90 na 9614.00.00,” inaeleza Bajeti Kuu ya Serikali 2023/2024.


Watengenezaji shisha hatarini zaidi

Edwin Jacob (19), maarufu ‘Dogo Ed’ ni mtengenezaji wa shisha katika kumbi moja ya starehe iliyopo Sinza, jijini Dar es Salaam, anasema kwa siku moja mwishoni mwa juma anatengeneza wastani wa shisha 17 hadi 25 za ladha tofauti, huku zote akilazimika kuzijaribu (kuvuta) kabla hazijaenda kwa mteja.

“Siku za wikiendi wateja wanakuwa wengi, unaweza kuuza mitungi 17, 20 au siku nyingine hata 25. Kuhusu kuijaribu kama ladha imekolea vizuri lazima nivute kwenye bomba ili nijue na wakati mwingine ili moto ukolee,” anasema.

Edwin anasema changamoto anazokutana nazo ni kukaa karibu na moto muda mrefu ambao anautumia kuandaa kilevi hicho ambacho anasema kinapendwa, zaidi  na vijana.

“Mimi sioni shida katika kuvuta (wakati wa kujaribu) ila naumia zaidi na moto ninaoutumia muda wote maana unaunguza kweli,” anasema.

Dk Zainabu Hussein kutoka Kituo cha Afya cha Shirika la Reli Tanzania (TRC) kilichopo Dodoma, anasema watengenezaji wa shisha wapo hatarini kupata maambukizi ya TB kwa sababu wanazijaribu kupitia bomba la shisha ambalo kuna baadhi ya wateja wao wanalitumia wakati wa kuvuta.

Anasema kama watengenezaji wa kilevi hicho ni zaidi ya mmoja, hatari ni kubwa zaidi.

“Hatari inakuwapo zaidi kama ukumbi wa starehe utakuwa na watengeneza shisha zaidi ya mmoja kwa sababu watachangia bomba la mtungi wa shisha katika kutengeneza, jambo ambalo linasababisha maambukizi ya TB kama mmoja wao ana vimelea hivyo,” anasema.


Bei ya shisha

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa makala haya umebaini bei za shisha hutofautiana kulingana na hadhi ya eneo husika, ikianzia Sh10,000 hadi Sh30,000.

Katika maeneo ya Mwenge, Tabata na Sinza jijini Dar es Salaam kilevi hicho kinauzwa Sh15,000, lakini katika kumbi za starehe za Mikocheni, Masaki na Oysterbay kinauzwa Sh20,000 hadi Sh30,000.

Mwandishi pia alibaini kuwa shisha huwekwa ladha kadhaa kama vile vanila, strawberry, mint, chocolate au kahawa, ili kuwavutia wavutaji. Ladha hizo zinatajwa kuwa kivutio cha mabinti ambao wameingia kwa kasi kwenye uvutaji huo.


Wanachuo vinara

Katika uchunguzi wa mwandishi wa makala haya, umebaini katika majiji ya Dodoma na Dar es Salaam wateja wakubwa ni wanachuo ambao hutumia fedha za kujikimu kuvuta shisha.

Magdalena John (si jina halisi), mwanafunzi wa chuo jijini Dodoma anasema haiwezi kupita wiki moja bila kuvuta shisha kutokana na hamu anayoihisi endapo hajavuta.

“Kila wikiendi mimi na rafiki zangu tunachanga fedha kwa ajili ya kwenda kuvuta shisha (anataja eneo maarufu jijini hapo), tunaipenda ladha ya mint na ‘stimu’ yake inakuwa nzuri,” anasema Magdalena.

Alipoulizwa anapata wapi fedha ya kununua kilevi hicho, Magdalena anasema katika fedha za boom (fedha za kujikimu zinazotolewa na Serikali) lazima watenge kiasi kwa ajili ya starehe hiyo.

Hali ni tofauti kwa wanafunzi wa vyuo jijini Dar es Salaam, ambao wameenda mbali na baadhi yao hununua mtungi wa shisha na kukaa nao vyumbani (ghetto).

“Baada ya kuona nyumba hii tumepanga wanachuo wanne na wote tunapenda shisha tulikubaliana tuchangishane na tununue mtungi wetu,” anasema kijana aliyejitambulisha kwa jina moja la Brighton, mkazi wa Mwenge Mpakani.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini mitungi ya shisha inauzwa kuanzia Sh70,000, huku biashara hiyo ikitangazwa zaidi katika mitandao ya kijamii, hususan Twitter.

“Shisha Pipes (mabomba) mawili kwa Sh70,000, vifaa vya mitungi ya shisha vipo, Vapes na Flavour (ladha) tofauti  zinapatikana kwa mawasiliano zaidi Karibu DM (uwanja wa meseji wa Twitter na Instagram). Mikoani tunatuma,” ni tangazo lililokutwa katika moja ya ukurasa za Twitter wa wauzaji wa shisha.

Akizungumzia ununuzi wa shisha na kuvuta pamoja nyumbani, Dk Zainabu anasema hilo ni hatari zaidi kwa kuwa vifaa vya kuvutia (filta) zikiwaishia watalazimika kutumia bomba moja ambalo linaweza kuambukiza maradhi hayo.

“Hao walionunua wapo hatarini kwa sababu filta zikiisha watatumia vivyo hivyo au watakuwa wanavuta kwa kiwango kikubwa kwa sababu ipo nyumbani muda wote. Hatari kwa mapafu kuathirika ni kubwa,” anasema Dk Zainabu.


Athari nyingine za shisha

Utafiti uliofanywa na kituo cha kudhibiti na kuzuia magonjwa (CDC) nchini Marekani mwaka 2021, ulioitwa ‘uvutaji na matumizi ya tumbaku’ umetaja athari zinazoweza kusababishwa na uvutaji shisha ambao kwa majina mengine hujulikana kama narghile, argileh, hookah, hubble-bubble na goza.

Maradhi ya kuambukiza; Uvutaji wa shisha hutumia bomba ambalo watu kadhaa hushirikiana. Hali hii husababisha maradhi ya kuambukiza ya Hepatitis B (homa ya ini).

Saratani; Shisha ina wingi wa nikotini, kiwango cha kemikali za tar, carbon monoxide, metali za kiwango cha juu kama cobalt na lead ambavyo ni visababishi vya saratani.

Uraibu; Uvutaji wa shisha husababisha kutengenezwa kwa kiwango kikubwa cha nikotini kwenye damu, hivyo mtu akishazoea kuvuta hawezi kuacha kwa kuwa kilichomo kwenye shisha huvutwa kwenye neva za fahamu na kusababisha mishipa hiyo kwenye ubongo kuhisi kupata faraja na raha ya kipekee.


Takwimu athari za shisha

Takwimu za Shirikisho la Madaktari wa Mapafu Marekani (ALA) zinaonyesha mtu anayevuta shisha kwa saa moja ni sawa na kuvuta sigara 100 katika kiwango cha moshi na sumu ya nikotini anayoivuta mtumiaji husika.

ALA walifanya utafiti kubaini sababu za vijana kuvuta shisha na kubaini wengi hudhani haina madhara ikilinganishwa na sigara.

“Wanaovuta kwa sababu ya rafiki zao (asilimia 25), wanaodhani haina madhara (asilimia 21), kupumzika na kufurahia (asilimia 31) na wanaovuta kujaribu kilevi kipya (asilimia 11),” imesema ripoti hiyo.

Imeandikwa kwa udhamini wa Bill & Melinda Gates Foundation