Dizeli yaendelea kupaa, ruzuku ikiondolewa
Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetangaza bei mpya za mafuta zitakazotumika kuanzia leo Jumatano, Januari 4, 2023 huku bei ya dizeli ikiendelea kupaa.
Katika taarifa hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Modestus Lumato imeonyesha kuwa katika jiji la Dar es Salaam bei ya mafuta ya dizeli itaongezeka hadi Sh3, 295 mwezi huu ikitokea Sh 3,247 Desemba.
Kwa upade wa mikoa ya Tanga na Mtwara bei ya mafuta ya dizeli imeongezeka kwa Sh91 na Sh135 kwa lita mtawalia.
Bei ya mafuta ya petroli imepungua kidogo hadi Sh2,819 mwezi huu kutoka Sh2,827 Desemba jijini Dar es Salaam, huku ongezeko likiwa kubwa kwenye mikoa ya Tanga na Mtwara ambayo itauza mafuta hayo kwa Sh2,993 na Sh2,979 mtawalia.
Kwa mara ya kwanza baada ya miezi saba ya Serikali kuweka ruzuku kwenye bei ya mafuta nchini, hatimaye kwenye taarifa ya Ewura ya bei za Januari 2023 hakuna kipengele cha ruzuku kutoka serikalini kwa ajili ya kupunguza makali ya bei.
Mei 2022, Serikali iliweka ruzuku ya Sh100 bilioni kwa ajili ya kupunguza makali ya bei.
Julai 2022, ruzuku ya Sh100 bilioni iliwekwa na Agosti mwaka huu ruzuku ilisalia Sh100 bilioni kabla ya kuanza kushuka hadi Sh65 bilioni Septemba na Sh59.58 bilioni Oktoba, huku Novemba na Desemba hazikutajwa kiasi.
Pia, bei ya mafuta ya taa kwa bandari ya Dar es Salaam yamepungua kwa Sh49 mwezi huu hivyo lita moja itauzwa kwa Sh 3,203 kutokea Sh3,252 Desemba.