Dereva bajaji aporomoka mteremkoni Ipogolo akiwakimbia trafiki
Muktasari:
- Bajaji 446 zikikamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Iringa kwa kukutwa na makosa mbalimbali, dereva mmoja amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa kwenye chumba mahututi kwa mada ya kuumia wakati akiwakimbia askari.
Iringa. Dereva wa bajaji aina ya TVS, Essau Kilawa amelazwa kwenye chumba cha watu mahututi (ICU), Katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa baada ya kuumia wakati akijaribu kuwakimbia polisi.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa kupitia Kitengo cha Usalama Barabarani lipo katika msako wa kuzikamata bajaji zinazovunja sheria ambapo, bajaj 446 zimekamatwa kwa kuhusika na makosa mbalimbali.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Machi 22, 2023, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi amesema dereva huyo alikutwa akiwa Ana majeraha eneo la mteremko wa Ipogolo maarufu kwa jina la kisima cha bibi huku bajaji yake ikikutwa imetelekezwa ikiwa haina funguo eneo la Kitanzini, Manispaa ya Iringa.
"Baada ya wananchi kutoa taarifa, Jeshi la Polisi lilimchukua dereva huyo na kumpeleka hospitali mpaka jana asubuhi machi 22 alikuwa kwenye chumba cha watu mahututi (ICU)," amesema Bukumbi.
"Tunavyokusimamisha ukakimbia hapo unakuwa unatukaribisha zaidi kwa sababu hatuwezi kuamini kama unakimbia kwa sababu ya kosa la bajaji ila tunaamini wewe ni mhalifu zaidi ya hayo makosa ya bajaji kwa hiyo lazima tukufatilie," amesema Bukumbi.
Ofisa Biashara Msaidizi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Mkuru Ally amesema kuwa faini ya shilingi laki moja itaendelea kuwepo kwa madereva wanaovunja sheria za usalama barabarani.
Kuhusu kamata kamata ya madereva, jeshi hilo limezikamata bajaji 446 kwa makosa mbalimbali ikiwemo kukiuka masharti ya njia, kuzidisha abiria, kuegesha maeneo yasiyo rasmi, kupakia mizigo hatarishi na kukosa leseni.
Machi 3, mwaka huu jeshi hilo lilikamata bajaj 140 kwa sababu ya kuhusika kwenye makosa hayo jambo lililosababisha kuingia kwenye mgomo ambao hata hivyo haukudumu kwa zaidi ya siku moja.
Bukumbi amesema kukamatwa kwa bajaji hizo ni mwendelezo wa oparesheni ya kuhakikisha vyombo hivyo vinazingatia sheria za usalama barabarani.
"Kama mnavyofahamu, kuna mgogoro kati ya bajaji na daladala, kwa hiyo hawa wanakuwa wanapita kwenye barabara ambazo hawaruhusiwi kupita na kusababisha daladala zishindwe kufanya kazi, msako huu utaendelea kwa bajaj zote zinazokiuka njia," amesema Bukumbi.
Kwa mujibu wa Bukumbi bajaji 25 zinashughulikiwa na watu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) kwa makosa ya leseni, baadhi wamelipa faini wameruhusiwa, bajaji 33 zimebaki kituo cha polisi zinaendelea kushughulikiwa.
Kwa upande wa Ofisa Msaidizi kutoka Mamlaka ya Udhibiti usafiri ardhini Iringa (Latra), Godfrey Calvin amesema baada ya kutoa elimu kwa madereva hao kinachoendelea kwa sasa ni kuwatoza faini wavunjaji wa sheria.
Wakizungumza na Mwananchi baadhi ya madereva bajaji leo Machi 23, 2023 wamesema wanalazimika kuzidisha abiria kwa kuwa idadi ya abiria wanayotakiwa kupakia haikidhi bei ya mafuta wanayotumia kwa raundi moja.
"Wanataka tupakie abiria watatu kwa maana hiyo tunapata 2100, kwa hao abiria watatu kwa tripu moja, mimi natoka Miyomboni kwenda Semtema, mafuta ninayotumia bei yake ni zaidi ya hiyo 2,100 ninayopata ndio maana unaona bora upakie abiria wanne ufidie kidogo mafuta," alisema dereva bajaji.