Dk Bashiru aliamsha, vijana wamshukia

Dk Ally Bashiru

Muktasari:

Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), umemwashia moto aliyekuwa Katibu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally, kwa kumtaka ajitathimini na kuomba radhi kwa madai ya kuibeza Serikali ya awamu ya sita.


Dodoma. Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), umemwashia moto aliyekuwa Katibu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally, kwa kumtaka ajitathimini na kuomba radhi kwa madai ya kuibeza Serikali ya awamu ya sita.

Kauli hiyo inakuja baada ya Dk Bashiru kuhutubia mkutano wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (Mviwata) uliofanyika juzi mkoani Morogoro, huku akisema mtandao huo si chombo cha kutoa shukrani kwa yeyote yule, bali ni chombo cha kudai haki na heshima.

Alisema mtandao huo sio chombo kidogo na kuwataka wanachama wake kuulinda na kuurithisha kwa vizazi vingine kimsimamo, na kwamba wakifikia hatua hiyo, hata changamoto wanazozizungumzia zitapungua.

“(Mviwata) si chombo cha kusifu, si chombo cha kushukuru, tunakushukuru kwa fedha hizi, tunakushukuru kwa kazi hizi, mkianza kazi ya kushukuru kwa haki yenu, hamna maana,” alisema Dk Bashiru ambaye ni mbunge wa kuteuliwa na Rais.

Akizungumza juzi jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa UVCCM, Kenani Kihongosi alisema Dk Bashiru alizungumzia maneno ambayo si ya kiungwana na yamejaa ukakasi na yamelenga kwenda kuichonganisha Serikali na wananchi hasa wakulima.

Alisema ileweke kuwa Serikali ya awamu ya sita imefanya kazi kubwa inayoenda kuacha alaDsma kwa Watanzania ikiwemo kuweka ruzuku katika mbolea ili kupunguza bei ya pembejeo hiyo nchini.

Alisema pia Serikali imetoa vitendea kazi, pikipiki, vipima udongo na kuongeza bajeti ya sekta ya kilimo, lengo likiwa ni kusaidia kukuza uchumi hasa katika sekta ya kilimo nchini.

“Sasa inapotokea kiongozi ambaye ana dhamana kubwa anatoa maneno yenye ukakasi na kusema viongozi hawapaswi kupongezwa bali wanapaswa kutolewa matamshi ya kuwashinikiza ili waweze kuwatendea wakulima, hiyo siyo sawa,”alisema Kihongosi.


Kauli zaidi za Dk Bashiru

Akiwa katika mkutano huo, Dk Bashiru aliyeweka rekodi ya kuwa Katibu Mkuu Kiongozi aliyedumu kwa muda mfupi katika wadhifa huo, alisema: “...hata watawala shibe zao, posho zao, raha zao pamoja na usalama wao havipo bila wakulima.”

Kadhalika alieleza hata kionachoitwa amani, utulivu, mshikamano, umoja havipo kama jamii ya wakulima imekata tamaa.

“Mshikamano wenu uweze kufikisha ujumbe kwa hao wanaotuongoza, kauli zenu na misimamo yenu iwatishe ili wawe upande wenu,”alisema.

Aliongeza kwa kusema sauti ya wakulima iwatishe aliowaita wanyonyaji na kama hawajafika kwenye hatua hiyo ya kuwa watu au kundi la kutisha wanyonyaji, bado watakuwa hawajafikia malengo.

“Hatutakuwa tofauti na mawakala wao wanaowapamba na wakati mwingine kuwadanganya kwamba unaupiga mwingi,” alisema.

Kwa upande wake, Kihongosi aliendelea kusema kuwa anapotokea mtu na kufifisha jitihada za Serikali, akadhalilisha Serikali, akadhalilisha viongozi wa Taifa na kuwataka wananchi hasa Mviwata waende kuishinikiza Serikali yao, wao kama UVCCM wanaona si sawa.

“Tunamtaka ndugu Bashiru kujitazama na kujitathimini, hiki anachokipanda kina faida gani kwa Taifa letu…Inapofikia mtu asione haya yote yanayofanyika maana yake huyu ana ajenda yake ya siri ama ana mkakati anaoujua yeye wa kwenda kuichonganisha Serikali na wananchi ambao inawaongoza,”alisema kiongozi huyo.

Alisema wajibu wao kama umoja wa vijana ni kuilinda Serikali, viongozi wa chama na Serikali hivyo, hawatamvumilia mtu wa aina yeyote ile.