Denmark yatangaza kufunga ubalozi wake Tanzania

Denmark yatangaza kufunga ubalozi wake Tanzania

Muktasari:

  • Baada ya kuwapo kwa takribani miongo sita, Denmark imetangaza kuufunga ubalozi wake nchini Tanzania ifikapo mwaka 2024, huku sababu zikitajwa kuwa ni kuendana na mpango wa nchi hiyo katika masuala ya kimataifa.

Dar es Salaam. Baada ya kuwapo kwa takribani miongo sita, Denmark imetangaza kuufunga ubalozi wake nchini Tanzania ifikapo mwaka 2024, huku sababu zikitajwa kuwa ni kuendana na mpango wa nchi hiyo katika masuala ya kimataifa.

Mbali na Tanzania, nchi hiyo pia itafunga ubalozi wake nchini Argentina, Ubalozi mdogo wa Chongqing nchini China na ujumbe wa biashara huko Barcelona (Uhispania) na inaelezwa kuwa jumla ya uwakilishi 16 na ofisi tisa katika makao makuu ya Wizara ya Mambo ya Nje huko Copenhagen zitaimarishwa.

Uamuzi huo ulitangazwa leo Ijumaa Agosti 27, 2021 na Waziri wa Mambo ya nje wa Denmark, Jeppe Kofod.

Waziri huyo amesema hayo ni matokeo ya sehemu ya marekebisho ya Denmark ya uwapo wa kimataifa. Amesema marekebisho haya yanajumuisha kuongezeka kwa ujumbe wa kidiplomasia uliopo na kufungwa kwa zingine.

Amesema huduma za kigeni za Denmark zinaandaliwa upya kwa kuzingatia vipaumbele vya Serikali.

“Upangaji upya unamaanisha uwakilishi zaidi utaboreshwa pamoja na mambo mengine, kazi ya Denmark katika EU, NATO, UN, Arctic, Afrika na juhudi za usafirishaji,” amesema waziri huyo na kuongeza:

“Kipaumbele changu cha kwanza kama Waziri wa Mambo ya Nje ni kuhakikisha usalama na usalama wa ndani katika ulimwengu ambao demokrasia, haki za binadamu na maadili yetu yako chini ya shinikizo. Mabadiliko haya lazima yasaidie kulenga juhudi tunazofanya nyumbani na nje ya nchi, ili tuweze kufanya tofauti kubwa iwezekanavyo,”

“Uamuzi wa kufunga Ubalozi jijini Dar es Salaam ni matokeo ya marekebisho ya vipaumbele vya serikali ya Denmark kwa ushirikiano wa maendeleo kama ilivyoainishwa katika mkakati mpya wa ulimwengu, 'The World we share',” imeeleza taarifa hiyo iliyowekwa katika tovuti ya ubalozi wa nchi hiyo Tanzania.

Amesema mkakati huo mpya una msisitizo mkubwa katika kushughulikia udhaifu, nchi zilizo kwenye mizozo au changamoto za uhamaji na uhamiaji. Barani Afrika mwelekeo zaidi utakuwa Sahel na katika pembe ya Afrika.

“Kutokana na hali hii, Serikali ya Denmark imeamua kumaliza ushirikiano wa maendeleo baina ya nchi mbili nchini Tanzania na kufunga Ubalozi wa Denmark jijini Dar es Salaam mnamo 2024 na huu haukuwa uamuzi rahisi kufikiwa,” imesema taarifa ya Ubalozi huo.

Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa Denmark itaheshimu ahadi zilizokubaliwa za kifedha na shughuli ya kufunga ubalozi imetengewa fungu ili kuhakikisha mchakato huo unakamilika vizuri.

“Denmark bado imejitolea kuendelea kufanya kazi kwa karibu na Tanzania katika ngazi ya nchi mbili na kwa kuzingatia maswala mapana ya kikanda na kimataifa,” imeeleza taarifa hiyo.

Akizungumza leo kwa simu, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk amesema bado hajapata taarifa hiyo, anaifuatilia na Msemaji wa Serikali Gerson Msingwa naye pia amesema vivyo hivyo na kuongeza kuwa Serikali ikishapata taarifa itatoa tamko.