Dk Bashiru aonya, ‘wapayukaji’ ndani ya CCM hawatavumiliwa

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally (kulia) na viongozi mbalimbali wa chama hicho wakiomba dua katika kaburi la Rais wa kwanza Zanzibar, Shekh Abeid Amaan Karume lililopo Kisiwandui Mjini Unguja. Bashiru yupo katika ziara maalum ya siku nne ya kujitambulisha kwa WanaCCM Zanzibar. Picha na Haji Mtumwa

Muktasari:

  • Waelezwa wanatumika kukidhoofisha badala ya kuendelea kusimamia na kuulinda uhuru

Zanzibar. Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema chama hicho kimejipanga kuanza kuchukua hatua dhidi ya mwanachama au makundi yenye tabia ya kukidhoofisha kwa kukisema vibaya kinyume na uhalisia.

Alisema chama hicho kimeumizwa na tabia hiyo mbovu isiyokubalika aliyoifananisha na ugonjwa wa saratani.

Dk Bashiru alitoa kauli hiyo alipojitambulisha kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi ofisini kwake mjini Zanzibar ikiwa ni sehemu ya ziara yake visiwani hapa.

Alisema kinachohitajika wakati huu ni kuimarishwa kwa chama hicho chenye uwezo wa kuendelea kulinda na kusimamia uhuru na ukombozi wa taifa.

Katibu huyo mkuu alisema katika mwelekeo wa uendelezaji wa CCM imara iliyoanza kurejesha imani kwa wananchi wengi, suala la makundi limefikia kikomo na kwamba, linatakiwa kuepukwa kwa vile ni sawa na najisi kwa watu wenye imani za kidini.

Dk Bashiru alisema CCM kamwe haitokubali kushindwa na makundi ya watu wasiokuwa na mwelekeo wa ulinzi wa ukombozi wa chama na taifa.

“Katika utumishi wangu wa chama kwa nafasi ya utendaji mkuu sitakubali kuchafuka wala kuchafuliwa, wala kuwachafua viongozi wetu wakuu walioniamini kunipa utumishi huu muhimu kwa chama chetu,” alisema Dk Bashiru.

Pia, Dk Bashiru aliwataka viongozi waliopewa fursa za kuwatumikia wananchi hasa majimboni kuacha tabia ya kupayuka hovyo.

Kuhusu utekelezaji wa Ilani ya CCM, Dk Bashiru aliwaagiza watendaji wa Serikali kuendelea na uratibu utekelezaji wa ilani.

Alisema kwamba ripoti ya utekelezaji huo wa ilani utakaoainishwa kwa pamoja na Serikali zote mbili utapaswa kuwasilishwa katika uongozi wa juu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM.

Katibu mkuu huyo alisema katika kufanikisha maendeleo alishauri Kamati Maalumu ya CCM Zanzibar iendelee kupewa nafasi yake katika masuala ya kisiasa yanayohusu visiwa hivyo.

Awali, Balozi Iddi ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, alisema Zanzibar kisiasa iko salama licha ya upinzani mkubwa unaojitokeza wakati wa uchaguzi mbalimbali unaohusisha vyama vya CCM na CUF.