Mtandao hatari wa dawa za kulevya baharini

Dar es Salaam. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imetaja mtandao wa uingizaji wa dawa za kulevya nchini unaoendelea kwa njia ya Bahari ya Hindi, huku ikieleza ilivyojipanga kimbinu kukabiliana na mtandao huo.

Kamishna Jenerali wa mamlaka hiyo, Aretas Lyimo amesema wamebaini kwa muda mrefu kumekuwa na wimbi la boti zinazotia nanga eneo la mipaka ya ukanda huru wa bahari wa kimataifa kwa ajili ya kusambaza dawa aina ya heroin kuingia mataifa ya Afrika.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili jana ofisini kwake, Lyimo alisema boti hizo hutumia vibali vya kuvua samaki ukanda huo na huonekana kwa wingi katika msimu wa Septemba hadi Desemba.

Alisema ndani ya boti hizo kwa chini zimetengenezewa eneo lingine la kuhifadhi dawa hizo. Kwa uzoefu, kila boti moja hujaza kilogramu 1,000 na kwamba wakati wote huonekana eneo hilo zikiendelea na shughuli za uvuvi wa samaki.

“Kwa hiyo Tanzania sio kweli kwamba ni hub (kituo cha kuingiza dawa za kulevya), ila nchi zote zilizopo mwambao wa bahari ya Hindi zinapokea dawa hizo kutoka nje zinasafirishwa kwa bahari, hususan heroin,” alisema Lyimo akifafanua:

“Boti hizo zinakuwepo eneo hilo kwa wingi katika msimu wake wa Septemba hadi Desemba, wakati bahari inapokuwa imetulia kwa ajili ya kuwezesha boti zinazotoka nchi za Afrika, ikiwamo Tanzania kwenda kuchukua mzigo eneo hilo. Bahari ikichafuka hizi boti haziwezi kwenda huko kina kirefu.”

Lyimo alieleza changamoto hiyo wakati takwimu za Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi za mwaka 2021/22, zikionyesha uwepo wa bandari 240 zisizo rasmi (bandari bubu), katika mwambao wa bahari ya Hindi.

“Kwa Tanzania, boti hutokea bara na Zanzibar kwenda kuchukua na dawa hizo zinazotokea Uarabuni. Biashara hiyo inafanyika kwa miaka mingi kusambaza nchi zote za Afrika. Nchi zote Afrika zinashushiwa. Tumejipanga kimbinu na tumeshakamata zaidi ya tani tatu eneo hilo.”

Alipoulizwa udhibiti katika vita hiyo, Lyimo alisema mapambano dhidi ya dawa za kulevya kidunia, yanaongozwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC), pamoja na kamisheni iliyopo Afrika.

“Lakini hawa watu wana nguvu ya kifedha, wanatumia mbinu mbalimbali kudhoofisha mamlaka na vyombo vinavyopambana na dawa za kulevya. Mbinu kubwa wanayotumia ni rushwa kwa waliopewa mamlaka, lakini wakawa hawana hofu ya Mungu na uzalendo,” alisema Lyimo.

Kwa mujibu wa ripoti mpya ya mwaka jana ya UNODC, asilimia 70 ya watu wanaopata matibabu baada ya kuathirika na matumizi ya dawa za kulevya barani Afrika wako chini ya umri wa miaka 35.


Mkakati wa bangi

Katika hatua nyingine, Lyimo alisema mamlaka hiyo imejiwekea mkakati wa kukomesha kilimo cha bangi nchini na kwamba, inahitaji angalau miaka mitatu kuanza sasa kukishughulikia, hususan kwenye mikoa sugu ya uzalishaji wa kilevi hicho.

Alitaja mkoa inayoongoza kuwa ni Mara (hasa maeneo ya Butiama, Serengeti na Tarime), Morogoro, Iringa, Ruvuma huku Kilimanjaro ikiongoza kwa mirungi.

“Arusha ni Wilaya ya Arumeru iliyoongoza, lakini hailimi tena, mashamba yote yana mazao.Mkakati ni kumaliza mikoa hiyo mwaka huu, kwa nchi nzima tunahitaji angalau miaka mitatu, kwani ni gharama na inahitaji elimu na utafiti wa kilimo ili wapate zao mbadala kulima, vinginevyo utafyeka kesho atalima tena bangi,” alisema.

Itakumbukwa mwezi mmoja baada ya kuingia madarakani, Lyimo alianzisha operesheni maalumu dhidi ya kilimo hicho.

Katika operesheni ya mkoa wa Mara Oktoba mwaka jana, ekari 807 za mashamba ya bangi, gunia 507 za bangi kavu, gunia 50 za mbegu za bangi na viwanda viwili vidogo vya kuchakata na kufunga bangi, viliteketezwa.

Mkoani Morogoro, operesheni ya siku nane maeneo mbalimbali ya wilaya za mkoa huo, kwa ujumla iliteketeza gunia 262, kilo 240 za mbegu, ekari 978 za mashamba huku watuhumiwa 18 wakikamatwa.


Kilimo mipakani

Kuhusu sababu za kulimwa mikoa ya mipakani, Lyimo alisema soko la bangi liko nje na wateja hutokea mataifa jirani.

“Ndio wanaofadhili gharama zote kwa wakulima kuanzia uzalishaji hadi wakati wa kuvuna ili waje kuchukua. Bangi inayolimwa Tanzania ni kali sana, ambayo haihitajiki viwandani. Hata kikitolewa kibali nchini, haitalimwa bangi hii, iko maalumu kwa viwandani ambayo sio kali,” alifafanua.

Kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya sura ya 95, kilimo na biashara ya bangi nchini ni kosa la jinai, hivyo kujihusisha kwa namna yoyote na bangi (kulima, kuuza, kuhifadhi, kutumia, kuichakata), ni kosa la jinai na adhabu yake inafikia hadi kifungo cha maisha jela.


Vibali, utafiti

Lyimo alifafanua kuwa wako baadhi ya Watanzania waliowasilisha maombi ya kulima bangi nchini kwa ajili ya masoko waliyopata nje ya nchi, lakini Serikali ilikataa na kisha kwenda kulima nchi jirani.

“Kuna Watanzania walikuja hapa wanaomba kibali cha kulima bangi, kuna kampuni huko nje iliwaahidi kununua,” alieleza.

Pamoja na mkakati huo, Lyimo alisema mamlaka hiyo iko kwenye maandalizi ya kufanya utafiti wa kisayansi kwa ajili ya kuondoa upotoshaji wa hoja zote zinazoibuliwa kuhusu manufaa ya bangi.

Alisema utafiti huo utafanyika kwa ushirikiano wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).

“Ni utafiti wa kawaida utakaolinganisha maeneo yanayotumia bangi na yale yasiyotumia bangi kwa kuangalia madhara na tabia zike. Kiwango cha kemikali iliyopo kwenye jani ndio kipimo cha madhara na Serikali haina mpango wa kuhalalisha matumizi ya bangi, lakini utafiti huo utaeleza kwa kina,” alisema na kuongeza:

“Lakini kwa mfano, hata ukiangalia Mkoa wa Iringa wanakotumia kwa ajili ya mboga ndio mkoa wenye matukio mengi ya watu kujiua. Mkoa wa Mara wanalima kwa wingi lakini ni miongoni mwa mikoa yenye viwango vikubwa vya umaskini, sasa manufaa yake ni nini?’’

Kwa mujibu wa DCEA, jumla ya tani 22.74 za bangi zilikamatwa mwaka 2021, ikiwa ni ongezeko la asilimia 72 ya kiasi kilichokamatwa mwaka 2020 na ikihusisha watuhumiwa 9,484.

Mirungi iliyokamatwa katika kipindi hicho ilifikia tani 10.93, ikihusisha watuhumiwa 1,395.


Makundi manne

Kuhusu ushirikiano wa umma, Lyimo alisema kiwango cha uelewa wananchi kimeongezeka na wameendelea kushirikisha makundi ya viongozi wa kimila, viongozi wa dini, vyombo vya habari na wanasiasa wanaotakiwa kutumia ushawishi wao kwa umma.

Hata hivyo, Lyimo alitoa wito kwa makundi manne yanayoweza kusaidia kumaliza vita hiyo ya matumizi ya dawa za kulevya nchini.

“Kwanza kuna kundi la viongozi wa dini ambao wana ushawishi na wakati mwingine watumiaji wa dawa za kulevya wanakuwa nao huko, pili ni kundi la wanasiasa, wazazi ambao ndio msingi wa jamii katika malezi na watumiaji wanaishi nao,” alisema Lyimo.

Akifafanua, alisema kundi la nne ni baadhi ya viongozi wa Serikali za mitaa, aliosema baadhi yao wanafikia hatua ya kushirikiana na wahalifu kuandaa na kulima mashamba ya bangi.

Lyimo alitaja athari za kitaifa zinazotokana na matumizi ya dawa hizo, ikiwamo gharama za matibabu kwa waathirika zinazotolewa na Serikali, kuchafua diplomasia ya Taifa kupitia matumizi ya dawa za kulevya, kupoteza nguvu kazi ya Taifa kwa njia ya maradhi na vifo.

“Lakini pia ongezeko la matukio ya uhalifu nchini. Kwa ushahidi tulionao ni kwamba zaidi ya asilimia 80 ya matukio ya uhalifu yanafanywa na watumiaji wa dawa za kulevya. Hata ukiuliza Jeshi la Polisi watakueleza takwimu hizo,” alisema Lyimo.

Kuhusu mageuzi ya kisera, alisema kwa sasa mamlaka hiyo iko katika maandalizi ya Sera mpya ya Kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya.

“Tayari imeshafikia katika ngazi ya mawaziri na hatua nyingine zinaendelea. Sera hiyo inaangalia maeneo mengi ya kuboresha,” alisema Lyimo.