DED Gairo na wenzake waliodaiwa kuiba mabati 1,172 wayarejesha

DED Gairo na wenzake waliodaiwa kuiba mabati 1,172 wayarejesha

Muktasari:

  • Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Gairo, Asajile Mwambambale na watumishi saba wa halmashauri ya Wilaya ya Kilosa waliodaiwa kuiba mabati 1,172 wameyarejesha wilayani humo.

Morogoro. Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Gairo, Asajile Mwambambale na watumishi saba wa halmashauri ya Wilaya ya Kilosa waliodaiwa kuiba mabati 1,172 wameyarejesha wilayani humo.


Hivi karibuni, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fortunatus Muslim alieleza kuwatia mbaroni watumishi saba wa halmshauri hiyo (Kilosa) akiwemo DED huyo kabla hajahamishiwa wilayani Gairo.


Akizungumza leo Septemba 7 katika urejeshwaji wa mabati hayo, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Majid Mwanga amewaonya watumishi wa umma watakaohusika na ubadhirifu wa mali za umma kuwa hawataachwa bali hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.


Mwanga amesema wale watumishi waliokuwa wakihusishwa na wizi huo wa mabati wamerejesha na tayari yamepokelewa na kugaiwa kwenye shule zote zilizotakiwa kugawiwa mabati hayo kutokana na upungufu uliyokuwepo wa mabati.


Naye Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Kisena Mabuba amesema kwa kuwa mabati hayo yalikuwa kwa ajili ya miradi ya serikali kwemye shule za msingi na sekondari yataezekwa kwa haraka na walimu tarari wamekabidhiwa.

Soma hapa:Mkurugenzi Gairo akamatwa na polisi tuhuma wizi wa mabati
Watumishi wanaodaiwa kufanya wizi huo ni maafisa ugavi wanne na madereva watatu wa halmashauri hiyo wakituhumiwa kuhusika na wizi huo wa mabati yaliyokuwa yamehifadhiwa kwenye stoo ya halmashauri ya Kilosa kwaajili ya kuezeka shule ya msingi Mzaganza kata ya Kidete.


Baadhi ya Wananchi Wakizungumza tukio hilo, wamesema jambo lililofanywa na uongozi wa wilaya na mkoa limewapa Imani kwa uongozi huo.