Demokrasia, upigaji fedha za umma vyatawala Kristimasi

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo.

Moshi. Maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), wakiongozwa na Mkuu wa kanisa hilo, Dk Fredrick Shoo wametoa salamu za Krismasi na Mwaka Mpya wa 2024, zikigusa wizi na ubadhirifu wa fedha za umma.

Mengine ni kuibuka kwa matukio ya ukatili, yakiwamo mauaji ya kutisha, mmomonyoko wa maadili, rushwa, kupungua kwa hofu ya Mungu na ustawi wa demokrasia ya vyama vingi.

Sikukuu ya Krismasi huadhimishwa duniani kila ifikapo Desemba 25, ikiwa ni kumbukumbu ya kuzaliwa Yesu Kristo.

Askofu Shoo, ambaye pia ni Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini ya KKKT, alisema Krismasi ni wakati wa kutakiana furaha, amani na upendo kwa kuwa Kristo amezaliwa na kutaka jamii ya Watanzania ikatae kwa nguvu vitendo vya ukatili.

“Tunasikia taarifa za kusikitisha kuhusu ukatili na hata mauaji miongoni mwa wanafamilia, na hawa ni Wakristo, hata mtu unajiuliza kulikoni?” alisema na kuongeza:

“Kwa wengine Ukristo umekuwa wa kuigiza tu na ushirikina umeingia hata makanisani na kuzaa chuki na magomvi kati ya ndugu, watoto na wazazi. Tunasikia habari za ubadhirifu wa mali ya umma, hasa katika halmashauri zetu, ukwapuaji umezidi,” alisema. Askofu Bagonza

Katika salamu kwa waumini, Askofu wa Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza alisema, “Kwa Kanisa kuna hukumu nzito inaelekezwa kwake juu ya mmomonyoko wa maadili katika jamii. Hofu ya Mungu imepungua sana katika jamii na dhambi inabugiwa kama chakula.

“Dhuluma inashabikiwa na haki inakejeliwa. Wasema kweli ni maadui wa Taifa na matapeli wanaitwa wazalendo na kuenziwa kama mashujaa”.

Aliongeza: “Hekalu limejificha katika sakramenti za kujenga mahekalu zaidi ambayo yamegeuka kuwa vitalu vya kuotesha na kustawisha ufisadi, dhuluma na dhambi.”

Kuhusu Taifa, Askofu Bagonza alisema kiwango cha rushwa kinawakatisha tamaa wapambanaji na kwamba badala ya kuungana kupambana na rushwa, baadhi ya watu wanapambana na wanaopambana na rushwa.

“Hata baadhi ya wananchi wanyonge nao wanadai rushwa kutoka kwa baadhi ya viongozi wao waliowachagua kwa neno ‘unatuachaje’. Hivi sasa dhambi si kutoa, kupokea wala kudai rushwa tu, bali hata kushuhudia na kukaa kimya ni rushwa,” alisema.

Alisema Taifa linahitaji mfumo mpya wa kidemokrasia unaowezesha viongozi kuogopa hukumu ya wananchi na ya Mungu na kwamba, dini imezama katika ujasiriamali wa kiroho na dhambi haikemewi.

 

Askofu Sendoro, Munga

“Mungu aendelee kutujalia ili tuzitumie vizuri mvua zinazoendelea kunyesha ili tupate chakula cha kutosha. Tunatambua kuwa katika maeneo mengine mvua hizi zimeleta maafa makubwa,” alisema Askofu Chediel Sendoro wa Dayosisi ya Mwanga ya KKKT, akitoa mfano wa maafa ya wilayani Hanang mkoani Manyara.

“Wapo wananchi 85 wamepoteza maisha na wengine kupoteza makazi. Tuwaombee faraja na msaada wa kweli kutoka kwa Mungu mwenye uweza wote. Tuendelee kumuomba atupe mvua za kiasi na zenye manufaa,” alisema.

Askofu mstaafu wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Stephen Munga alizungumzia miswada inayopendekeza marekebisho ya sheria za uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwakani na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, akitaka yafanyike kwa weledi.

Alisema: “Ili kuyafanya hayo kwa weledi kunahitajika ushauri wa hekima kwa watawala. Ushauri wa hekima ni pamoja na watawala kujua matakwa ya watu juu ya miswada ya sheria itakayotuongoza katika njia ya amani chaguzi hizo zijazo.”

Askofu Mkuu wa Kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki (KKAM), Oscar Ulotu alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kusimamia amani na kuwaleta pamoja viongozi wa vyama vya siasa.