Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Diwani Mbozi afariki kwa kunywa maji ya betri

Lusekelo Mwalukomo aliyekuwa diwani mteule wa kata ya Shiwinga wilayani Mbozi mkoani Songwe enzi za uhai wake.

Muktasari:

  • Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Hamad Mbega, amesema chanzo hakijajulikana, japokuwa taarifa za awali zinadai msongo wa mawazo.

Songwe. Diwani mteule wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Shiwinga, Wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe, Lusekelo Mwalukomo, amefariki dunia baada ya kunywa maji ya betri.

Tukio hilo lililotokea Novemba 26, 2025 wakati akiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Mbozi Mission.

Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Hamad Mbega, akizungumza na Mwananchi Digital leo Novemba 27, 2025 kwa njia ya simu, amethibitisha kutokea kwa kifo hicho huku akisema sababu zilizopelekea diwani huyo kunywa maji hayo bado hazijafahamika.

Mbega amesema taarifa za awali zinadaiwa kuwa ni msongo wa mawazo, lakini wataalamu wanaendelea kufuatilia kwa undani, taarifa kamili zitatolewa juu ya nini kilichosababisha kunywa maji ya betri.

“Wataalamu wetu wanaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo halisi, maana alikutwa amekunywa maji ya betri Novemba 26, 2025 saa nne asubuhi. Madaktari walifanya jitihada za kuokoa uhai wake, lakini hawakufanikiwa,” amesema Mbega.

Mkuu huyo wa wilaya amesema anajiandaa kwenda nyumbani kwa marehemu kukaa na familia ya marehemu pamoja na Chama cha Mapinduzi, ambacho diwani huyo alitokana nacho, na taarifa ya taratibu za mazishi zitatolewa baada ya kikao.

Hata hivyo, baada ya kikao hicho, mkuu huyo wa wilaya amesema mazishi yanatarajiwa kufanyika kesho, Novemba 28, 2025 nyumbani kwake Shiwinga.

Akizungumza kutoka kijijini Shiwinga, baba wa marehemu, Mchungaji Ambukege Mwasomola, amesema mwanawe alianza kuugua wakati wa michakato ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, na mara kadhaa alilalamikia kuishiwa nguvu na kukosa hamu ya kula.

Amesema marehemu alimueleza mkewe kuwa amekunywa maji ya betri alipotoka kununua mbolea, na alipelekwa hospitalini haraka baada ya hali yake kubadilika.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augostino Senga, alipoulizwa kwa njia ya simu juu ya tukio hilo, amesema hakuna taarifa ya tukio hilo iliyoripotiwa polisi.

“Sijaipokea taarifa hiyo, kama kweli angekunywa maji ya betri, kwa taratibu zilivyo lazima ingeripotiwa polisi ili kutolewa fomu kwa ajili ya matibabu. Nitaendelea kufuatilia, tukipata taarifa kamili tutaeleza,” amesema Kamanda Senga.