DED Uvinza, mwekahazina matatani fedha za miradi
Muktasari:
- Waziri Mchengerwa atoa maagizo ya utekelezaji wa maelekezo ya Waziri Mkuu Kasim Majaliwa ya kuwasimamisha kazi Mkurugenzi na Muwekahazina Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma.
Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa amemuelekeza Katibu Mkuu wake kutekeleza maelekezo ya Waziri Mkuu Kasim Majaliwa kwa kuwasimamisha kazi Mkurugenzi na Muwekahazina kuanzia leo Septemba 21,2O23.
Uamuzi huo umetolewa baada ya Waziri Mkuu kukagua ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma wakati akiwa kwenye ziara mkoani humo huku Mkurugenzi Zainab Mbunda akikiri kuwepo kwa fedha za utekelezaji wake tangu mwaka 2021 lakini ujenzi huo bado haujakamilika.
Majaliwa alichukua hatua hiyo baada ya kukinzana kwa kauli baina ya Mkurugenzi Zainabu na mwekahazina Majid Mabanga ambaye alisema fedha hazipo kwenye akaunti ya Halmashauri.
Hata hivyo, Mchengerwa amemuelekeza Katibu Mkuu Adolf Ndunguru kuteua Ofisa atakayekaimu nafasi ya Mkurugenzi huyo na muweka hazina hadi uchunguzi utakapokamilika.
Pia, Mchengerwa amewataka Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao kwa kuzingatia thamani ya fedha na kuhakikisha inakamilika kwa wakati.
huku wakihakikisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri unafanyika kikamilifu ili kupeleka maenedelo kwa wananchi.
“Hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa watendaji watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao kikamilfu na kusababisha ucheleweshwaji wa upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi,”amesema Mchengerwa.