Diwani afariki dunia ghafla baada ya kuhutubia mkutano

Muktasari:
- Inaeleza diwani hiyo, Felix Waya wa CCM, amefariki ghafla jioni ya Mei 23, 2025 baada ya kujisikia vibaya baada ya kumaliza kuhutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika ukumbi wa Masai, kata hiyo.
Iringa. Diwani wa Kiwere, Felix Waya, amefariki dunia ghafla jana Mei 23, 2025, baada ya kumaliza kuhutubia katika mkutano wa ziara ya CCM uliofanyika katika ukumbi wa Masai uliopo kwenye kata hiyo, Wilaya ya Iringa.
Akizungumza na Mwananchi leo Mei 24, 2025, Katibu wa UVCCM Wilaya ya Iringa Vijijini, Mfaume Gomangulu, amesema kifo cha Diwani Waya ni cha ghafla na kimetikisa chama na jamii kwa ujumla.
“Baada ya Waya kumaliza kujibu maswali mbalimbali kutoka kwa wananchi katika mkutano wa hadhara, alisema anahisi hayupo sawa na akaomba kutoka nje apunge upepo.
“Lakini muda mfupi baadaye, alisema anajisikia vibaya, akapelekwa haraka katika Kituo cha afya Nzihi, lakini hali yake ilionekana kuwa mbaya zaidi na hivyo akakimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa,” amesema Gomangulu.
Dwani huyo alikuwa ni kiongozi mwenye historia ya kujitolea na utumishi kwa wananchi, ambapo alianza uongozi wake kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambako alihudumu kuanzia mwaka 2015 hadi 2020.
Baadaye alijiunga na CCM na kuchaguliwa tena kuongoza Kata ya Kiwere kwa kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025, mauti yalipomfika.
Wananchi wa Kata ya Kiwere wameeleza masikitiko yao kutokana na kifo cha kiongozi wao, kwani alikuwa mwadilifu, mchapakazi na mwenye maono ya maendeleo kwa jamii.
“Kifo cha diwani wetu kimekuwa cha ghafla na hata hatuelewi imekuaje, lakini tunamuachia Mungu, yeye ndiye mpangaji,” amesema Aziza Charles, mkazi wa Kata ya Kiwere, Wilaya ya Iringa mkoani Iringa.
Kwa mujibu wa Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa CCM Wilaya ya Iringa Vijijini, Anold Mvamba, mipango ya mazishi inaendelea kufanyika na taarifa zaidi zitatolewa kadri maandalizi yanavyoendelea.