Said Fella, Master Jay wafunguka msako wa wasanii ‘mateja’

Dar es Salaam. Wasanii wamekuwa na mitizamo tofauti kuhusu hatua ya kusakwa na kukamatwa wanaotumia dawa za kulevya, wengi wakitaka wanaohamasisha matumizi ya dawa hizo kushughulikiwa.

Wametoa maoni hayo walipozungumza na gazeti hili, ikiwa ni siku moja baada ya Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo kuwaonya wasanii wanaotumia na kuhamasisha matumizi ya dawa hizo, zikiwamo cocaine, heroin na bangi.

Lyimo alisema juzi kuwa wana orodha ya wasanii wanaotumia dawa hizo ambao wamewapa muda wa kujirekebisha kabla ya kuwashughulikia baada ya maabara ya mamlaka kukamilika.

Alisema wasanii hao wanahamasisha jamii kwa kutumia nyimbo zao, mavazi yao yanayokuwa na majani ya bangi, maneno na matendo yao yanayoonyesha dhahiri kutumia dawa za kulevya.

Meneja wa mwanamuziki, Naseeb Abdul (Diamond), Said Fella alisema kama Serikali inaona wasanii wanatoka nje ya maadili si vibaya kuchukua hatua.

“DCEA iliyoyaona imeyaona au kama kuambiwa kaambiwa, ombi langu ni atumie vyombo vyake kwa uzuri (Aretas Lyimo) ili mradi afanikishe hili, Watanzania wengi huwa tunapenda kunyooshea vidole watu, wengine wakifanikiwa wapo wanaotaka wasifanikiwe. Kikubwa ni kuwa na vyanzo vya uhakika kwenye hili,” alisema Fella, maarufu kama Mkubwa Fella.

Alisema wasanii wanapaswa kuwa makini na kufanya mambo kwa weledi na maadili ya nchi.

Mtayarishaji wa muziki nchini, Joachim Kimario maarufu kama Master Jay alisema hajui DCEA itatumia njia gani, lakini wasanii wanaotumia bangi ni wengi.

“Niwe mkweli tu, hili kwa wasanii halijaanza leo wala jana, tangu kitambo, kama watakamatwa basi waandae na jela za kutosha, maana ni wengi,” alisema.

Hata hivyo, alisema wanaohamasisha matumizi ya dawa za kulevya hawapaswi kufumbiwa macho.

“Wasanii wa sasa wengi ni kama hawaiogopi Serikali, wanafanya mambo ambayo wasanii wa zamani hawakufanya. Zamani tuliiona Serikali kama baba na mlezi wetu, lakini sana ni kama hawana hofu kabisa,” alisema.

“Wanafanya vitu ambavyo si vya maadili, wapo wengine wanafanya hadi video wakivuta bangi, hawa si wa kuwavumilia, tena wamechelewa kuwachukulia hatua stahiki za kinidhamu,” alisema.

Mwenyekiti wa Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (Chamudata), Luiza Nyoni alisema wasanii kutumia dawa za kulevya au bangi ni tatizo la kimaadili linaloanzia katika ngazi ya familia.

“Siku moja nilimuona rafiki yangu ambaye ni mwanamuziki siwezi kumtaja jina, alivuta bangi mbele ya mama yake, nilishangaa sana na mzazi wake hakumkemea, nilimuuliza akaniambia mama hana tatizo, lakini kama kuanzia ngazi za familia tungekuwa tukikemea ingesaidia,” alisema.

Alisema msanii kama kioo cha jamii anapaswa kufanya mambo ya maadili yanayoendana na taratibu za nchi.

“DCEA iko sahihi, msanii kama kioo cha jamii huwezi kutumia vitu hivyo kwenye video za nyimbo zako, hiyo ni sababu ya kuiga tu, kama tuko Tanzania hatuna budi kufuata taratibu za nchi na kuyaishi maadili yetu, huwezi bora uhame nchi ukafanyie huko ambako wanaruhusu,” alisema.