Diamond awasili Marekani kwa ajili ya tuzo za BET 2021

Diamond awasili Marekani kwa ajili ya tuzo za BET 2021

Muktasari:

  • Msanii wa Bongofleva, Diamond Platnumz tayari amewasili Los Angeles nchini Marekani kwa ajili ya tuzo za BET 2021 ambazo zinatarajiwa kutolewa kuanzia Juni 27 mwaka huu katika ukumbi wa Microsoft Theater.Dar es Salaam. Msanii wa Bongofleva, Diamond Platnumz tayari amewasili Los Angeles nchini Marekani kwa ajili ya tuzo za BET 2021 ambazo zinatarajiwa kutolewa kuanzia Juni 27 mwaka huu katika ukumbi wa Microsoft Theater.

Diamond anawaniwa katika kipengele cha Best International Act pamoja na wasanii wengine kamaWizkid, Burna Boy, Emicida, Headie, Aya Nakamura, Youssoupha na Young T & Bugsey.

Mara ya kwanza Diamond kuwania tuzo hizo ilikuwa mwaka 2014 akishindana na Mafikizolo, Sarkodie, Tiwa Savage na Davido aliyetangazwa mshindi. Akawania tena mwaka 2016 huku washindani wake wakiwa ni Wizkid, Yemi Alade, AKA, Cassper Nyovest na Black Coffee aliyeshinda.

Katika safari yake Diamond ameongozana na Meneja wake, Babu Tale ambaye amekuwa akimtumia mara zote kwa safari za Marekani, pia kasafiri na Mpigapicha wake, Lukamba.

Tuzo hizi zinazoandaliwa na Black Entertainment Television (BET) toka Juni 19, 2001 zinalenga kusheherekea mafanikio ya kazi za Wamarekani Weusi katika sanaa ya muziki, uigizaji na michezo. Mwaka 2010 ndipo walipoanzisha kipengele cha Best International Act.

Hadi sasa Mwimbaji Beyoncé ndiye anashikilia rekodi ya kushinda tuzo nyingi za BET kwa muda wote akiwa nazo 31, amechaguliwa kuwania mara 66, huku mara 58 akiwa pekee yake, na mara nane kupitia kundi la Destiny's Child.

Wasanii wengine wanaongoza kwa kushinda tuzo nyingi za BET ni Drake ambaye ana tuzo 15, Lil Wayne ana tuzo 11 na Kanye West ana tuzo 10.