Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

DCEA yamnasa raia wa Comoro na aina mpya ya dawa za kulevya Dar

Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo

Muktasari:

  • Mashamba ya bangi yamebainika Tabora, Shinyanga, ekari 262 zateketezwa.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imemkamata Ahmed Bakar Abdou (32), raia wa Comoro akiwa na kilo 4.623 za aina mpya ya dawa za kulevya inayotajwa kusababisha madhara ya haraka kwa mtumiaji.

 Dawa hizo zinazofahamika Methylene Dioxy Pyrovalerone (MDPV) zimekamatwa kutoka kwa mtuhumiwa huyo akiwa katika harakati za kuzisafirisha kutokea Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa leo Aprili 4, 2024 na Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo inaeleza MDPV ni dawa mpya ya kulevya iliyo katika kundi la vichangamshi inayotengenezwa kwa kutumia kemikali bashirifu.

“Dawa hii ina kemikali inayoweza kuleta madhara ya haraka kwa mtumiaji ikilinganishwa na dawa nyingine za kulevya. Pia, imeongezwa nguvu ya kilevi inayozidi cocaine, heroin na methamphetamine,” amesema.

Kamishna Jenerali Lyimo amesema, “Dawa hii ya kulevya huuzwa kwa njia ya mtandao (intaneti) na husafirishwa kupitia kampuni za usafirishaji vifurushi, hufichwa kwa kuwekwa chapa za majina bandia kama vile bath salts, Ivory wave, plant fertilizer, Vanilla Sky, na Energy.”

Mbali ya hilo, amesema mamlaka kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania  (TFS) imefanya operesheni katika mikoa mitano na kukamata kilo 54,506.553 za dawa za kulevya za shambani na viwandani.

Ametaja dawa zilizokamatwa kuwa bangi kilo 54,489.65, mirungi kilo 10.3, heroin gramu 90.93 na cocaine gramu 1.98

Mikoa iliyohusika kwenye operesheni hiyo ni Shinyanga, Tabora, Iringa, Mbeya, Arusha na Dar es Salaam.

Amesema ekari 252 za mashamba ya bangi zimeteketezwa.

“Tumebaini uwepo wa mashamba makubwa ya bangi katika hifadhi za misitu ya Ubangu mkoani Shinyanga na Mabatini mkoani Tabora, wahalifu wamekata miti katikati ya misitu na kulima bangi. Kwa ushirikiano tulioupata kutoka TFS tumeteketeza mashamba hayo na kuwakamata wahusika,” amesema.

Amewashukuru wananchi kwa kutoa taarifa sahihi kuhusu wazalishaji na wauzaji wa dawa za kulevya katika maeneo yao.

Amesema wanaendelea kushirikiana na wadau na jamii kwa ujumla, ili kufanikisha operesheni.

Kamishna Jenerali Lyimo amesema watuhumiwa 72 wamekamatwa kuhusika na dawa hizo na baadhi tayari wamefikishwa mahakamani.