Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Shisha, ‘visungura’ vyateketeza vijana

Dar es Salaam. Uvutaji shisha na matumizi ya pombe kali kwa baadhi ya vijana inaonekana kuwa ndiyo kwenda na wakati katika maisha.

Hata hivyo, mtindo huu wa maisha unaelezwa kuchangia ongezeko la maradhi ya moyo.

Wataalamu wa afya wanasema idadi ya wanaougua shinikizo la damu, kiharusi na maradhi ya moyo katika umri mdogo wa miaka 20 hadi 40 inaongezeka.

Awali, ugonjwa huo uliwapata zaidi watu wenye miaka 60 na zaidi.

“Uvutaji shisha na sigara huongeza mara tatu hatari ya mtu kufa mapema kutokana na ugonjwa wa moyo na kiharusi ikilinganishwa na kutovuta,” alisema Dk Upendra Bhalerao, mapema wiki hii alipotoa mada kwenye mdahalo uliowahusisha madaktari wa Tanzania na India, ulioandaliwa na taasisi ya Medeviva.

Dk Upendra, mbobezi wa upandikizaji moyo na mshauri wa magonjwa hayo kutoka Hospitali ya Jaslok iliyopo Mumbai nchini India, alisema kwa wavutaji sigara na watumia tumbaku ni rahisi kupata changamoto ya mishipa ya damu inayosababisha mshtuko wa moyo na kiharusi.

Alisema uvutaji sigara huongeza kasi ya kuziba kwa mishipa ya moyo, pia huharibu mishipa mingine ya damu.

“Wakati mishipa inayosambaza damu kwenye mikono na miguu inapoathirika, huathiri pia mzunguko wa damu. Acha kuvuta shisha au sigara,” alisema Dk Upendra.

Alisema vijana walio na shinikizo la damu, unene kupita kiasi na kisukari wana nafasi kubwa ya kupata maradhi hatari hadi utu uzima.

Dk Upendra alisema takriban asilimia 80 ya ugonjwa wa moyo wa mapema unaweza kuzuilika kwa kubadili mtindo wa maisha.

“Matumizi mabaya ya vitu, ikiwamo ulaji na unywaji usiofaa, mfadhaiko wa kisaikolojia, kifedha na maisha yanayohusiana na mtindo wa maisha yanaweza kuongeza nafasi kwa kijana kuchochea magonjwa ya moyo mapema,” alisema Dk Upendra.

Kwa mujibu wa wataalamu, vijana wengi hupata dalili za kuhisi maumivu ya kifua na mwili kutokwa jasho lakini huona ni hali ya kawaida.

Wataalamu wanaotoa tiba Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), wanasema wengi hufika hospitalini wakiwa wamepata shambulio la moyo au kiharusi, huku wakitaja chanzo kuwa shinikizo la damu la muda mrefu pasipo kugundulika na kuanza tiba.

Takwimu zilizotolewa Mei 17, mwaka huu na Wizara ya Afya zinaonyesha ugonjwa wa shinikizo la juu la damu umeongezeka kutoka wagonjwa 688,901 mwaka 2017 hadi kufikia 1,345,847 mwaka 2021, sawa na ongezeko la asilimia 95.4 katika kipindi cha miaka mitano.

Takwimu pia zinaonyesha watu watatu hadi wanne kati ya 10 wana shinikizo la juu la damu kwa uchunguzi uliofanywa katika jamii mikoa ya Pwani, Arusha, Geita, Mtwara, Lindi, Iringa na Dar es Salaam pamoja na Zanzibar.

Kwa wagonjwa wanaotibiwa JKCI ambayo ni hospitali pekee ya moyo nchini, kati ya wagonjwa 83,356 waliotibiwa mwaka 2022, asilimia 66.8 (59,022) walikuwa na tatizo la shinikizo la juu la damu.

Hii ina maana kwa kila wagonjwa 10, sita wana tatizo la shinikizo la juu la damu au madhara ya ugonjwa huu.

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo JKCI, ambaye pia ni mkuu wa idara ya utafiti na mafunzo, Dk Pedro Palangyo alisema kati ya wagonjwa wanaofika hospitalini hapo kwa ajili ya uchunguzi, asilimia 50 wamekuwa wakikutwa na changamoto ya dalili ya shambulio la moyo baada ya kuziba kwa mishipa ya damu kwenye moyo.

Alisema shambulio la moyo (heart attack) husababishwa na kuziba kwa mishipa inayopeleka damu kwenye moyo. Hata hivyo, ugonjwa huo unaweza kusababisha kusimama kwa moyo ‘cardiac arrest.’

Dk Palangyo alisema tatizo hilo huenda sambamba na magonjwa ya kuziba mishipa ya moyo kijumla.

“Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha asilimia kubwa ya watu wanaopoteza maisha wanatokea Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwamo.

Asilimia 50 ya wagonjwa wa moyo wanaugua aina hii ya ugonjwa na kisababishi ni magonjwa kama presha na kisukari, lakini chanzo hasa ni uvutaji shisha, sigara, unywaji pombe kupindukia, uzito mkubwa, kutokufanya mazoezi na ulaji uziofaa,” alisema Dk Palangyo.

Kiharusi

Dk Palangyo alisema hivi karibuni kumekuwa na wagonjwa wengi wanaopata maradhi ya Transient Ischemic Attack (TIA) ambao huja kama kiharusi kwa kuwa mgonjwa hupata dalili zote, ikiwamo kupooza kwa mbali na mdomo kwenda upande.

“Visababishi vya ugonjwa huu ni vile vile kama vya kiharusi, anayepata hii yupo kwenye hatari kubwa ya kupata kiharusi kamili kwa maana shinikizo la juu la damu lilipanda lakini halikufika juu likamletea kupooza moja kwa moja.

“Mdomo ukaenda upande kidogo au mdomo ukawa dhaifu lakini siyo kwamba umepooza na mkono ukarudi kawaida lakini akipata ya pili mara nyingi inakuwa ni ya moja kwa moja asipofuata masharti,” alisema Dk Palangyo.

Alisema kuna uhusiano mkubwa kati ya TIA na shinikizo la damu kwa kuwa presha ikipanda inategemea imefika kiwango gani.

“Mishipa midogo midogo ya damu au mikubwa ikipasuka au kuvimba zaidi kama eneo la ubongo limeathirika na mishipa ni mikubwa anapooza,” alisema.


Hatua za kulinda moyo


Dk Upendra alitaja mambo ya kufanya kulinda moyo usishambuliwe na maradhi, ikiwamo kuacha kuvuta sigara au shisha.

Kuhusu pombe, alisema matumizi ya mvinyo kiasi ni afya kwa moyo, lakini unywaji kupindukia hufanya kazi kinyume chake na kusababisha ugonjwa wa moyo.

“Kunywa mara mbili mpaka tatu kwa wiki kuna athari ya kinga kwa moyo. Unywaji pombe kupita kiasi kunaweza kuongeza shinikizo la damu na kusababisha ugonjwa wa moyo. Utafiti uligundua kuwa hatari ya shinikizo la damu huongezeka kulingana na unywaji pombe,” alisema.

Kwa upande wa lishe, alishauri ulaji matunda na mboga, nafaka zisizokobolewa, vyakula vyenye nyuzinyuzi, samaki mara mbili kwa wiki, nyama, maziwa yenye mafuta kidogo, kupunguza vyakula vyenye sukari, chumvi kidogo na kutokula kupita kiasi.

Dk Upendra alisema ni muhimu kupunguza msongo wa mawazo ambao husababisha shinikizo la damu. Katika kutekeleza hilo, alishauri kuweka vipaumbele katika maisha na kuwa na wakati wa marafiki na familia.

Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi akitoa mada katika mdahalo huo alisema ni muhimu kuzingatia uzito usizidi kwa kupanga mlo bora na kula pale mtu anaposikia njaa.

“Chakula kingi, kisicho bora na bila kipimo ni chanzo cha vitambi, uzito kupita kiasi ambao huzaa shinikizo la damu ndiyo huzalisha magonjwa ya moyo, ini na baadaye magonjwa ya figo.

“Kitu cha kwanza ni nidhamu ya kula, umekula chakula cha mchana kwa sababu una njaa au unakula tu? Pia zingatia kula mlo wa usiku saa 12 jioni ili unapolala uchakataji uwe umefanyika,” alisema Profesa Janabi.

Alisema ni muhimu kupima afya ya mwili mara kwa mara na kuwa mwangalifu katika kuangalia presha ya damu na mafuta mwilini, kupunguza uwezekano wa kupata kisukari na uzito uliozidi na kufanya mazoezi.

Kwa mujibu wa wataalamu, dalili za maradhi ya moyo ni maumivu ya kifua, upungufu wa pumzi, kukohoa, kizunguzungu, kuzirai au kukaribia kuzirai, kutetemeka kwa kifua, mapigo ya moyo kwenda mbio au mapigo ya moyo kwenda polepole.